Mhariri wa Sema Kenya anasema

Image caption Mhariri wa Sema Kenya Wanyama Chebusiri

Kajiado imeorodheshwa kama kaunti yenye utajiri mkubwa sana nchini Kenya.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za tume inayosimamia mgao wa fedha, wakaazi wengi wa Kajiado wanaishi maisha ya viwango vya juu ikilinganishwa na wenyeji wa kaunti zingine.

Hata hivyo, huenda utajiri huu wa Kajiado ukaathirika vibaya kwenye mfumo mpya huu wa serikali za ugatuzi.

Kajiado ni pengine kaunti ya kipekee nchini Kenya ambapo kiongozi ni mateka wa bunge la waakilishi.

Kwa hivyo, jumapili hii katika makala yako unayoyapenda ya BBC Sema Kenya, tunapiga darubini kaunti ya Kajiado tukiuliza, je, ni vipi wakuu wa kaunti hii wanatekeleza majukumu yao huku wakikabiliwa na uhasama mkali wa kisiasa za vyama?

Sasa kwa mukhtasari turejelee magharibi mwa Kenya katika kaunti ya Siaya tulikopiga kambii wiki jana.

Siaya ni kitovu cha wasomi nchini Kenya.

Mbali na kuwa asili ya rais wa Marekani, Barack Obama, maprofesa wengi waliotabakaa sio tu nchini Kenya bali kimataifa wanatoka Siaya.

Waasisi wa siasa za upinzani na demokrasia kama vile hayati Jaramogi Oginga Odinga, mwanae aliyekuwa waziri mkuu, Raila Odinga, ni miongoni tu wa viongozi wa kisiasa waliobobea ambao asili yao ni Siaya.

Lakini licha ya sifa hizi hata za kimataifa, kiwango cha maendeleo ni cha kusononesha.

Kwa hivyo, ilikuwa bora sana kuona BBC Sema Kenya ikitoa fursa kwa viongozi na wenyeji wa Siaya kuzungumza bayana kuhusu swala hili.

Kwa hivyo, nakuomba katika misingi hiyo hiyo ya kuzungumza bayana bila shauku wala uoga, uchangie mada hii ya Kajiado kuwa kaunti inayokabiliwa na baraza linalokumbwa na mkorogo.

Karibu!!

Wanyama wa Chebusiri,

Mhariri, Sema Kenya.