Blogu: Waraka wa Warungu

Image caption Msimulizi wa Sema Kenya Joseph Warungu (kushoto) na Gavana wa Isiolo Godana Doyo.

Eneo la Isiolo, kaskazini mwa Kenya lina msururu wa sifa mbaya.

Ya kwanza ni sifa ya machafuko ya mara kwa mara baina ya jamii mbalimbali. Na si ajabu kuwa na mizozo ya aina hiyo, kwani Isiolo inawajumuisha watu wa jamii tofauti kama vile Waborana, Waturkana, Wameru, Wasamburu na hata Wanubi.

Pili kaunti hii pia inasifika kwa umaskini na njaa, huku ikikadiriwa kwamba zaidi ya nusu ya wakaazi wake hutegemea misaada ya chakula kutoka kwa serikali na mashirika yasiyokuwa ya serikali.

Hali hii husababishwa na ukame unaowaathiri wakaazi wa hapo ambao wengi wao ni wafugaji.

Misaada hiyo ya chakula imetolewa kwa miaka mingi sana kiasi kwamba wenyeji wa Isiolo na mashirika ya misaada sasa wamekuwa ni kama mapacha wasioachana.

Ni jambo linalojukilana wazi kwamba Isiolo imetengwa na kusahaulika kisiasa na kiuchumi na hivi kuwaacha wenyeji wake bila mbele wala nyuma.

Ukabila pia na siasa za mapendeleo baina ya koo za wakaazi wa eneo hili zimechangia pakubwa katika kuachwa nyuma kwa Isiolo.

Hata hivyo, sura ya kaunti hii inatarajiwa kubadilika sana baada ya kutimia kwa ruwaza ya serikali ya Kenya mwaka wa 2030.

Kaunti hii karibuni itakuwa na jiji jipya na la kisasa kuwavutia wageni wanaotembelea mbuga maarufu za wanyama kama vile Buffalo Springs, Shaba na Bisanadi.

Ipo pia hifadhi ya wanyama inayosimamiwa na watu binafsi ya Lewa Downs ambayo imeshikanisha kaunti tatu – Isiolo, Meru na Laikipia.

Na si hayo tu. Hapo Isiolo panajengwa uwanja mpya wa kimataifa wa ndege huku kukiwa na mipango mingine ya kufungua kichinjio kikubwa cha kuhudumia eneo lote la kaskazini mwa Kenya.

Wakati huo huo kuna mradi mkubwa wa kujenga barabara, reli na njia ya kusafirishia mafuta kutoka Sudan Kusini hadi bandari mpya ya Lamu kupitia Isiolo.

Mradi huu wa mawasiliano utakapokamilika, utawezesha eneo lote la kaskazini mwa Kenya kufunguka na kufikika huku Isiolo ikiwa ni kama lango kuu.

Basi tulipowasili mjini Isiolo kwa mjadala wa wiki hii, tulitarajia kwamba kipindi kitachangamka kwa maswali na majibu ya kutalii mambo haya yote yanayoizingira kaunti.

Na kwa kweli hatukukosea. Punde tu nilipomaliza tangazo langu la kufungua kipindi na kuanzisha mjadala, nilinyeshewa na maswali na maoni mazito ya wakaazi wa Isiolo yaliyoelekezwa kwa Gavana wao, Bw Godana Doyo.

Na hata kabla ya mheshimiwa Gavana kupewa nafasi ya kupumua kidogo, alishambuliwa vikali pia na mwanajopo wetu mmoja, Bi Tiyah Galgalo ambaye ni mbunge wa kiti cha akina mama kutoka Isiolo.

Bi Galgalo alilalamikia utendaji kazi wa Gavana na pia kutokuwa na usawa wakati wa kutoa nafasi za kazi kwa wananchi wa Isiolo.

Gavana alipata nafasi ya kujitetea na kueleza sera za serikali yake ya kaunti, lakini wananchi hawakukoma kumsakama koo.

Mada yetu ilikuwa ni kuhusu ugavi wa raslimali za Isiolo kwa njia ya wazi na usawa. Na tulipofika tamati ya kipindi chetu, ilikuwa ni wazi kwamba usawa ni kitu ambacho kitaendelea kutafutwa kwa nguvu hapo Isiolo.

Tofauti na msimu wa kwanza wa Sema Kenya uliokuwa kabla ya uchaguzi mkuu, katika msimu wa sasa, wananchi wako tayari kabisa kwa meno na makucha makali kumvamia kiongozi yeyote ambaye hatoi tamko la kuridhisha jinsi mali ya umma inavyogawanywa na kutumika.

Sasa tusubiri maswla ya Nairobi wiki ijayo – sijui kama nako huku moto wa kutetea maendeleo utazimika.

Joseph Warungu,

Msimulizi wa Sema Kenya