Mwaka mmoja baada ya kifo cha Gaddafi, familia yake iko wapi?

Imebadilishwa: 22 Oktoba, 2012 - Saa 08:57 GMT

Muamar Gaddafi

Mwaka mmoja baada ya kukamatwa na kuuwa kwa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi tarehe 20 mwezi Oktoba mwaka 2011, familia yake iko wapi?

Watoto watatu wa Gaddafi waliuawa wakati wa harakati za mapinduzi akiwamo aliyekuwa mshauri wake wa usalama wa kitaifa Mutassim Gaddafi, aliyefariki mikononi mwa waasi siku moja na babake.

Jamaa za Gaddafi wanaosalia wamekumbwa na hali tata tangu kifo cha Rais huyo mwezi Oktoba, huku mjane wake akitafuta hifadhi katika nchi jirani ya Algeria, mwanawe na aliyeonekana kama mrithi wa wake Saif al-Islam yuko gerezani nchini Libya akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake kuhusu uhalifu wa kivita.

Safiya Gaddafi (Mjane wa gaddafi)

Safiya Farkash, mama wa watoto wanane wa Gaddafi amekuwa akiishi nchini Ageria alikopewa hifadhi kwa sababu za kibinadamu.

Pamoja na wanawe Ayesha na mwanawe wa kambo kutoka kwa mke wa kwanza wa Gaddafi, waliingia nchini Algeria wakati waasi walipoudhibiti mji mkuu Tripoli.

Amepewa hifadhi nchini humo na kuwekewa vikwazo na serikali vya kutotoa matamshi yoyote ya kisiasa wala kuingilia mambo ya Libya

Muhammad Gaddafi (Mwanawe)

Ikiwa mambo yangekwenda vinginevyo Muhammad angehudhuria michezo ya Olimpiki 2012 kama mkuu wa kamati ya michezo hiyo nchini Libya.

Badala yake, Muhammad mwanawe wa kwanza Gaddafi, amekuwa nchini Algeria kwa mwaka mmoja sasa tangu kukimbilia huko wakati waasi walipovamia mji wa Tripoli.

Ni mtoto wa mke wa kwanza wa Gaddafi, Fathia, pia alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya taifa mawasliano ya simu za mkononi nchni Libya.

Hatakikani na mahakama ya ICC na hakuhusika pakubwa na kujaribu kuzima harakati za mapinduzi dhidi ya babake mwaka jana.

Saif al-Islam Gaddafi (Mwanawe Gaddafi)

Alionekana na wengi kama ,mrithi wa babake, alikamatwa mwezi mmoja baada ya kifo cha babake, na amekuwa akizuiliwa mjini Zintan tangu hapo.

Alihitimu kutoka chuo cha mafunzo ya uchumi mjini London, na amekuwa sababu ya mvutano kati ya mahakama ya kimataifa ya ICC ambako anakabiliwa na tuhumza za uhalifu wa kivita na maafisa wa sheria nchini Libya ambao wanasisitiza kuwa lazima kesi yake iendeshwe nchini humo.

Idara ya sheria nchini Libaya kwa sasa inaonekana kushinda katika mvutano huo, lakini hakuna tarehe rasmi ya kusikilizwa kwa kesi yake, inaarifiwa kuwa jela ya kifahari ikiwa na uwanja wa mpira wa vikapuni na mpishi wake binafsi vimeandaliwa kwa Saif mjini Tripoli

Saadi Gaddafi (Mwanawe Gaddafi)

Saadi Gaddafi, aliyekuwa mkuu wa shrikisho la soka nchini Libya pamoja na kuongoza vikosi maalum, amepewa hifadhi nchini Niger ambako anaishi katika makao makuu baada ya kutoroka kupitia jangwa la Sahara.

Saadi ana sifa tata ambapo alikuwa akicheza soka katika ligi ya Italia ingawa safari yake ilikatizwa baada ya kuhusishwa na madawa haramu pamoja na maisha yake ya anasa.

Niger imekataa ombi la Libya kumpeleka nchini humo huku waziri wa sheria akisema kuwa huenda akahukumiwa kunyongwa.

Mnamo mwezi Septemba, shirika la Polisi wa kimataifa Interpol lilitoa onyo ambalo litawaruhusu nchi wanachama kamkamata Saadi.

Mwezi Disemba mwaka jana polisi nchini Mexico walisema wana taarifa za kijasusi kuwa magenge ya wafanyabiashara haramu ambao wanajaribu kumhamisha Saadi nchini Mexico kwa kutumia stakabadhi bandia.

Hannibal Gaddafi (Mwanawe Gaddafi)

Hannibal ni mtoto wa tano wa Gaddafi na Safiya Farkash. Inaamini alikuwa kwenye msafara wa magari ya Gaddafi uliokuwa unaelekea nchini Algeria mwaka Jana .

Alikuwa anaongoza majeshi kulinda eneo la Gharyan, Kusini mwa Tripoli, kabla ya waasi kudhibiti Tripoli.

Alisifika kwa tabia zake za anasa na aliwahi kukamtwa akiwa amelewa wakati akiendesha gari aina ya Porsche mjini Paris.

Alizua mgogoro wa kidiplomasia na Uswizi baada ya kuwashambulia wafanyakazi wawili wa hoteli nchini humo na kusababisha babake kuwafunga jela wafanyakazi kutoka nchini humo, na hata kuiwekea nchi hiyo vikwazo.

Aisha Gaddafi (Mwanawe Gaddafi wa kike)

Mwanawe pekee wa kike alipewa hifadhi nchini Algeria pamoja na mamake na ndugu yake.

Siku tatu baada ya kuwasili Algeria, alijifungua mtoto msichana na kumuita Safiya, jina la mamake.

Licha ya kuwekewa ulinzi mkali na serikali ya Algeria, aliripotiwa hivi karibuni kuwataka watu nchini Libya kupindua serikali ya sasa. Kwa usaidizi wa wakili wake Muisraeli, aliitaaka mahakama ya ICC kuchunguza kifo cha babake

Aisha pia aliripotiwa kuunga mkono Algeria katika mechi moja kati yake na Libya akisema kuwa serikali mpya ya Libya haimwakilishi kivyovyote.

Hanaa Gaddafi (Mwanawe wa kuasiliwa)

Kanali Gaddafi alikuwa kwa muda mrefu akidai kuwa Hanaa aliuawa katika shambulizi la Marekani mwaka 1986 wakati akiwa na mwaka mmoja na nusu. Lakini tangu mapinduzi kufanyika, kumekuwa na taarifa kuwa Hanaa yuko hai ingawa hajulikani aliko.

Moussa Ibrahim (aliyekuwa msemaji wa Serikali)

Tarehe 20 mwezi Oktoba, mwaka mmoja baada ya kifo cha Gaddafi, taarifa kutoka kwa ofisi ya waziri mkuu zilisema kuwa Ibrahim alikamatwa na waasi mjini Tarhouna, maili arobaini kutoka mji mkuu.Maafisa wengine hata hivyo walishuku habari hizo.

Kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu kukamatwa kwake lakini baadaye ikasemekana kuwa uongo.

Alikuwa mwsemaji wa serikali na kujulikana na vyombo vya habari vya kimataifa, alionekana mwisho mjini Tripoli kabla ya waasi kuudhibiti mji huo.

Kila siku alitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwa imara na kwamba waasi hawatafanikiwa kuiangusha.Alitoka kabila moja na Gaddafi na alijigamba kuishi nchini Uingereza kwa miaka 15 kabla ya kurejea nyumbani.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.