Blogu: Waraka wa Warungu

Image caption Msimulizi wa kipindi Joseph Warungu (kulia) pamoja na washiriki waliohudhuria mjadala wa Narok.

Jamii ya Wamaasai ina uhusiano wa kipekee na maji. Kila sehemu Wamaasai walimotua hapo zamani, walipachika eneo hilo jina la Kimaasai kutokana na maji ya pale.

Nairobi kwa mfano inatokana na jina la Kimaasai enkare Nairobi, kumaanisha eneo la maji baridi.

Mji wa Narok nao ulipewa jina hilo la enkare Narok, kumaanisha maji meusi – kwa vile mto mmoja hapo Narok ulikuwa na maji ya rangi nyeusi.

Uhusiano huu wa karibu wa Wamaasai na maji pengine ni kwa sababu hii ni jamii ya wafugaji. Na kila mfugaji anazingatia mambo mawili muhimu – malisho ya wanyama wake na maji.

Lakini tulipofika Narok tuligundua kwamba sio maji tu yaliyokuwa na rangi nyeusi, bali maendeleo ya kaunti hiyo yana rangi isiokuwa ya kuvutia.

Elimu ni ya kiwango cha chini sana huku maelfu kwa maelfu ya wakaazi wa Narok wakiwa ni watu wasiojuwa kusoma na kuandika.

Barabara za Narok ni mbovu na hazipitiki. Hospitali nazo ni za kubahatisha.

Na licha ya uhusiano wa Wamaasai na enkare ama maji, bidhaa hii ambayo ni kiini cha maisha haipatikani kwa urahisi.

Sehemu nyingi za Kenya zina matatizo kama haya. Lakini kinyume na kaunti nyingi za Kenya, Narok ina utajiri mkubwa. Ukiacha Nairobi na Mombasa, Narok ndio kaunti ya tatu kwa utajiri.

Raslimali muhimu zaidi ya Narok ni hifadhi maarufu duniani ya wanyama pori ya Maasai Mara ambayo inaingiza zaidi ya shilingi bilioni mbili kila mwaka.

Narok pia ina utajiri mkubwa unaotokana na kilimo cha ngano, mahindi na shayiri.

Basi kwa nini kaunti yenye utajiri wa juu ikawa na maenedeleo ya chini? Hilo ndilo swali tulilotaka kutafutia jawabu katika majdala wetu.

Lakini pindi tu kipindi kilipoanza nilibaini kwamba utakuwa ni mchezo wa kukanusha na kulaumu.

Wananchi waliwataka viongozi wawajibike, lakini viongozi walisema wa kuajibika sio wao bali ni wale wa zamani.

Gavana wa kaunti ya Narok, Bw Samuel Tunai, alikabiliwa na kibarua kigumu kueleza ilikuwaje kwamba kandarasi ya ukusanyaji wa ada ya Maasai Mara ilipokonywa benki ya Equity na kupewa kampuni ambayo ana uhusiano nayo?

Tulipouliza raslimali ya Narok inamfaidi nani hasa, wananchi hawakusita kusema kwamba wanaofaidika sio wao walio wengi, bali wachache wenye mali na mamlaka.

Kwa mara ya kwanza kabisa tangu tuanze Sema Kenya nilishuhudia viongozi wakisusia jukwaa letu la mazungumzo. Mmojawapo wa wabunge tuliowaalika alisimama na kuondoka uwanjani akilalamika kwamba tulimvunjia heshima kwa kutomualika kukaa kwenye jopo.

Tukio hilo pamoja na kukatikakatika kwa umeme mtu anapokuwa bafuni akioga lilitoa sura ya mji na kaunti inayoyumbayumba kimaendeleo.

Kipindi chetu kilitoa nafasi kwa wananchi kuwasaidia viongozi wao kutambua ni maswala yapi ya muhimu zaidi ili yatengewe hela kubwa zaidi kutoka mfuko wa kaunti.

Tulipoondoka nilibaki kushangaa jinsi watalii wanavyotoka mbali kuja kustarehe na kuponda mali yao huku wakizingirwa na upepo tulivu wa umaskini wa hali ya juu.

Matumaini yangu ni kwamba maji ya Narok hatimaye yatageuka kuwa mafuriko ya utajiri kwa wananchi na afya ya hali ya juu.

Joseph Warungu