Blogu: Waraka wa Warungu

Image caption Mratibu wa kipindi Joseph Warungu.

Tulipofunga safari kuelekea kaskazini mashariki mwa nchi kwa mjadala wa Sema Kenya wiki hii, ya kutia moyo yalinilaki bega kwa bega na ya kuvunja moyo.

La kwanza ni kwamba ingawaje mjadala wetu ulihusu usalama katika kaunti ya Garissa, hatungeweza kuendesha kipindi chetu huko Garissa kutokana na sababu za kiusalama.

Hilo lilikuwa ni la kusikitisha - kwamba kuna baadhi ya sehemu za nchi usizoweza kufika kwa hofu ya usalama.

Kwa hivyo ilibidi tupige kambi katika mji wa Mwingi, ulio kaunti ya Kitui. Lakini tulijitia moyo tukikumbuka kwamba Mwingi na Garissa ni pua na mdomo.

Jambo la kwanza la kutia moyo lilikuwa ni barabara.

Kutoka Nairobi kuelekea Mwingi - umbali wa kilomita 160, njia ni ‘nywee’ kama alivyozoea kusema mwanasiasa mmoja mashuhuri wa Kenya.

Kwa maana kwamba unaweza kulala usingizi mnono wa saa tatu - ambao ndio muda wa safari hiyo ukiendesha kwa mwendo wa taratibu - bila ya kugutuliwa na mashimo barabarani.

Jingine la kutia moyo ni kwamba tulipowasili Alhamisi jioni ili kujiandaa kurekodi kipindi chetu Ijumaa, tuliwapata wakaazi wa Garissa walioalikwa kushiriki mjadala tayari wamefika.

Moyo wangu pia ulijawa na furaha nilipogundua kwamba Mwingi msimu huu sio joto sana.

Hili ni muhimu kwangu, kwa sababu kama mratibu wa kipindi, kazi yangu kubwa huwa ni kusimama kwenye jua kali nikipigana mieleka ya maneno na viongozi katika kutafuta ukweli wa mambo.

Basi eneo likiwa na joto kali, kijasho hunitiririka mfano wa maporomoko ya maji, hadi hatimaye ikabidi kubadilisha shati nililovaa baada ya kulowa jasho.

Kitu kingine cha kutia moyo siku ya kurekodi kipindi ni pale tulijua kwamba wanajopo wetu wote wane walifika uwanjani kwa saa walizopangiwa bila ya kuchelewa.

Image caption Mratibu Joseph Warungu akiwauliza wanajopo maswali wakati wa mjadala wa Garissa.

Katika msimu wetu wa kwanza wa Sema Kenya tulikuwa tumezoea kuishi kwa wasiwasi kutokana na kuechelewa kwa viongozi walioalikwa kwenye jopo.

Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba nilikuwa na hofu Mhariri wangu Caroline Karobia, atapatwa na mshtuko wa moyo siku moja, baada ya kushurutishwa bila huruma na wanajopo wetu waliokuwa na mazoea ya kuchelewachelewa au kutofika kabisa kwenye uwanja wa majadiliano.

Punde wananchi waliofika kushiriki mjadala walopoanza kuingia uwanjani na kukaa tayari kwa kipindi, nilikumbushwa kwamba Kenya ina watu wa dini, mila na tabaka mbalimbali.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kabisa katika vipindi vyetu kwa wanawake kukaa sehemu yao tofauti na wanaume – kawaida wote huwa wanajumuika pamoja.

Siku zote za matayarisho, muda wote wa kuingiwa na wasiwasi huyoyoma punde tu msimamizi wa kipindi anapoanza kunihesabia sekunde zilizosalia: “…tano, nne, tatu, mbili, moja….Warungu uko hewani sasa!”

Basi kwa tabasamu la kutoka moyoni, mimi hugeuka kutizama kamera na kunena: “Hujambo na karibu kwa Sema Kenya…”

Huko Mwingi nilidhani kwamba swala la usalama kaunti ya Garissa litakuwa ni swala zito la kuzua hisia nzito na maneno makali.

Lakini nilishangaa wakaazi wa Garissa walipoanza kusimulia sio tu athari za mashambulio mengi ya kigaidi yanayotokea mara kwa mara huko, bali jinsi wanavyonyanyaswa na vyombo vya usalama vikiwa katika harakati za kuwasaka wahalifu.

Mtu mmoja alieleza jinsi alivyolazimishwa kulala kifudifudi, kichwa ndani ya maji ya mtaro eti atege samaki kwa mdomo wake.

Kamishna mpya wa kaunti ya Garissa alisikiliza kwa makini kilio cha raia na kuahidi kuchukua hatua dhidi ya afisa yeyote atakayepatikana na makosa ya kuwaadhibu au kuwatesa raia.

Basi baada ya saa nzima ya maswali makali ya wananchi, na jopo kupata nafasi ya kujibu na kukariri maswala, nilifunga kipindi kwa kutafuta mapendekezo ya suluhu kwa swala gumu la kuzorota kwa usalama Garissa.

Joto la jua na lile la mjadala hatimaye lilifikia kilele na tulipoingia garini kwa safari ya kurudi Nairobi, nilishukuru kwamba barabara ni ‘nywee’ na kuyafunga macho, njozi kuzialika hadi kufika jijini.

Sasa kipindi cha Garissa kimepeperushwa hewani, tayari nimeanza matayarisho ya kipindi kipya cha wiki ijayo kitakachotupeleka hadi Kisii, magharibi mwa Kenya.