Chama cha Conservative

Chama cha Conservative kinaweza kujivunia sifa ya kuwa chama kikongwe zaidi barani Ulaya.

Image caption Chama cha Conservative kinamtegemea David Cameron wakati Uingereza inashuhudia uchaguzi wenye upinzani mkali wa vyama vikuu vitatu vya kisiasa.

Mnamo karne ya 17, waasisi wake, wakijulikana kama Tories, walikuwa wakiunga mkono utawala wa kifalme kama njia moja ya kudhibiti madaraka ya bunge na mikakati ya wapinzani wake, wakijulikana kama Whigs.

Kundi hilo la Whigs lilitawala bunge kwa miaka mingi ya karne ya 18 hadi William Pitt alipochaguliwa Waziri mkuu mwaka 1783. William aliunga mkono mfumo wa biashara huria na sera kabambe za kifedha. Mtazamo huu ndio ulijenga msingi wa kukibadilisha chama cha Conservative kuwa chama cha kisasa. Kilipinga hatua zozote za serikali kuingilia biashara binafsi. Jina Conservative, lilitumika kwa mara ya kwanza mwaka 1830 ingawa lile lingine, yaani Tory ambalo linamaanisha ‘haramia’ au ‘muasi’ lingali linatumika mpaka sasa. Mnamo karne ya 19, chama hicho kilikumbwa na mgawanyiko kuhusu uamuzi wa Waziri mkuu Sir Robert Peel kuondoa sheria ambayo ilidhibiti bei ya vyakula katika kiwango cha juu. Kwa upande mmoja kuna wale ambao waliunga mkono sera za soko huria lakini kwa upande mwingine kulikuwa na wale ambao walitetea maslahi ya wakulima. Wakati wa uongozi wa Benjamin Disraeli chama cha Conservative kiliungana kuitetea ajenda ya kuinua nafasi ya Uingereza duniani huku kikiendelea kuimarisha maisha ya maskini. Wakati chama cha Liberal kilipomeguka kwa kutoelewana kuhusu utawala wa ndani wa Ireland mnamo mwaka wa 1886, chama cha Liberal Unionist kiliundwa. Liberal Unionist kilishirikiana na Tories kabla ya kuungana kikamilifu mnamo mwaka wa 1912. Hili ndilo chimbuko la jina kamili la chama cha wahafidhina la Conservative and Unionist Party.

Ni chama ambacho kimekuwa kikihusishwa sana na wenye mashamba, mabwenyenye na watu wenye pato wastani. Lakini sasa kinajaribu kuwavutia watu wa matabaka yote ya kipato.

Miaka ya vita

Mnamo miaka ya 1930 utawala wa mawaziri wakuu ulikumbwa na changamoto ndani ya nchi na ng’ambo. Kwa mfano, Waziri mkuu Stanley Baldwin, alikabiliwa na hatua ya ghafla ya Mfalme Edward wa nane kuasi mamlaka yake. Wakati wa Waziri mkuu Neville Chamberlain, chama chake kilijaribu kujipendekeza kwa kiongozi dhalimu Adolf Hitler. Wakati vita vya dunia vilipozuka, Winston Churchill alibeba jukumu la kuokoa serikali ya chama chake na taifa la Uingereza. Churchill alikuwa akieleza sifa ya Uingereza kama nchi ambayo hupigania haki zake bila kukata tamaa. Alitukuka kama kiongozi shupavu zaidi kuwahi kukiongoza chama cha Conservative. Lakini Conservative walipigwa na butwaa wakati chama cha Leba kilipopata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa 1945. Hata hivyo, baada ya matatizo mengi na nyakati ngumu za miaka ya 1930, kulikuwa na haja ya mabadiliko. Conservative walirejea madarakani mnamo mwaka wa 1951 ambapo walitawala kwa miaka 13. Wakati mmoja, Waziri mkuu Harold MacMillan ambaye alichaguliwa mwaka 1957 alijigamba kwamba utawala wa Conservative ulukuwa umewaletea Waingereza ustarabu. Lakini miaka saba baadaye, mdororo wa uchumi ulizuka na kukisomba chama Conservative. Harold Wilson wa Leba alichaguliwa Waziri mkuu.

