Ban Ki-moon ataka nchi zipunguze wakimbizi

Wakimbizi Haki miliki ya picha AP
Image caption Ban anataka serikali zichukue hatua kupunguza wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezihimiza serikali kuchukua hatua kupunguza idadi ya watu waliofurushwa makwao.

Amesema lengo linafaa kuwa kupunguza idadi ya watu waliotoroka makwao kwa asilimia 50 katika kipindi cha miaka 15 ijayo.

Bw Ban amekuwa akihutubia mkutano mkuu wa kimataifa kuhusu migogoro ya kibinadamu na utoaji misaada ambao unaendelea mjini Istanbul.

Mkutano huo umewaleta pamoja wanasiasa na maafisa wa mashirika ya misaada kutoka nchi zaidi ya 150.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema mfumo wa sasa wa kushughulikia wakimbizi unafaa kutathminiwa upya kwani haukidhi mahitaji kikamilifu na kwamba nchi zaidi zinafaa “kubeba mzigo” wa wakimbizi.

Amesema taifa lake kwa sasa lina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, zaidi ya milioni 3 kutoka Syria na Iraq.

Haki miliki ya picha epa
Image caption Maafisa kutoka nchi 150 wanahudhuria mkutano huo

Huku misaada ya kimataifa ikizidi kufifia kila uchao hasa katika miaka ya hivi karibuni, mkutano huo wa siku mbili una nia ya kujaribu kuwaleta pamoja wadau kote duniani ili kutathmini namna ya kupunguza au kuwaondolea kero waathiriwa hao ambao ni wakimbizi, wengi wao wakikataliwa hata katika mataifa wanayokimbia kutafuta hifadhi.

Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto anawakilisha taifa la Kenya katika mkutano huo, huku shinikizo likizidi kutolewa kwa Kenya ambayo tayari imetangaza kufungwa kwa kambi za wakimbizi nchini humo.