Polisi yakamata wauza watoto Nigeria

Polisi wa Nigeria wamevamia zahanati moja iliyoko katika mji wa Aba kusini mashariki mwa nchi hiyo ambako wameokoa wasichana 32 wanaodaiwa kuwa walikuwa wakishikiliwa na genge la wauza binadamu.

Image caption Watoto wao hufanywa kafara

Wasichana hao walio kati ya umri wa miaka 15 na 17, walizuiliwa ndani ya vyumba na kutumiwa kwa ajili ya kupata watoto, amesema mkuu wa polisi wa jimbo la Abia.

Madhumuni ya watoto wanaozalishwa ni kuuzwa kwa waganga wanaowahitaji kwa shughuli za ushirikina na wengine labda kuwapatia watu wanaohitaji kizazi.

Lakini mwenye hospitali hio amekanusha madai kwamba anaendesha biashara ya kuzalisha watoto wa kuuzwa, na kuongezea kusema kuwa ni hospitali ya kuwasaidia wasichana wanaoshika mimba kabla ya wakati wao.

Shirika linaloshughulikia maslahi ya watoto,Unicef linakadiria kuwa hadi watoto 10 huuzwa kila siku kote nchini Nigeria ambako biashara ya binadamu inashika nafasi ya tatu katika visa vya uhalifu baada ya rushwa katika uchumi wa nchi na biashara ya mihadarati.

Hata hivyo, mwandishi wa BBC Fidelis Mbah mwenye makao yake katika mji wa pwani kusini mwa Nigeria wa Port Harcourt anasema kuwa wahalifu wanapokamatwa si kawaida kuchukuliwa hatua au kukabili sheria.

Watoto wa kiume wanapendwa zaidi. Kamishna wa Polisi wa Jimbo la Abia Bala Hassan amesema kuwa watoto wanne, ambao tayari walikuwa wameisha uzwa wakisubiri walionunua kuwachukuwa nao walinusuriwa katika operesheni hiyo.

Upelelezi wa shirika la kujitolea kupambana na biashara haramu ya binadamu nchini Nigeria linasema kuwa upelelezi wake umezua kua watoto wachanga wanafikia kiwango cha hadi dola za Marekani $6,400 kila mmoja ikitegemea pia jinsia ya mtoto.

Mtoto wa kiume ana bei kubwa zaidi, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC.

Katika sehemu za nchi ambako watoto hufanywa kafara inaaminika mwili wa mtoto mchanga hufanya mazingaombwe kuwa makali sana.

Wengine huuzwa kwa watu wanaohitaji watoto.

Wanawake ambao hawajaolewa nchini Nigeria, wenye uwezo mdogo wanakabiliwa na matatizo wanaposhika mimba. Mara nyingi hutengwa na jamii zao.

Mwandishi wetu anasema kuwa wasichana ambao hujikuta katika hali ya uja uzito mara nyingi hulazimika kwenda katika hospitali ambazo zitaficha siri yao na matokeo yake ni kuwaacha watoto kwa wafanya biashara.

Baadhi ya wasichana walionusurika huko Abia waliambia polisi kuwa baada ya watoto wao kuuzwa walipewa $170 na mwenye hospitali.

Polisi imesema kuwa mmiliki wa hospitali hiyo The Cross Foundation, Dkt Hyacinth Orikara huenda akafunguliwa mashtaka ya kuwanajisi watoto pamoja na biashara haramu ya binadamu.

Mwandishiw etu huko anasema kuwa biashara ya kununua na kuuza watoto wachanga ni haramu nchini Nigeria na hukumu yake ni hadi miaka 14 jela.

Miaka minne iliyopita mwanamke mmoja kutoka Nigeria alikamatwa na mtoto nchini Uingereza akiona kuwa ndiyo njia rahisi ya kupatiwa nyumba ya manispaa.