Kibarua cha Nkosazana Dlamini Zuma

Imebadilishwa: 18 Oktoba, 2012 - Saa 07:23 GMT

Noel Mwakugu, mwandishi wa BBC wa maswala ya Umoja wa Afrika

Umoja wa Afrika unafungua ukurasa mpya leo, siku ambayo mwanamke wa kwanza anaapishwa rasmi kama mwenyekiti wa tume ya umoja huo.

Aliyekuwa waziri wa masuala ya ndani nchini Afrika Kusini Dr Dlamini Zuma, anaanza kuhudumu kama mwenyekiti baada ya kushinda uchaguzi ulioshuhudia mvutano mkali kati yake na mwenyekiti anayeondoka Jean Ping kutoka Gabon.

Lakini je ni kibarua kipi kinachomkabili kiongozi huyu mpya ?

Ushindi wa Dr Dlamini Zuma katika kinyang'anyiro cha kuongoza tume ya umoja wa afrika, ilikuwa ishara tosha kuwa, umoja huo unahitaji mageuzi.

Ingawa wengi wanatarajia umoja huo uwe ndio chachu ya mabadiliko Barani Afrika sawa na jinsi ule wa ulaya unavyotenda kazi zake, umedumaa na wengi wanautizama kama baraza la viongozi wazee la kupiga soga tuu kila mwaka.

Kwa mtazamo huu, kazi ya Bi Zuma ipo wazi. Uchaguzi wake ulikuwa tofauti na desturi iliyokuwepo ambapo ni wagombea wa nchi ndogo, yaani zenye uchumi mdogo ambao wanachaguliwa kwa nafasi hiyo, lakini yeye anawakilisha taifa lenye uchumi mkubwa na huenda ushawishi huu utamwezesha kufanya mageuzi makubwa kwenye tume hiyo labda kuufufua umoja huo wakati wa kusherekea miaka 50 tangu kuasisiwa.

Lakini ili kufanya mabadiliko haya, lazima ajenge uhusiano mpya kwenye bara hili, ambalo liligawanyika kwa pande mbili wakati wa uchaguzi wake.

Mwanyekiti mpya wa AU

Kwa ujumla nchi zinazozungumza kiingereza zilimuunga mkono, huku mataifa yanayotumia lugha ya kifaransa yakimpigia kura mpinazani wake Jean Ping kutoka Gabon. Punde tu alipochaguliwa alisema ushindi wake ni wa Afrika na sio nchi yake au ukanda wa Afrika kusini, kauli ambayo lazima adhihirishe kwa vitendo katika siku zake 100 za kwanza ofisini.

Mashirika ya kijamii na hata wafanyikazi katika umoja huo wanasubiri kwa hamu sana kuona jopo washauri na wandani wake watatokea wapi.

Kawaida kila aliyekuwa kwenye wadhifa huo amezungukwa na washauri kutoka nchi au eneo lake, ikiwa basi atabadilisha taswira hii itakuwa hatua nzuri.

Bila shaka baada ya kuwepo kwa nusu karne, mhula wake wa miaka minne utaangaziwa sana. Je Bi Zuma atachukua fursa hii kuwahusisha zaidi raia wa Afrika katika mikakati ya umoja huo? Hali ilivyo sasa ni wataalamu tuu wanaoelewa utenda kazi wa umoja huo.

Alimenyana na aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo Jean Ping

Wadadisi wanasema huenda ndio maana viongozi hawawajibishwi kila wanapopitisha maazimio yao. Matokeo, ni machache yanayotekelezwa au yanapewa kisogo.

Na ili kuleta mageuzi, Bi Zuma anahitaji ngao kuendesha ajenda yake. Ngao hiyo kulingana na wanaofuatia masuala ya Umoja wa Afrika ni wafanyikazi bora.

Ngazi za tume hiyo zinahitaji ari mpya ya utendakazi, wanaomfahamu Bi Zuma wanasema ni kiongozi anayewajibika, sifa anayohitaji sana katika makao yake mapya mjini Addis Ababa ikiwa nia yake ni kubadili tume hiyo iende na mahitaji ya dunia ya sasa inayoegemea sana vitendo na sio gumzo tu.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.