Mwanamitindo Albino. Je inawezekana?

Imebadilishwa: 29 Oktoba, 2012 - Saa 08:40 GMT

Diandra Forrets akijiandaa kwa maonyesho ya mitindo nchini Afrika Kusini

Nyuma ya ukumbi, kelele zikiwa zimejaa katika tamasha la Wiki ya mitindo Afrika nchini Afrika Kusini, mwanamke mmoja amekaa kimya.

Wanamitindo wenzake pamoja na wabunifu wa mitindo kutoka kote barani Afrika wana kazi nyingi si haba. Kuna shughuli si haba kiasi cha mtu kusema kuwa kuna ushindani wa kelele.

Lakini licha ya kimya chake, Diandra Forrest mwanamitindo wa kulipwa raia wa Marekani, ndiye nyota ya chumba hiki.

“Ni muhimu kwangu kuwa hapa kwa sababu nataka kubadili ambavyo watu wanavyowatizama wasichana maalbino katika bara hili.” Alisema Diandra

Akiwa na ukosefu wa rangi katika ngozi yake au nywele zake, msichana huyo aliyekulia mjini New York, hususan katika mtaa wa Bronx ambao ni makao kwa wamarekani weusi, ni kawaida kwake kuwa na tabasamu.

Takriban mtu mmoja kwa kila watu 17,000 anazaliwa akiwa na hitifalu katika genetiki zake ambayo inaweza kumsababisha kuwa kipofu au kuwa na ulemavu wa ngozi.

Lakini anajua kuwa kuwepo kwake hapa katika maonyesho ya mitindo ya kiafrika, ina umuhimu mkubwa kuliko kuhoji dhana ya ''ni nini urembo?''

Katika baadhi ya nchi za afrika, hasa Afrika Mashariki, watu anbao ni Albino, wanaishi katika hofu ya kutekwa na kuchinjwa kwa sababu viungo vya miili yao vinaaminika kuwa na nguvu fulani.

"Ni muhimu kwangu sana kuwa hapa kwa sababu nataka kubadili dhana za watu kuhusu wasichana walio na ulemavu wa ngozi’’ aliambia BBC

"Nilidhani kuwa maisha yalikuwa magumu kwangu nilipokuwa mtoto, watoto wengine wakinikejeli saa zote. Kila nikienda nyumbani nilikuwa nalia’’ alisimulia Diandra.

'Apigwa na butwaa'

" Lakini hiyo sio hoja ikilinganishwa na kile ambacho watu kama mimi hupitia katika safu kama hii, hususan katika maeneo ya mashinani’’

Watengezaji wa mtindo, wa kimataifa wanawatumia maalbino sana siku hizi katika kuonyesha mitindo yao.

“Nilipogundua kuwa katika nchi kama Tanzania, maalbino kama mimi wanaishi na hofu ya kukatwa sehemu zao za mwili kwa sababu za kibiashara, nilipigwa na butwaa. Watu kama mimi wanaishi kwa hofu kila siku ya maisha yao. Inasikitisha sana.’’

Lakini inapokuja kwa mitindo ya kimataifa Bi Forrest anatoa mwelekeo.

Kama wengine, katika sanaa ya mitindo, msanii wa Afrika Kusini anayeishi uingereza, Jacob Kimmie alifurahi sana alipokutana na Bi forrest.

"Anaonekana tofauti sana na ana mvuto ambao sijawahi kuona kama mwanamitindo. Niliona kama lazima kuwa naye mwenye tamasha la leo.’’ Alisema Jacob.

Wakati huu katika safu za mitindo, kumtumia mwanamitindo Albino katika maonyesho yoyote , ni kitu kinachowika sana sasa. lakini natumai kuwa kutumia watu kama hawa kutaleta mabadiliko yatakayodumu’’

Refilwe Modiselle, mwanamitindo wa Afrika Kusini, na ambaye ni Albino aliyekulia mtaani Soweto,anakubaliana na kauli hii.

Kazi yake ya uwanamitindo ilianza tangu akiwa na umri wa miaka 13, na sasa yeye ndiye sura ya kampuni ya mitindo ya Legit na anasema kuwa wakati huo mtu yeyote aliyekuwa albino alibaguliwa sana.

"Nahisi kuwa kazi ambayo Diandra na mimi tunafanya ni kuleta mabadiliko ya kweli.’’ Anasema Modisile

Ushirikina

Lakini katika mkoa wa Kwazulu Natal, siku moja baada ya kuanza kwa tamasha hili, inaarifiwa mtoto mmoja mvulana hajulikani aliko mwaka mmoja baada ya kutekwa nyara.

Maalbino wamekuwa waathiriwa wa mauaji ya kishirikina

Familia yake inahofia kuwa huenda alitekwa kwa sababu za kishirikina

Na hivi karibuni, katika eneo la Meru, nchini Tanzania maiti ya mwanaume anayeonekana alikuwa na umri wa miaka 30, ilipatikana mwezi Juni ikiwa haina baadhi ya sehemu za mwili wake.

Sasa je sanaa ya mitindo inaweza kuleta mabadiliko?

Peter Ash, mwandishi wa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu masaibu ya maalbino, anasema inawezekana

“Kadri ujumbe kama huu unavyoendelea kutolewa kuhusu maalbino, ndivyo mambo yanakvokuwa sawa juu yao. Kwa hakika itasaidia” alisema Ash

"Tunavyoona ni kwamba dhulma dhidi ya albino ni kama zinakubalika katika jami kwa sababu wanaonekana kama sio watu kama wengine. Wanaonekana kama laana au wanawakilisha ushirikina’’ anasema Ash.

Kwa hivyo ni muhimu kwa jamii za kiafrika kuanza kuona watu kama hawa ambao wanaleta mabadiliko katika dhana kuhusu maalbino’’

“Mimi ni msichana mweusi mwenye ngozi ya mtu mweupe na hilo pekee linapaswa kuleta taswira ya binadamu na anachopaswa kuwakilisha

Katika ripoti ya umoja wa mataifa iliyofanywa na Ash,takriban watu 71 waliuawa nchini Tanzania kati ya mwaka 2006 na 2012, na wengine 31 wakanusurika mauaji.

Maalbino kumi na saba waliuawa nchini Burundi, saba nchini Kenya na wengine watatu nchini Swaziland.

Visa vya mauaji havikutokea sana nchini Afrika Kusini anasema Nomasonto Mazibuko kutoka kwa shirika linalotetea maslahi ya wenye ulemavu wa ngozi

Lakini anasema kuwa mabadiliko yanapaswa kuja kutoka ndani ya bara la Afrika.

“Swala nyeti hapa ni watu hawaoni maalbino kama binadamu. Ni juu yetu kuzungumzia swala hili na kuweza kuangamiza unyanyapaa.”

Anaongea kwa ukali “Hatuwezi kukimya wala hatuwezi kujificha. Na msichan yeyote ambaye ni albino na ambaye yuko katika jukwaa la kimataifa la mitindo au hata kwenye barabara akiwa anajivunia, ni kiungo kinachohijitajika kuweza kuwa moyo wasichana wengine’’

Bi Modiselle anatumai kuwa yeye atakuwa chachu ya mabadiliko

"mimi ni ishara ya umoja. Mini ni msichana mweusi mwenye ngozi nyeupe

" Ningependa kusifika tu kama mwanamitindo wala sio kwa sababu ya ulemavu wangu wa ngozi.’’ aliongeza Modisile

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.