Matibabu mapya ya saratani ya tezi kibofu

Haki miliki ya picha SPL
Image caption Seli za saratani ya tezi kibofu

Mbinu mpya ya kutibu dalili za mapema za saratani ya tezi kibofu huenda ikawa na athari ndogo kwa wagonjwa ikilinganishwa na matibabu ya sasa.

Hii ni kulingana na utafiti kwenye jarida la matibabu la Uingereza, The Lancet .

Kwa mujibu wa wataalamu wa matibabu ya saratani , utafitui uliofanyiwa wagonjwa 41, unaonyesha kuwa mbinu hiyo inayotumia miale ya Ultrasound kulenga tu sehemu iliyoathirika, inapunguza uwezekano wa mtu kuondolewa uwezo wa kuzalisha, ambayo ni mojwapo ya athari ya matibabu ya saratani hiyo.

Watafiti wanasema kuwa utafiti huu huenda ukabadili matibabu ya saratani ya tezi kibofu katika siku za usoni ikiwa utaradiwa na kufanywa kwa ukubwa zaidi.

Baraza la utafiti wa matibabu ambalo lilifadhili utafiti huo, limepongeza matokeo yake ambayo lilisema ni dalili ya mustakabali mzuri wa matibabu ya saratani.

Kila mwaka wanaume 37,000 nchini Uingereza, hupatikana na saratani ya tezi kibofu.

Wengi hukabiliwa na wakati mgumu wanapoathirika: ugonjwa huo huua takriban watu 10,000 kila mwaka, lakini kwa baadhi ya wanaume ugonjwa huo huenda usiwe tisho kubwa ikiwa hautatibiwa.

Matibabu ya saratani hiyo kwa njia ya upasuaji au kwa kutumia miale ya eksirei, hujumuisha kutibiwa kwa sehemu yote ya tezi kibofu. Matibabu hayo yanaweza kuathiri seli zilizoko kwenye sehemu hiyo ya mwili, na kusababisha athari kubwa kwa mpira wa mkojo ambapo mtu anakosa uwezo wa kubana mkojo pamoja na kumkosesha uwezo wa kuzalisha.

Matibabu maalum

Madaktari katika chuo kikuu cha College Hospital mjini London, wamefanya utafiti wa kwanza, kwa kutumia miale mikali ya ultrasound ikilenga tu seli za saratani katika tezi kibofu.

Haki miliki ya picha
Image caption Seli za saratani ya tezi kibofu

Daktari wa upasuaji, Hashim Ahmed, alielezea ambavyo matibabu hayo yanafanya kazi.

Madaktari walitumia mbinu hiyo kwa kuweka miale kwenye tezi kibofu huku miale hiyo ikilenga tu seli zenye saratani na hivyo kusababisha athari ndogo mno kwenye misuli na seli ya za neva zinazozunguka sehemu hiyo.

Kulingana na Hashim Ahmed, daktari wa upasuaji aliyeongoza utafiti huo miezi 12 baada ya matibabu hayo kujaribiwa , matokeo yake ni ya kuridhisha.

Bwana Ahmed, amesema kuwa ushahidi unaonyesha mbinu hiyo ya kutibu na kuzuia kusambaa kwa saratani ni nzuri. Robert Page mwenye umri wa miaka 72, aliyetibiwa kwa njia hiyo miaka miwili iliyopita amesema kuwa matibabu hayo yalimsaidia sana.

Bwana Page alisema, " Matokeo yalikuwa mazuri sana. Nilifurahia sana baada ya kupokea matibabu hayo hasa kwa sababu sikupata athari zozote, ikilinganishwa na matibabu mengine."

Hata hivyo wataalamu wamependekeza kufanyika utafiti zaidi kwa kuwa ulifanyiwa tu wanaume chini ya 50.