Clinton: Siwezi kushindwa na Bernie Sanders

Clinton Haki miliki ya picha Getty
Image caption Clinton anahitaji wajumbe 90 kupata ushindi

Mgombea urais anayeongoza katika chama cha Democratic nchini Marekani Hillary Clinton amesema haiwezekani iwe kwamba hatakuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba.

Katika mahojiano na kituo cha runinga cha CNN, amesema anajivunia uongozi mkubwa mbele ya mpinzani wake wa pekee Bernie Sanders.

"Nitakuwa mgombea wa chama change,” ameambia CNN.

“Hilo limekamilika tayari, kimsingi. Haiwezekani hilo lisitokee.”

Bi Clinton ana idadi kubwa ya wajumbe, wajumbe 2,293 na anahitaji wajumbe 90 pekee kujihakikishia ushindi.

Seneta wa Vermont Bernie Sanders naye ana wajumbe 1,533 na anahitaji wajumbe 850 kushinda.

Lakini maafisa wa Sanders wanasema Bi Clinton hafai kudhani kwamba tayari ameshinda, wakitaja ushindi wa karibuni wa Bw Sanders katika majimbo ya Indiana, West Virginia na Oregon.

Haki miliki ya picha AP

Kwenye mahojiano hayo na CNN, Bi Clinton pia amemkosoa mgombea mtarajiwa wa chama cha Republican Donald Trump akisema hajahitimu kuwa rais wa Marekani.

Amesema mfanyabiashara huyo tajiri kutoka Marekani ni hatari kwa demokrasia Marekani na kwamba msimamo wake kuhusu sera ya kigeni ni hatari sana.