IAAF yaongeza marufuku kwa maafisa Kenya

Image caption Mwenyekiti wa zamani Isaiah Kiplagat, naibu wake David Okeyo na mweka hazina wa zamani , Joseph Kinyua wamepigwa marufuku ya miezi 6 zaidi

Shirikisho la riadha duniani (IAAF) limeongeza muda wa marufuku iliyowapa maafisa wakuu watatu wa shirikisho la riadha la Kenya kwa zaidi ya miezi sita zaidi.

Mwenyekiti wa zamani Isaiah Kiplagat, naibu wake David Okeyo na mweka hazina wa zamani , Joseph Kinyua wataendelea kutumikia kipindi hicho kipya cha siku 180 ilikuipa kamati maalum inayoendesha uchunguzi dhidi yao muda zaidi kukamilisha shughuli yake.

Watatu hao walikuwa wamepigwa marufuku ya miezi 6 tangu tarehe 30 Novemba mwaka uliopita kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa mali ya umma matumizi mabaya ya madaraka yao mbali na ufisadi.

Mchunguzi mkuu bwana Sharad Rao alinukuliwa na jarida la Citizen akisema kuwa bado hawajamaliza uchunguzi.

''Kwa hakika hatujamaliza uchunguzi hususan kuhusiana na madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za ufadhili kutoka kwa kampuni ya kutengeza bidhaa za michezo ya Nike.

''Hatuja kamilisha mazungumzo na shirikisho la riadha la Qatar''

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kiplagat, Okeyo na Kinyua wanadaiwa kupunja takriban dola nusu milioni fedha zilizotolewa na Nike kukuza riadha nchini Kenya.

''Aidha hatujapata fursa ya kuwahoji mashahidi kadhaa''

Kutokana na hilo tukaomba muda zaidi kutoka kwa kamati ya maadili alisema bwana Rao.

Afisa wa nne wa shirikisho hilo bw Isaac Mwangi angali anatumikia marufuku ya miezi sita itakayokamilika mwezi Agosti.

Kiplagat, Okeyo na Kinyua wanadaiwa kupunja takriban dola nusu milioni fedha zilizotolewa na Nike kukuza riadha nchini Kenya.

Kiplgat vilevile anakabiliwa na tuhuma za kupokea hongo ya magari mawili kutoka kwa shirikisho la riadha la Qatar ilikuwapigia kura wakati wa kongamano la kutoa zabuni ya uwenyeji wa mashindano ya riadha ya dunia ya 2019.