Mhariri wa Sema Kenya anasema…

Image caption Wanyama wa Chebusiri - Mhariri

Hujambo shabiki mpendwa wa kipindi chako cha Sema Kenya!

Msimu wa pili wa Sema Kenya umeng’oa nanga kwa kasi. Tayari tumezuru kaunti tano kati ya thelathini tunazolenga kutembelea katika msimu huu wa pili, na kuwapa fursa wenyeji kuwahoji viongozi wao kuhusu maswala nyeti yanayowakumba.

Athari za ukosefu wa usalama kaunti ya Garissa, jinsi huduma za serikali mpya ya ugatuzi hazijawafikia wakaazi wa Kisii, kutengwa kimaendeleo kwa muda mrefu huko Turkana, uhaba wa ajira kwa vijana jijini Nairobi, na umaskini uliokithiri katika kaunti ya Narok licha ya utajiri mkubwa na rasilimali nyingi, ni baadhi tu ya maswala ambayo yameng’amuliwa hadi sasa kwenye kipindi cha Sema Kenya.

Nairobi wiki hii

Serikali ya muungano wa Jubilee ya rais Uhuru Kenyatta inaadhimisha miezi mitatu tangu ichukuwe hatamu za uongozi nchini Kenya. Wakati wa kampeni Muungano huo wa Jubilee ulitoa ahadi nyingi tu ambazo iliahidi kutekeleza iwapo wangelichaguliwa.

Kwa hivyo, Sema Kenya Jumapili hii inarudi jijini Nairobi kukuuliza swali, je, katika siku mia moja za kwanza, serikali ya Jubilee imetekeleza wajibu wake kwa matarajio ya wakenya?

Tunakuletea vigogo wa serikali ya Jubilee kujibu maswali yako. Hii ni fursa kwako kuipiga msasa serikali yako, kwa hivyo nakusihi utembelee tovuti yetu ya bbcswahili.com\semakenya na kushiriki kwenye mjadala.

Kila wiki.

Kama mhariri wako, nimejitwika jukumu la kukuwasilishia ujumbe kila wiki kuhusu makala ya BBC Sema Kenya. Nitakudondolea machache niliyoyaona, niliyosikia na pia niliyosoma.

Kwa hivyo basi, naomba uendelee kutazama, kuskiliza na pia kusoma BBC Sema Kenya kila wakati.

Wanyama wa ChebusiriMhariri