Je ni nani huyu rais mpya wa Somalia?

Imebadilishwa: 11 Septemba, 2012 - Saa 09:59 GMT

Rais mpya wa Somalia

Hassan Sheikh Mohamud, mwenye umri wa miaka 58, ni msomi sawa na kuwa mwanaharakati. Alifanya kazi na mashirika mbali mbali ya amani na maendeleo ndani na nje ya Somalia.

Alifuzu digree yake katika chuo kikuu cha taifa nchini Somalia mwaka 1981 na kuelekea kwa masomo ya ziada nchini India ambako alipata digree ya Uzamili (Masters) katika chuo kikuu cha Bhopal.

Kwa miaka miwili, rais Sheikh Mohamud alifanya kazi na shirika la kuwahudumia watoto la UNICEF kama afisaa wa elimu Kusini mwa Somalia hadi majeshi ya amani ya UN yalipoondoka Somalia mnamo mwaka 1995.

Miaka minne baadaye, alianzisha taasisi ya mambo ya usimamizi na utawala bora mjini Mogadishu, ambayo baadaye ilifanywa kuwa chuo kikuu cha Simad.

Mnamo kwaka 2011, aliunda chama cha kisiasa cha amani na maendeleo au PDP. Kwa sasa yeye ndiye mwenyekiti wa chama hicho,

Anaongea kisomali na kiingereza na anatoka katika mojawapo ya koo kubwa sana nchini Somalia, Hawiye.

Ulinzi mkali wakati wa uchaguzi

Mchakato wa uchaguzi ulichelewa kwa saa tano, kwa sababu ya ukaguzi mkali wa usalama uliokuwa unafanywa.

Uchaguzi huo pia ulichelewa kwa sababu ya shughuli ya kuwaapisha wabunge waliosalia na kisha kupiga kura kuhusu ikiwa wabunge waliozua utata wakiwemo wababe wa zamani wa kivita wangeweza kuhusika na uchaguzi huo. Wabunge wote waliunga mkono hilo.

Spika mya wa bunge Mohamed Osman Jawari, aliwasihi wabunge watafakari sana wakati wakipiga kura.

"tunamuomba Mungu atusaidie kumchagua kiongozi katika mazingira tulivu. Lazima tuwape vijana wa Somalia mustakabali mzuri wa nchi yao. '' alisema rais huyo.

Shughuli ukabidhi wa mamlaka inaonekana kusimamiwa pakubwa na wahusika wa nje ambao wamekuwa kwa miaka mingi wakijihusisha kijeshi na kisiasa nchini Somalia. Kwa mujibu wa mchambuzi wa mambo ya Somalia Mary Harper.

Lakini rais Hassan Sheikh Mohamud huenda akawakilisha mustakabali tofauti wa somalia kwa sababu hahusiki kivyovyote na mapigano au ufisadi chini Somalia.

Hata hivyo, anakabiliwa na changamoto nyingi, kutoka pembe zote. Atahitaji kukabiliana na wanasiasa mashuhuri walioshindwa kwenye uchaguzi, kisha atatarajiwa kuleta uwiano katika nchi hiyo baada ya miongo miwili ya vita, ambavyo hata leo vinahusisha kundi la al-Shabab.

Tangu kung'olewa kwa rais Siad Barre mwaka 1991, Somalia imeshuhudia wababe wa kivita kutoka koo mbali mbali, wanamgambo wa kiisilamu na nchi jirani zikipigania udhidibiti wa nchi.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.