Muhtasari: Habari kuu leo Jumatatu

Miongoni mwa habari kuu leo, Iraq imeanza vita vya kuukomboa mji wa Falluja kutoka kwa Islamic State na Rais Obama amesema hataiomba msamaha Japan.

1. Iraq yaanza operesheni ya kukomboa Falluja

Haki miliki ya picha AFP

Waziri mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi, ametangaza kuwa kuanza kwa operesheni kali ya kijeshi yenye nia ya kuutwaa tena mji wa Falluja, kutoka kwa wapiganaji wa Islamic State, walioutwaa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, zimeanza.

Jeshi pamoja na polisi wametumwa kuuzingira mji huo.

Mamlaka kuu nchini Iraq awali ilikuwa imetoa tahadhari ya kuwaonya maelfu ya raia, wengi wao familia ya wapiganaji hao wa IS, kuondoka mjini humo kabla vita vikali havijaanza.

2. Bunge Ugiriki laidhinisha mageuzi ya kiuchumi

Haki miliki ya picha .

Bunge la Ugiriki limeidhinisha mageuzi kadhaa ya kiuchumi na fedha baada ya mjadala mkali wa dharura uliochukua siku nne.

Bunge limepitisha uamuzi huo, katika hatua zake kali zinazoendelea, kuokoa uchumi wa nchi hiyo.

Waziri mkuu Alexis Tsipras amesema matokeo hayo yanaonesha kuwa Ugiriki inaheshimu ahadi ilizotoa kuhusu uchumi wake.

Amesema ana imani sasa wakopeshaji wake wa - Eurozone sasa wataipa Athens mkopo wa pesa inazohitaji.

3. Kampuni kuu ya bima yajitenga na tumbaku

Haki miliki ya picha Reuters

Kampuni kubwa zaidi ya bima duniani AXA, inasema kuwa inajiondoa kabisa kutoka kwa rasilimali za aina yoyote zinazohusiana na tumbaku.

Inasema rasilimali hizo zinakisiwa kuwa za thamani ya dola bilioni moja nukta moja ya mtaji.

Kampuni hiyo imesema kwa si busara kuendelea kuwekeza katika sekta ambayo Shirika la Afya Duniani limekadiria itasababisha vifo vya mamilioni ya watu karne hii.

4. Upinzani kuandamana tena Kenya

Haki miliki ya picha Reuters

Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya-CORD, umetangaza kuendelea na maandamano ya upinzani hii leo Jumatatu, kama ilivyopangwa ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kutaka kuvunjiliwa mbali kwa tume ya uchaguzi nchini humo, IEBC, kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Maandamano kama hayo yaliyofanyika Juma liliopita, yaliambatana na ghasia ambapo polisi walishutumiwa kwa vitendo vya ukatili.

5. Obama awasili Vietnam kwa ziara rasmi

Haki miliki ya picha Mike Theiler Pool Getty Images

Rais Barack Obama amewasili nchini Vietnam, katika mwanzo wa ziara yake ya wiki moja barani Asia. Maafisa wakuu wa Marekani wanasema kuwa nia ya ziara hiyo ni harakati za kuboresha ulinzi na uchumi, kati ya maadui hao wawili wa jadi, huku ikielezea hitaji la Marekani dhidi ya rekodi ya ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini Vietnam.

6. Obama asema hataiomba msamaha Japan

Haki miliki ya picha Getty Images

Rais Barack Obama amesema kuwa hataomba msamaha kwa Japan kuhusiana na tukio la kushambulia miji yake miwili ya Hiroshima na Nagasaki kwa mabomu ya atomiki.

Amesema kuwa kuomba msamaha sio muhimu kwani wakati wa vita, viongozi hufanya "maamuzi ya aina yoyote".

7. Walinzi Libya wabeba maboti yenye wahamiaji 850

Haki miliki ya picha Libyan Coastguard

Na walinzi wa pwani nchini Libya wanasema kuwa wamezuia na kunasa maboti yaliyokuwa yamewabeba wahamiaji 850 Waafrika, waliokuwa wakivuka kujaribu kuingia bara Ulaya.

Afisa mmoja aliyetambuliwa kama Kanali Ayoub Qassem, amesema kuwa miongoni mwa wahamiaji hao kulikuwa na wanawake 11 waja wazito.

Inakisiwa kuwa, mwaka huu pekee, zaidi ya wahamiaji wapatao 30,000 wameingizwa kimagendo kupitia njia ya mkato ya katikati mwa bahari ya Mediterranean hadi Italia.