Maswali na majibu: Bunge ni nini?

Kura za maoni za hivi karibuni zinaonesha uwezekano mkubwa wa kuwepo na bunge mning’inio bada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Njia ya kuepuka hali hii ni kwa chama cha Labour kuhakikisha kinaimarisha hali yake ipasavyo katika uchunguzi wa maoni ya watu (polls), au chama cha Conservatives itabidi kifanikiwe kuvuta kura nyingi toka kwa watu wasiojifungamanisha na chama chochote (swing votes).

Lakini tangu baada ya vita ya pili ya dunia, imetokea mara moja tu ambapo bunge mning’inio lilichaguliwa.

Lakini Bunge mning’inio ni nini hasa?

Bunge mning’inio ni pale ambapo hakuna chama kilichoweza kupata zaidi ya nusu ya wabunge wote katika Bunge la Wawakilishi (House of Commons).

Ina maana pia kuwa serikali bila ya kuungwa mkono na wabunge wa vyama vingine haitaweza kupata kura za kutosha kuiwezesha kupitisha sheria mbalimbali.

Katika uchaguzi wa mwaka huu idadi ya viti vya ubunge itaongezeka kutoka 646 hadi 650 baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya mipaka ya majimbo ya uchaguzi.

Hiyo inamaanisha kuwa chama chenye uwingi wa wabunge itabidi kiwe na viti 326. Bila ya kuwepo na chama kitakachokuwa na uwingi wa viti, bunge mning’inio litakuwa limechukua nafasi yake.

Vile vile ijulikane kuwa Spika wa bunge na manaibu wake, japo ni wabunge, kwa kawaida huwa hawapigi kura.

Pia katika bunge la sasa, kuna wabunge watano toka Sinn Fein ambao hawali kiapo cha utii kwa Malkia na hivyo kutokuwa na haki ya kupiga kura.

Chama cha Labour kitapoteza uwingi wake bungeni endapo kitapoteza viti 24 na chama cha Conservative kinaweza kupata uwingi wa viti bungeni endapo kinaweza kunyakua viti 116.Matokeo yoyote hapo kati yatasababisha kuwepo na bunge mning’inio.

Nini kinatokea endapo kuna bunge mning’inio?

Waziri Mkuu wa sasa atabaki madarakani hadi hapo atakapojiuzulu. Anaweza pia kujaribu kuendelea kuwemo ndani ya serikali hata kama chama chake hakikupata idadi kubwa zaidi ya viti.

Mwaka 1974, Edward Heath alikaa madarakani kwa siku nne baada ya uchaguzi akijaribu kuunda serikali ya mseto, ingawa chama cha Labour kilikuwa na idadi kubwa ya viti.

Chama kinaweza kukaa madarakani bila ya kuwa na uwingi wa viti bungeni (absolute majority) kwa kujaribu kuunda serikali ya mseto kwa kushirikiana na chama kidogo. Hii huhusisha maridhiano mbalimbali ya sera na kuruhusu wabunge toka chama kidogo kuingia katika baraza la mawaziri

Katika baadhi ya nchi, badala ya kuunda serikali za mseto, kumetokea makubaliano ambapo vyama vidogo huridhia kuunga mkono serikali pale inapotokea kuna kura zinazolenga kuiangusha serikali na kulazimisha uchaguzi.

Uwezekano mwingine ni kwa chama kikubwa zaidi kuunda serikali (minority government) bila makubaliano na vyama vingine na kujaribu kutafuta uungwaji mkono na wabunge wengi katika miswada mbalimbali kadiri inavyojitokeza.

Ikiwa hakuna chama kilicho tayari kufuata njia hizi bunge huvunjwa na uchaguzi mpya kuitishwa; ingawa hali hii haitarajiwi kutokea kwa sababu chaguzi mbili zilizokaribiana sana hazitakuwa na mvuto kwa watu na huenda matokeo yakawa vile vile.

Je hali hii imewahi kutokea Uingereza hapo kabla?

Katika uchaguzi wa kwanza kati ya mbili mwaka 1974 hakuna chama kulichopata uwingi wa viti.

Labour kilipata viti 301 ukilinganisha na Conservative kilichopata viti 297.

Harold Wilson akaunda serikali, lakini haikudumu muda mrefu.Uchaguzi mwingine mwaka huo mwezi wa kumi ukamwezesha Harold Wilson kupata uwingi wa viti kwa idadi ndogo ya kura tatu tu.

Bunge mning’inio jingine lilikuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1929. Ramsey MacDonald wa chama cha Labour alipata viti 287, Stanley Baldwin wa Conservative viti 260 na David Lloyd George viti 59.

Imewahi kutokea pia bunge likawa la mning’inio katikati ya safari kutokana na matokeo ya chaguzi ndogo ndogo, kama ilivyotokea kwa serikali ya bwana John Major mwaka 1996.

Mpaka hapo tunaona kuwa kumekuwepo kwa uchache sana mabunge mning’inio ndani ya Uingereza.

Nchi nyingine zinaonekana kuwa na mabunge mning’inio mengi. Kwanini si Uingereza?

Kwa jadi siasa za Uingereza zimekuwa zikitawaliwa na vyama viwili, ingawa inaonekana hali kuanza kubadilika.

Mfumo wa uchaguzi unatajwa kuwa sababu ya kuwepo kwa nguvu kubwa ya vyama viwili.

Israel ina mfumo mzuri sana wa uwakilishi bungeni.Wapiga kura huchagua kutoka katika orodha ya vyama. Vyama hivyo hupata viti katika bunge kutegemea na idadi ya kura walizopata katika nchi nzima.

Hali hiyo huhamasisha vyama vinavyojulikana kupigania maslahi ya mambo fulani, mf.mazingira, na vyama vyenye mvuto kwa sehemu fulani ya jamii na kuweka mazingora magumu kwa chama kimoja kushinda idadi kubwa ya viti bungeni.

Baada ya uchaguzi, chama kikubwa zaidi hujaribu kuunda serikali ya mseto kwa kushirikiana na vyama vidogo ili kuvuta uungwaji mkono bungeni.

Hali Uingereza ni tofauti. Chama kitapata kiti bungeni ikiwa tu kitaweza kushinda kura nyingi katika jimbo la uchaguzi.

Hiyo humaanisha kuwa vyama lazima vijaribu sana kuwavuta wapiga kura wengi katika majimbo ya uchaguzi kadiri iwekanavyo.

Vyama vidogo vinaweza kupata maelfu ya kura nchini kote lakini vikashindwa kupata viti vya ubunge.

Mfumo huu unaweka mazingira ya chama kimoja kuwa na uwekano wa kushinda kura nyingi zaidi.