Wasifu wa Gordon Brown

Gordon Brown, kiongozi wa chama cha Labour.
Image caption Gordon Brown, kiongozi wa chama cha Labour ambaye anatumai wananchi watathamini sera za chama chake, ingawa kura za maoni zinaonyesha yuko nyuma ya wapinzani wake.

Gordon Brown katika mahojiano ya hivi karibuni amekuwa akijitahidi kuimarisha taswira yake kwa jamii. Anajitambulisha kama kitabu ‘kilicho wazi’ (open book).

Hayo ni maneno kutoka kwa mtu ambaye katika kipindi cha miaka kumi ya utumishi wake kama Waziri wa fedha ameelezewa kama mtu msiri, akijitokeza mara mbili kwa mwaka kutoa taarifa za kifedha kwa bunge (House of Commons).

Pia maisha yake binafsi yamekuwa ya siri akiepuka kuanikwa hadharani na vyombo vya habari.

Kimsingi, Bw Brown, anaonekana kutofurahia mahitaji ya kisasa ya vyombo vya habari na kuonekana kukosa uchangamfu kama aliokuwa nao Tony Blair.

Jitihada za kuibadili hali hiyo iwe faida kisiasa zimekuwa zikilenga kumwonesha kama mtu makini katika nyakati za misukosuko ya kiuchumi.

Lakini wakati uchaguzi mkuu ukiwa unakaribia, amekuwa akishauriwa kuweka ladha katika mwonekano wake mbele ya vyombo vya habari. Katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni, Bw Brown alitoa machozi pale alipoongelea juu ya kifo cha mtoto wake wa kwanza, Jennifer Jane.

Bw Brown alizaliwa na kukua Kirkcaldy, mji mdogo wa pwani kaskazini ya Edinburgh huko Scoland.

Kutambulika

Akiwa mtoto wa pili wa kiume wa mchungaji Dr. Ebenezer Brown, katika kanisa la Scotland, James Gordon Brown, alikuwa kijana mwenye aibu, mwenye kupenda kusoma na michezo.

Akiwa shuleni alijikuta akiathiriwa na mpango wa kutambua wanafunzi wenye uwezo mkubwa ambapo katika umri wa miaka 16 tu alikuwa sambamba na kaka yake wakiwa wote wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Edinburgh. Huku akichukua masomo ya historia, Brown alikuwa ni mwanafunzi mdogo kabisa wa shahada ya kwanza toka baada ya vita ya pili ya dunia.

Baada ya muda mfupi chuoni akawa maarufu na kuwa mwiba mkali kwa utawala wa chuo hicho kikuu. Akaendelea kujitengenezea jina ndani ya Scotland pale alipochaguliwa kuwa mkuu wa bodi ya utawala ya Chuo Kikuu cha Edinburgh. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mwanafunzi kukamata nafasi hiyo.

Lakini ajali aliyopata katika mchezo wa rugby na kupoteza nguvu ya kuona katika jicho moja, ilileta mtazamo mpya katika maisha yake.

Mwaka 1983 akawa mbunge katika jaribio la pili kupitia chama cha Labour. Hiyo ilikuwa baada ya kwanza kufanya kazi kama mhadhiri na ripota wa runinga. Akiwa mbunge akajenga ushirikiano na mbunge mwenzake Tony Blair na Peter Mandelson. Mtazamo wake ukawa kwamba chama kifanye mabadiliko ya kisasa na kuongeza mvuto wake kwa wapiga kura.

Mwaka 1984, wakati kiongozi wa chama cha Labour, Bw John Smith alipofariki ghafla, watu wengi walifikiri Bw Brown, wakati huo akiwa Waziri kivuli wa fedha, angerithi kiti cha uongozi wa chama.

Kipindi muhimu

Lakini ni Tony Blair aliyepewa nafasi kubwa ya kukipeleka tena chama katika utawala. Bw Brown akakubali kumuunga mkono Blair kwa makubaliano kuwa wakati fulani katika siku za usoni Blair angemwachia madaraka Brown.

Baada ya ushindi mkubwa wa chama cha Labour mwaka 1997, bwana Brown akatokea kuwa waziri wa fedha mwenye nguvu kubwa katika miaka ya karibuni.

Lakini Bw Brown hakupoteza shauku yake juu kiti cha uwaziri mkuu na ilionekana kama vile katika kipindi cha miaka kumi alikuwa akimkumbushia Bw Blair juu ya mpango wao. Baada ya Bw Blair kung’atuka mwaka 2007 akiwa na rekodi ya kushinda uchaguzi mara tatu, Brown akakamata nafasi ya uongozi wa chama na uwaziri mkuu bila ushindani.

Bw Brown bada ya kukamata nafasi ya uwaziri mkuu akaweka msisitizo juu ya kufuata siasa zenye kanuni na maadili. Mkakati huu ukaonekana kufanya kazi vyema kwani miezi michache ya mwanzo maoni yalionesha chama cha Labour kikizidi kufanya vyema.

Bw Brown akaingiwa na mawazo ya kuitisha uchaguzi mkuu mwaka 2007 ili kuimarisha uongozi wake, lakini akabadili mawazo yake dakika za mwisho baada ya kura za maoni kuonesha chama cha Tory kufanya vyema. Bw Brown akadai anahitaji muda ili kuweka sawa mtizamo. Lakini wapinzani wake wakadai hizo zilikuwa ni mbinu tu za kisiasa.

Kipindi kilichofuata kilikuwa kigumu hasa uchumi ambao ulikabiliwa na hali ngumu zaidi. Kura za maoni zikaonesha kuporomoka kwa chama cha Labour na ndani ya miaka miwili toka 2007 mawaziri kadhaa walijiuzulu na jitihada za kumwondoa Brown zikawa zikifanyika.

Ili kuweza kukabiliana na misukosuko Bw Brown ikambidi kutegemea mbinu za kisiasa toka kwa Lord Mandelson ambaye alisamehewa usaliti wake wa hapo awali na kushawishiwa kurudi Uingereza kutoka Brussels makao makuu ya Umoja wa Ulaya.

Bw Brown, ambaye chama chake kimeweza kupunguza uongozi wa chama cha Conservative katika kura za maoni kuelekea uchaguzi mkuu, atakuwa akijipa matumaini kuwa wapiga kura watazingatia uzoefu wake katika kukabiliana na msukosuko wa kiuchumi na kumchagua kuwa kiongozi wao.