Msamiati sio Mawasiliano

Imebadilishwa: 3 Oktoba, 2012 - Saa 10:17 GMT

Maisha bila mawasiliano si maisha. Lakini Je haya mawasiliano yana umuhimu wowote katika jamii ikiwa wanaowasiliana hawaelewani? Bila shaka jawabu ni la. Tatizo hili lipo katika lugha ya Kiswahili na limesambaa kama moto katika kichaka kikavu. Je wahusika ni kina nani? Watangazaji wana nafasi kubwa mno. Walimu na wahadhiri wa Kiswahili ni wachangizi wakuu jinsi walivyo wahubiri na mashekhe.

Katika sehemu nyingi duniani wanahabari wanaaminika kwa yale wanayosema hewani ama katika nakala wanazoandika. Wananchi pia huamini kuwa maneno wanayotumia wanahabari ni sanifu. Lakini je matumizi ya msamiati wasiofahamu watu wengi yana manufaa gani katika jamii?

Tuongee kiswahili

Jambo lisilopingika ni kuwa ni bora wanahabari katika idhaa mbalimbali za Kiswahili kote ulimwenguni kutumia maneno yaliyozoeleka ili wasiwataabishe wasikilizaji wao. Ni dhahiri kuwa mojawapo ya sifa kuu ya lugha ni kuwa lugha hukua na vile vile hubadilika. Hata hivyo makuzi na mabadiliko ya lugha hayatakiwi kutatiza mawasiliano baina ya wahusika.

Kutokana na msimamo huo ni vyema watangazaji wazingatie hadhira. Kwa mfano lugha unayotumia kumhoji Profesa wa Kiswahili si sawa na ile unayotumia kumhoji mtu wa elimu ya shule ya msingi. Hata hivyo kuna kiwango cha wastani cha lugha ambacho mwanahabari wa Kiswahili anaweza kujiweka ili kuwafikia na kuwaelewesha wasikilizaji au wasomaji wake anacholenga.

Sisemi watu wasijue visawe vya maneno mengine ya Kiswahili namaanisha ni vizuri kuvijua visawe hivyo ila tujue pa kuvitumia. Kwa mfano nikisema 'Shangazi' nitaeleweka kuliko nikisema 'mbiomba.

Vivyo hivyo nikisema 'heshima' wengi watanielewa lakini ninapotumia jina 'mbeko' wengi watakimbilia kamusi kwa ushauri. Kadhalika ninaposema 'shaibu' watu wataniuliza mbona nisiseme tu mzee? Aidha nchini Kenya watangazaji wengi wamekuwa wakitumia neno 'ghushi' wala hawako radhi kutumia 'bandia'. Ni dhana zinazokaribiana ila kwa maoni yangu unapotumia bandia utaeleweka kwa urahisi.

Kwa hivyo haya mabomu ya msamiati wanayotumia baadhi ya watangazaji wa lugha ya Kiswahili ni hatari kwa usalama wa lugha yenyewe. Aidha vituo mbalimbali vya matangazo vinatakiwa kutumia majina yanayoeleweka katika makala na vipindi vyake. Kwa mfano jina la taarifa za habari linatakiwa kueleweka kwa urahisi.

Idhaa ya Kiswahili ya BBC ni moja ya Idhaa ambazo zimezingatia kwa dhati umuhimu wa kuwasiliana na hadhira yake kwa njia kunjufu zaidi. Mathalani unapotazama majina ya vipindi vyake unajua moja kwa moja yaliyomo katika makala hayo. Kwa mfano vipindi kama vile Ulimwengu wa Soka, Michezo na wachezaji, Amka na BBC, Leo Afrika, Nipe kitabu, makala ya Kiswahili na kadhalika. Majina hayo yanaeleweka kimuktadha. Ni maoni yangu tu. Nini maoni yako?

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.