BVR ni nini?

Imebadilishwa: 14 Novemba, 2012 - Saa 09:33 GMT

Washiriki wa kipindi cha Sema Kenya Kisumu.


Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Usajili wa wapiga kura utafanywa kwa njia ya elektroniki, Biometric Voter Registration (BVR).

BVR ni nini?

Biometric Voter Registration (BVR) ni njia ya kusajili wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya kompyuta kunasa data za maumbile ya mtu kwa vile jina, umri, jinsia, alama za vidole na uso. Teknolojia hii inatumika kuthibitisha uhalisi wa wapiga kura na kuhakikisha uwazi na usadiki zaidi wa uchaguzi.

Je, vipi vifaa muhimu vya BVR?

Vifaa vya BVR ni pamoja na:
a) Kompyuta ndogo ya mkononi
b) Skena ya kuchukua alama za vidole
c) Kamera
d) Programu ya usajili
e) Hifadhi ya umeme
f) Pazia la nyuma la kuchukulia picha

Nini inaifanya BVR bora zaidi katika kuunda sajili ya kuaminika?

Habari za kibinafsi zinazonaswa na BVR ni za kipekee kwa kila mtu na haziwezi kutumiwa na mwingine. Hii inasaidia kuunda sajili ya kuaminika. BVR inahitaji kila mpiga kura kufika mwenyewe katika kituo cha kura ili kuhakikisha ni wapiga kura tu hakika ambao wamesajiliwa na wanaofika wenyewe siku ya uchaguzi ndio wanapiga kura.

Ni manufaa yapi ya BVR yaweza kulinganishwa dhidi ya sajili ya karatasi inayotumia mbinu ya Optical Mark Reader (OMR)?

BVR ina manufaa yafuatayo dhidi ya mbinu za zamani za usajili;

a) Kipekee: BVR hunasa maelezo ya kipekee ya mtu. Ni vigumu kabisa kuwa na watu wawili walio na data sawia za maumbile.

b) Haiwezi kutumiwa na watu wawili: Data za maumbile zinazonaswa na BVR ni hususan za mtu binafsi na haziwezi kunakiliwa ama kuwa za watu wawili (huwezi kumpa mtu nakala ya uso ama vidole vyako!) hii haikuwa hivyo katika sajili ya awali ambapo nambari za vitambulisho ama pasipoti zilizotumika kumtambua mpiga kura zilikuwa rahisi kubuni ama kunakili.

c) Haiwezi kunakiliwa: Ni vigumu kabisa kubuni ama kudanganya maumbile. Hii inahakikisha maelezo yanayotolewa ni ya mtu aliye hai.

d) Haiwezi kupotea: Maumbile ya mtu yaweza tu kupotea katika ajali mbaya kabisa kinyume na sajili ya karatasi ambapo mpiga kura aweza kupoteza kadi yake ama kitambulisho na kikatumiwa na mlaghai kupigia kura.

e) Sahihu: BVR hunasa maelezo ya mpiga kura moja kwa moja katika kifaa cha teknolojia. Mpiga kura huthibitisha data hii kabla haijaakibishwa. Hii huchangia kuwepo kwa sajili sahihi nay a kuaminika.

f) Haraka: Mbinu hii hutoa fursa ya kunaasa maelezo kwa haraka na data hiyo haihitaji kuchambuliwa na kutengenezwa tena. Hii inakuwa haraka kuunganisha sajili ya wapiga kura kinyume na mbinu ya zamani iliyohitaji data kukaguliwa na kutengenezwa.

g) Epesi na sawasawa: BVR inahakikisha mpiga kura anatambulika kwa wepesi na sawasawa na ni msingi wa uchaguzi wowote wa kuaminika. Mbinu hii inatoa viwango vya juu kabisa vya usalama wa kupiga kura na inazuia udanganyifu katika uchaguzi.

Je, kuna mataifa mengine kando na Kenya ambayo yametumia BVR?

NDIO! Mataifa haya ni Ghana, Nigeria, Gambia, DRC, Zambia, Sierra Leone, Namibia na Msumbiji.

Je, BVR ni salama?

Mifumo ya kutambua na kuthibitisha data za maumbile zimetumika kwa zaidi ya miaka 25. Mbinu zinazotumika katika BVR hazina madhara yoyote ya kiafya.

Je, mahitaji yapi yafaa kutimizwa na mtu ili asajiliwe kwa kama mpiga kura kwa kutumia BVR?

Kusajiliwa kama mpiga kura unahitaji kufika mwenyewe katika kituo cha usajili ukiandamana na stakabadhi zifuatazo za kujitambulisha;

a) Kitambulisho cha kitaifa ama
b) Pasipoti

Maelezo yapi yatanaswa na BVR?

Habari zitakazonaswa na BVR ni pamoja na: jina la ukoo na majina mengine, tarehe ya kuzaliwa, umri, jinsia, alama za vidole, picha ya uso, na data za uchaguzi (eneo bunge, vituo vya usajili na kadhalika).

Je, mtu asiye na mikono aweza kusajiliwa kwa kutumia BVR?

Iwapo hakuna mikono, BVR inatoa fursa kwa hali za kipekee ambapo wapiga kura walio na ulemavu wanaambatishwa ipasavyo na nyuso zao kutumiwa kuwasajili na kuwatambua.

BVR itaendeshwaje?

Watu wote wafaa kufika wenyewe katika vituo vilivyotengwa kwa usajili (yaani, vituo vya kawaida vya kupiga kura) ili kusajiliwa kama mpiga kura.

a) Usajili; awamu ya kujiandikisha. Data zifuatazo za maumbile zitanaswa: majina kamili ya anayesajiliwa, tarehe ya kuzaliwa, jinsia, alama za vidole, picha, kituo cha uchaguzi (kituo cha kupiga kura, wodi ya kaunti, eneo bunge na kaunti), namabari za mawasiliano, hali ya usajili, nambari spesheli ya mpiga kura, aina ya stakabadhi ya kumtambua (kitambulisho cha kitaifa ama Pasipoti), na stakabadhi ya kumtambua.

b) Utengenezaji: Seva Kuu ya Maumbile (Central Biometric Server) inayotumia teknolojia ya kisasa ya kutambua alama za vidole, Automated Fingerprint Identification System (AFIS) itatengeneza rekodi za wapiga kura ili kutambua rekodi zilizonakiliwa. Rekodi hizi spesheli zitatengeneza sajili ya muda kwa kila kituo cha usajili/kupiga kura. Orodha maalum ya waliojisajili marudufu na kasoro zingine katika shughuli ya usajili kwa kila kituo cha usajili/kupiga kura pia
itatayarishwa.

c) Sajili ya muda ya wapiga kura itachapishwa pamoja na orodha hiyo maalum ya kasoro zitapelekwa katika kibtuo cha usajili/kupiga kura ili kukaguliwa.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.