Watu wa Nakuru wataka maridhiano

Imebadilishwa: 18 Oktoba, 2012 - Saa 08:25 GMT

Mwanasiasa Koigi wa Wamwere ashauriana na mshiriki wa kipindi cha Sema Kenya.

Je! kaunti ya Nakuru iko tayari kwa uchaguzi wa amani Machi mwaka ujao? Hili ndilo swali SemaKenya, mjadala mpya wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ilinuia kupata jawabu wakati ilipozuru kaunti ya Nakuru hivi karibuni.

Kufuatia maswali yaliyo ulizwa na baadhi ya wakaazi, ilikuwa wazi kuwa kuna hatari ya vurugu kutokea tena iwapo serikali haitahakikisha kuna maridhiano ya kweli. Kaunti ya Nakuru ilikuwa kitovu cha machafuko yaliyoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007.

Mwanasiasa mashuhuri katika kaunti ya Nakuru, Koigi wa Wamwere, alisema kuwa kutokana na hali ilivyo kwa sasa, huenda kukawa na machafuko. Alidai serikali haijajitokeza kuhakikisha kuwa kuna uwiano baina ya makabila mbalimbali.

“Kamahatutaangalia vizuri, kutatokea machafuko. Kwa maoni yangu hatukupata funzo kutokana na machafuko tuliyoshuhudia,” alionya bwana Koigi.

Hata hivyo, waziri msaidizi wa barabara ambaye pia ni mbunge wa eneo la Nakuru mjini, Lee Kinyanjui, alitofautiana na bwana Koigi. Bwana Kinyanjui aliwahakikishia wakaazi wa Nakuru kwamba serikali itajitahidi kuhakikisha uchaguzi wa mwakani utakuwa wa amani.

Alisema kuwakamamwakilishi wa eneo bunge la Nakuru mjini, hajaona dalili yoyote kwamba huenda kukatokea machafuko. “Hakuna mafikira mabaya. Wakaazi wanataka mwanzo mpya na uchaguzi ujao ndio utakuwa huo mwanzo mpya,” alisema bwana Kinyanjui.

Naye mwenyekiti wa tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), Mzalendo Kibunjia, aliwaelezea wakaazi wa Nakuru kwamba tume yake haitaruhusu uchochezi wa aina yoyote, ambao matokeo yake yatakuwa ni vurugu wakati wa uchaguzi.

“Wakati tutakapopiga kura hakutakuwa na vurugu nchiniKenyakwa sababu tume haitaruhusu kiongozi yeyote kuchochea Wakenya wapigane” Kibunjia aliahidi.

Aliwahimiza wakaazi wa Nakuru kutoa ripoti kwa tume hiyo iwapo watasikia mtu yeyote akitoa matamshi ya uchochezi huku akiahidi kuwachukulia hatua watu wanaodaiwa kuchochea wengine.

Lakini, Obama Stephen, mkaazi mwingine wa Nakuru, alitoa mfano wa matamshi ya uchochezi yanayotolewa. Alisema kuwa, “Saa hivi tunapozungumza kuna kabila fulani hapa Nakuru ambalo limeambiwa tafuteni nyumba kwingine nakamasi hivyo, vile kulivyotokea mwaka wa 2007 kutatokea tena”.

Ukabila na ugavi wa viti vya kisiasa

Mshiriki wa kipindi cha Nakuru auliza swali.

Ikiwa ni eneo lenye jamii kutoka sehemu mbali mbali za nchi, swala la ugavi madaraka kuambatana na muundo mpya wa serikali ya ugatuzi pia liliibuka.

Wakaazi wa Nakuru wanahofia kwamba huenda kabila kubwa likachukua viti vingi vya uongozi kuanzia gavana, seneta, mbunge na viti vya uwakilishi bungeni.

Viongozi kwenye jopo la Kipindi cha SemaKenyawaliwashauri wenyeji wa Nakuru kuwachagua viongozi ambao watashughulikia maslahiyaobila kujali wametoka kabila gani.

Lakini ilikuwa wazi kuwa iwapo kutatokea kwamba kabila moja litanyakua viti vyote, basi hili huenda likachochea uhasama wa kikabila na pengine vurugu.

Wakaazi walipendekeza kufanyike mazungumzo baina ya viongozi ili kutafuta njia ya kuhakikisha kila kabila limewakilishwa katika uongozi.

Mwenyekiti wa NCIC, Mzalendo Kibunjia, aliwafahamisha kwamba mazungumzo kuhusu swala hili yanaendelea na kwamba viongozi tayari wameafikiana kuhusu swalahiloambapo watahakikisha makabila madogo madogo yanawakilishwa.

Hata hivyo Isaack Kaacho hakubaliani na wazohilo. “Nafikiri bwana Kibunjia lile jambo analojaribu kufanya inaitwa ”negotiated democracy” na mara nyingi katika nchi kama yetu yaKenyaambapo makabila mengine ni makubwa huenda inaweza kukosa kufanya kazi,” Kaacho alisema.

Wakimbizi wa ndani kwa ndani

Miaka minne baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007, ambapo maelfu ya watu walitoroshwa makwao katika eneo hili, bado swala la wakimbizi wa ndani ni donda dungu.

Katika makala ya Sema Kenya Kaunti ya Nakuru, wakaazi walidai serikali imeshindwa kusuluhisha swalahilo.

Waziri wa barabara na mbunge wa eneo la Nakuru mjini, Lee Kinyanjui alijipata matatani alipojaribu kuelezea kuwa tatizohilolinashughulikiwa ipasavyo.

Kwa mujibu wa Bwana Kinyajui, ni asilimia tano pekee ya wakaazi ambao hawajapewa makazi mapya.

Ilikuwa wazi kuwa swala la wakimbizi wa ndani katika eneo la Nakuru ni nyetisanana iwapo serikali haitalitatua kwa haraka, basi huenda likasababisha matatizo katika uchaguzi mkuu ujao.

Usalama

Jopo la Sema Kenya Nakuru

Sababu kuu ya wakimbizi kushindwa kurudi makwao ni kutohakikishiwa usalama na serikali wanaporejea makwao.

Judy Wairimu ni mkimbizi wa ndani mjini Nakuru, alifurushwa kutoka eneo la Burnt Forest na anasema ameshindwa kurudi Nyumbani huko kwa sababu majirani wake wanadai huko si kwao sasa.

Nathan anayetoka eneo la Kuresoi alieleza maisha yake yalivyobadilika baada ya machafuko hayo ya baada ya uchaguzi. “Ndugu yangu aliuawa mwaka wa 2008 na ninajua waliomuua. Hata sikupata fursa ya kumzika kaka yangu. Kutoka wakati huo sijarudi nyumbani. Mara ya mwisho kuenda kwa kaburilakenilipelekwana askari sita wa polisi.”

Nathan anasema haonikamakumekuwa na maridhiano ya kweli kwa sababu alidai watu wanaotuhumiwa kumuua kaka yake bado hawajachukuliwa hatua za kisheria na ni watu wanaojulikana.

Jiunge nasi kwenya mitandao ya kijamii Facebook/BBCSemaKenya na pia kwa @BBCSemaKenya

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.