Wahandisi sasa kutumikishwa jeshini Korea Kusini

Korea Kusini Haki miliki ya picha AP
Image caption Raia huhudumu miaka miwili jeshini Korea Kusini

Korea Kusini imetangaza kwamba wanafunzi wanaosomea uhandisi na sayansi, ambao awali walikuwa hawashurutishwi kuhudumu jeshini, wataondolewa nafuu hiyo.

Serikali imesema hatua hiyo imetokana na kupungua kwa idadi ya watu.

Nchini humo, huwa ni lazima kwa kila raia kutumikia miaka miwili jeshini.

Watu wa makundi hayo mawili hata hivyo walikuwa hawalazimishwi kuhudumu katika jeshi ili kusaidia katika ukuaji wa sekta ya viwanda nchini humo.

Afisa wa wizara ya ulinzi ameambia shirika la habari la Yonhap kwamba nafuu hiyo itaondolewa kufikia 2023, kutokana na uhaba wa wanajeshi.