Blogu: Waraka wa Warungu

Image caption Msimulizi wa Sema Kenya Joseph Warungu akijitayarisha kuanzisha mjadala wa Siaya.

Ingawaje nimezaliwa na kuishi Kenya miaka yote hii, kila nikitembelea sehemu tofauti ya nchi kwa makala ya BBC Sema Kenya, nakutakana na jambo jipya la kushangaza.

Baada ya kufika mjini Narok huko umasaini wiki mbili zilizopita, nilijulishwa kwamba majina ya miji mingi ya Kenya yanatokana na lugha ya Kimasai, kwa mfano Limuru wanamoishi jamii ya Wakikuyu na pia Eldoret kwa jamii ya Wakalenjin.

Wiki jana safari yetu ilitufikisha huko Siaya kando kando ya ziwa Victoria. La kushangaza hapa lilikuwa ni kwamba hii ndio kaunti ilio na maprofesa wengi zaidi kushinda sehemu nyingine yoyote ya Kenya.

Siaya pia ndimo wanamotoka watu mashuhuri kama vile babake Rais wa Marekani, Barack Obama na pia waziri mkuu wa zamani Raila Odinga. Naye James Orengo, mtetezi mashuhuri wa haki za wanyonge ndiye Seneta wa Siaya.

Siaya kadhalika inasifika kwa shule maarufu nchini Kenya, kwa hivyo sio ajabu kwamba ina wasomi wengi mashuhuri.

Hata hivyo, licha ya utajiri wake mkubwa wa akili, elimu katika kaunti ya Siaya ni ya kiwango cha chini hasa shule za msingi. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, Siaya ilishikilia nafasi ya 45 katika kaunti 47 kwa hali mbaya ya elimu katika shule za msingi.

Tulipowasili Siaya mjini kutayarisha kipindi chetu cha mjadala, gari letu lilipita maduka machache tukiwa mbioni kuutafuta mji wa Siaya. Tuliposimama kumwuliza bwana mmoja atuelekeze, alitujibu:

“Eti mwatafuta njia ya kuelekea mji wa Siaya?” aliuliza kwa mshangao.

“Mji ndio huu huu mnaouna," alitujibu huku akiashiria foleni ya majengo machache pembeni mwa barabara.

Sote tulipigwa na butwaa.

Yaani anamaanisha huu ndio mji na makao makuu ya Kaunti yenye sifa ya kimataifa ya Siaya? Nilibaki kujiuliza kimoyomoyo.

Baada ya duka la mwisho hapo mjini, barabara nzuri ya lami iliotufikisha Siaya iliyeyuka na kuwa mchanga, mashimo na vumbi.

Basi nilikuwa na hamu kubwa kusikia kutoka kwa watu wa Siaya kwa nini kuna mgon'gano huu wa akili za hali ya juu na elimu ya kiwango cha chini; au watu maarufu na umaskini mashuhuri.

Sababu moja kubwa iliotajwa kuelezea hali hii ni kutengwa kwa Siaya kisiasa.

Kwa vile mpinzani mkuu wa Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, marehemu Jaramogi Oginga Odinga alitokea Siaya, wenyeji wanadai serikali tangu miaka hiyo ya sitini ililipa kisogo eneo la Siaya.

Lakini sababu nyingine muhimu iliojitokeza katika mjadala wetu Siaya, ni kwamba baadhi ya wenyeji wa Siaya wakifanikiwa kimaisha na kitaaluma na kuhamia Nairobi na nchi za ulaya, wengi hawarejei nyumbani kuwekeza au kujaribu kunyanyua maisha ya waliochwa nyuma.

Basi serikali ya kaunti ya Siaya na viongozi wake walijipata taabani huku wananchi wakiwasakama koo wawajibike kwa hali duni ya maisha Siaya, na kuwabana wakariri mipango yao ya maendeleo.

Tulipofunga virago vyetu kuelekea Nairobi kupitia Kisumu, nilitizama nje ya dirisha kuona bararabara za kisasa zikijengwa karibu na uwanja wa ndege wa Kisumu.

Nilibaki kuomba kwamba siku moja maendeleo hayo hayo yatatanda na kupenya Siaya.

Waswahili wanasema kwamba elimu ni taa, gizani huzagaa. Natumai elimu ya juu ya watu mashuhuri wa Siaya itafikia kiwango cha kuwa mwangaza wa kufukuza giza la maendeleo duni huko Siaya.

Joseph Warungu,

Msimulizi, Sema Kenya