Uchaguzi Mkuu Uingereza kufanyika Mei 6

Viongozi wakiwa katika mdahalo
Image caption Huu ni uchaguzi wa kwanza nchini Uingereza kuwapambanisha viongozi wa vyama vikuu vitatu katika midahalo kwenye televisheni.

Uchaguzi mkuu wa Uingereza utafanyika tarehe 6 mwezi Mei katika majimbo 650 kuchagua wabunge. Uchaguzi wa jimbo moja la Thirsk and Malton umeahirishwa mpaka tarehe 27 Mei kutokana na kifo cha mgombea wa chama cha UKIP, John Boakes. Chama cha UKIP kitatakiwa kuteua mgombea mpya aweze kuwania kiti hicho kwa muda uliopangwa.

Uchaguzi mkuu kwa kawaida unalihusu bunge la makabwela (House of Commons), wabunge wa bunge kubwa (House of Lords) wao hupatikana kwa kuteuliwa. Mwaka huu majimbo 650 yatagombaniwa, idadi iliyoongezeka kutoka 646 katika uchaguzi wa 2005.

Uchaguzi ulitangazwa tarehe 6 Aprili, na bunge lilivunjwa tarehe 12 Aprili kutoa fursa kwa kampeni za uchaguzi kuanza. Kwa mujibu wa sheria, uchaguzi utaanza saa moja asubuhi majira ya Uingereza mpaka saa nne usiku. Katika baadhi ya maeneo pia kutakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mikakati kushinda viti vingi

Chama tawala cha Labour Party kinapigania kupata ushindi wa nne mfululizo na kujenga upya imani waliyojijengea kwa wapiga kura tangu mwaka 1997. Chama cha Conservative kinajaribu kuwapiku Labour kujijenga katika nafasi nzuri ndani ya siasa za Uingereza, baada ya kushindwa kufurukuta kunako miaka ya 1990. Lengo lao kuu ni kuiengua Labour kama chama tawala.

Wapinzani wengine Liberal Democrats wanatumai kunufaika kutokana na makosa ya Labour na Conservative; vyovyote itakavyokuwa, shabaha yao inaweza kuwa kuainisha viti bungeni katika bunge linalotarajiwa kukosa chama kimoja chenye idadi ya viti kuunda serikali bila kuhitaji usaidizi wa chama kingine.

Vyama vidogo

Scottish National Party, baada ya matokeo mazuri ya 2007 katika bunge la Uskochi, wamejiwekea malengo ya kunyakua viti 20 na pia watakuwa wakitumai kujikuta katika nafasi ya kuweka uwiano wa madaraka. Sawia na hilo, chama cha Plaid Cymru pia kinakusudia kupata mafanikio huko Wales.

Vyama vidogo vilivyopata mafanikio katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi wa bunge la Ulaya 2009 (United Kingdom Independence Party, Green Party, British National Party) vitajipanga kuongeza idadi ya viti vya uwakilishi katika bunge la makabwela (House of Commons). Chama cha Democratic Unionist kitakuwa kikitarajia kubakiza, kama siyo kuongeza idadi ya viti, kwa sasa ni chama cha nne kwa ukubwa bungeni.

Himaya mpya kwa viongozi

Huu ni uchaguzi wa kwanza kwa kiongozi wa Labour, Gordon Brown akiwa Waziri mkuu, baada ya kuchukua hatamu hiyo mwaka 2007 kutokana na kujiuzulu kwa Tony Blair. Pia ni mara ya kwanza kwa viongozi wa upinzani David Cameron wa Conservative na Nick Clegg wa Liberal Democrats.

Kwa maana hiyo, ni mara ya kwanza tangu mwaka 1979 ambapo viongozi wa vyama vyote vitatu vikuu wanaingia katika uchaguzi wakiwa hawajawahi kuongoza vyama vyao katika uchaguzi mkuu mwingine.

Jambo jingine jipya katika uchaguzi mkuu 2010, ni midahalo ya viongozi wa vyama vitatu vikuu ambayo imekuwa ikifanyika kwenye televisheni. Tayari kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, Nick Clegg, amepata umaarufu kutokana na uwezo wake wa kujieleza dhidi ya wenzake Gordon Brown na David Cameron.

Endapo kura za maoni zinatokana na midahalo hiyo litakuwa ni jambo la kuaminiwa, basi chama cha Liberal Democrat kimejiweka katika nafasi nzuri ya kuongeza viti, lakini pia itafanya bunge lizidi kuwa na mchanganyiko wa nguvu za vyama.