Mhariri wa Sema Kenya anasema...

Image caption Mhariri wa Sema Kenya Wanyama wa Chebusiri

Darubini ya BBC Sema Kenya wiki hii inalenga kaunti ya Kiambu, katikati mwa Kenya.

Kaunti hii, kwa mujibu wa takwimu za vyombo vya habari, ni kitovu cha watu wenye utajiri mkubwa zaidi nchini Kenya.

Pia, Kiambu ni mahali ambapo mtu maskini zaidi anapatikana.

Kaunti hii ilioko pembeni mwa mji mkuu wa Nairobi, pia inasifika kwa ukulima wa mashamba makubwa ya majani chai na viwanda vingi vilivyoko katika mji wa Thika.

Rais mwanzilishi wa taifa la Kenya Mzee Jomo Kenyatta, na mwanae ambaye ni kiongozi wa sasa, Uhuru Kenyatta, na aliyekuwa mfanya biashara maarufu marehemu Njenga Karume, ni miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kifedha kutoka kaunti ya Kiambu.

Jumapili hii tunaagazia ni jinsi gani rasilimali zilizoko Kiambu zinaweza kutumika katika juhudi za kuziba pengo kati ya mabwenyenye na walala hoi.

Sasa je, unadhani ni mbinu gani zitumike ili matumizi ya rasilimali ilioko, na utajiri mkubwa wa mali miongoni mwa baadhi ya wakaazi zinufaishe wenyeji wengi?

Kando na hayo, kwa muda wa wiki mbili ijayo, kuanzia Jumapili hii, naomba kukufahamisha kuhusu mabadiliko ya jinsi utakavyotazama kipindi chako unachokipenda cha BBC Sema Kenya kwenye runinga ya taifa ya KBC.

Kutokana na mashindano ya riadha ya dunia yanayoanza wikendi hii mjini Moscow, Urusi ambapo runinga ya KBC itakuwa ikirusha kinyang'anyiro hicho moja kwa moja, makala yako ya BBC Sema Kenya sasa yatakuja hewani kuanzia saa TATU NA DAKIKA HAMSINI za usiku Jumapili, badala ya saa kumi na mbili jioni.

Kumbuka mabadiliko haya ni ya wiki mbili tu kisha tutarejelea utaratibu wetu wa kawaida.

Wiki jana wakaazi wa kaunti ya kajiado walitoa tahadhari kwa viongozi wao wanaozozana na kulemaza utekelezwaji wa maendeleo katika kaunti hiyo.

Akina mama, wazee na hata vijana walisihi jopo la viongozi waliohudhuria kikaao hicho kuacha tofauti zao za kisiasa na kuzingatia upangaji na utekelezwaji wa miradi ya maendeleo ili kuinua hali ya maisha ya wakaazi wa kaunti ya Kajiado.

Wanyama wa Chebusiri

Mhariri