Kurasa za Mark Zuckerberg zimedukuliwa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kurasa za Mark Zuckerberg zimedukuliwa

Kurasa za mitandao za kijamii za bwenyenye mwanzilishi wa Facebook Mark Zuckerberg zimedukuliwa.

Kurasa za mtandao wa Instagram, Twitter, LinkedIn na ule wa Pinterest zilidukuliwa na kutekwa kwa muda siku ya jumapili kabla ya wataalamu wa usalama wa mitandao kumudu kuzidhibiti saa chache baadaye.

Kundi la wadukuzi la Ourmine limedai kudukua akaunti za Zuckerberg.

Kundi hilo lilijidai kwenye ujumbe waliochapisha kwenye mtandao wa Twitter kuwa ndio waliodukua kurasa hizo na wakamtaka

Zuckerberg awatumie ujumbe wa moja kwa moja iwapo alikuwa anataka umiliki wa akaunti hizo.

"Vipi @finkd tumedukua kurasa zako za Twitter , Instagram, Pinterest, tupigie iwapo unataka tukurudishie''

Image caption kurasa za Mark Zuckerberg zimedukuliwa

Ujumbe huo hata hivyo umefutwa kwa sasa.

Japo anaimiliki ukurasa huo Zuckerberg hajachapisha ujumbe wowote tangu mwaka wa 2012.

Mbunifu Ben Hall alichapisha picha ya ukurasa wa bwana Zuckerberg wa Pinterest uliodukuliwa.

BBC inafahamu kuwa muundo wa usalama wa kampuni ya Facebook ndiyo iliyowazuia wadukuzi hao kuteka ukurasa wake wa Instagram.

Mtandao huo wa kijamii unaotumika kuchapisha picha unamilikiwa na Facebook.

Wandani wa maswala ya usalama wa mitandao ya Intaneti wanadai kuwa huenda udukuzi wa mwaka wa 2012 wa ukurasa wake wa LinkedIn ndio uliochangia tukio hilo la jana.