200 wahofiwa kuzikwa ardhini Sri lanka

Sri lanka Haki miliki ya picha EPA
Image caption Shughuli za uokozi zikiendelea kufuatia maporomoko ya udongo nchini Sri lanka

Wahudumu wa uokozi nchini Sri Lanka wanasaka watu kadhaa waliotoweka baada ya maporomoko makubwa ya ardhi yaliyofuatia mvua iliyonyesha kwa siku kadhaa

Shirika la msalaba mwekundu linasema zaidi ya familia 200 zinahofiwa kuzikwa kwenye matope katika vijiji vitatu vya wilaya ya kati ya Kegalle.

Takriban miili 13 imebainika hadi sasa. Miili mingine mitatu ilipatikana katika maeneo mengine ya wilaya hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Takwimu rasmi zinasema watu 32 wamekufa kutokana na maporomoko ya ardhi Sri lanka

Maafisa wanaohusika na majanga wanasema kuwa watu wapatao 150 wameokolewa lakini nyumba 60 zimezikwa kwa chini ya matope.

Watu wapatao 32 wamekufa katika mafuriko wakati wa siku yayu za mvua za masika nchini Sri Lanka, kwa mujibu wa takwimu rasmi.

Karibu watu 350,000 wameyahama makazi yao kufuatia mafuriko.

Maporomoko makubwa zaidi yalitokea juu ya vijiji vya Siripura, Pallebage na Elagipitya Jumanne asubuhi na mchana.