Utawala wa Thatcher

Ilibidi Conservative wasubiri hadi 1970 wakiongozwa na Edward Heath, utawala ambao ulidumu kwa miaka minne tu na kupokonywa tena na Leba. Mwaka wa 1979 ulikuwa wa kihistoria kwa Uingereza. Waziri mkuu wa kwanza mwanamke, Bi Margaret Thatcher alichaguliwa. Thatcher hakusita kuzozana na vyama vya wafanyakazi pamoja na kuendeleza sera zake za kubinafsisha mashirika ya serikali. Huku nyumbani kukiteketezwa na migomo ya wafanyakazi hasa wa migodi ya makaa ya mawe, sifa za Bi Thatcher katika safu za kimataifa ziliendelea kung’aa. Aliongoza vita vya kuwatimua wanajeshi wa Argentina kutoka kwenye kisiwa cha Falklands. Vishindo vyake na mbwembwe zake ziliwafanya watu kumbandika jina la utani kama, Iron Lady. Thatcher alilazimika kuondoka madarakani kufuatia ugomvi katika chama chake mwenyewe. John Major alirithi wadhifa huo na kuhakikisha chama cha Conservative kinashinda uchaguzi wa 1992 ingawa kwa kura chache zaidi. Mjadala kuhusu nafasi ya Uingereza katika Muungano wa Ulaya uliendelea kuwa tatizo sugu katika chama cha Conservative. Huku wimbi la sintofahamu likiwazungusha vigogo wa Conservative, John Major aliamua liwe na liwalo. Mwaka wa 1995 alitangaza kujiuzulu kwake huku akiwakemea wakosoaji wake kuhimili au wafunge domo. Major alichaguliwa tena kama waziri mkuu lakini kelele ndani ya chama hazikukoma. Major alizindua kauli mbiu ya kuzingatia maadili mema katika jamii lakini kashfa za mawaziri wake wenye mienendo mibovu zilitanda. Kuna wale ambao walipokea rushwa ili kuuliza maswali fulani bungeni. Conservative walianguka kwa kishindo katika uchaguzi wa 1997. Katika jitihada za kunyanyuka, chama hicho kilimchagua William Hague kama kiongozi. Lakini alishindwa kutikisa umaarufu wa chama cha Leba chini ya uongozi wa Tony Blair. William Hague alifunga virago na Iain Duncan Smith akajitosa kitini. Naye pia akashindwa kumdhibiti Blair. Duncan Smith aliondoka na kumpisha Michael Howard. Lakini wakati wa uchaguzi wa 2005, mambo yalibaki yale yale. Conservative walishindwa ingawa umaarufu wa chama tawala cha Leba ulikuwa umeanza kupungua, hasa kutokana na vita vya Iraq. Licha ya shinikizo za kuendelea kukiongoza Conservative, Howard alisema umri haungemwezesha kukiongoza chama chake hadi kwenye uchaguzi utakaofuata.

Uongozi mpya

Mlango wa Conservative ulibaki wazi kumkaribisha David Cameron akiwa na umri wa miaka 39. Azma yake ya awali ilikuwa ni kubadilisha sura ya Conservative na kukipamba kuwa chama cha kuvutia, chenye kuzingatia maswala ya mazingira na chenye kujali maslahi ya Mwingereza wa kawaida. Alianza kuwalenga vijana na wanawake. Matokeo yakaanza kudhihirika wakati sifa za Conservative zilianza kupaa kwenye kura za maoni. Cameron alikinyooshea kidole chama cha Leba kwa kutodhibiti fumo wa marupurupu kwa wabunge hali iliyowafanya wengi kuyatumia kiholela. Huku Uingereza ikiwa bado inajikokota kutoka kwa wingu la mdororo wa kiuchumi, Cameron anaahidi kwamba ana uwezo na maarifa ya kuunyanyua uchumi na kubuni ufanisi. Kuongezeka kwa umaarufu wa Cameron kumewasisimua wafuasi wa Conservative na kuwapa matumaini kwamba huenda huu ni mwaka wao kurejea madarakani.