BLOGU: Waraka wa Warungu

Image caption Msimulizi wa Sema Kenya Joseph Warungu (kushoto) na Gavana wa Bomet Isaac Ruto.

"Kwa nini Kenya siku zote inakuwa katika harakati za kampeini za uchaguzi? Jamani, kwani uchaguzi wenu haumaliziki?”

Hilo ni swali ambao ninaulizwa mara kwa mara ninapotembelea nchi nyingine za Afrika, huku watu hao wakifikia uamuzi kwamba Wakenya bila shaka wanapenda sana siasa.

Wiki hii tulipofika kwenye ukumbi wa mjadala wetu katika chuo kikuu cha Multimedia huko maeneo ya Ongata Rongai, swala hili la Wakenya na msururu wa siasa zisizokwisha uliniteka akili.

Mada ya mazungumzo ilikuwa ni kutathmini changamoto za mfumo wa utawala wa ugatuzi.

Hii ni kufuatia kampeni kubwa ya magavana wengi wanaotaka katiba ibadilishwe, ili serikali ya taifa ishurutishwe kugawa kiwango kikubwa zaidi cha fedha kwa serikali za kaunti.

Juhudi hizo za magavana zikifanikiwa itawabidi wakenya kurejea kwenye vituo vya kupigia kura ili kushiriki katika kura ya maoni kuamua iwapo wangependa katiba ibadilishwe.

Hii ni kwa sababu kisheria marekebisho makubwa ya katiba yanahitaji wananchi washauriwe kupitia kura ya maoni.

Basi wiki hii katika jopo letu tuliwakutanisha watu mashuhuri katika swala hili la utendaji kazi wa serikali za kaunti na utaratibu mzima wa kufanikisha ugatuzi.

Isaac Ruto ni gavana wa kaunti ya Bomet katika muungano unaotawala wa Jubilee na pia ni mwenyekiti wa baraza la magavana.

Yeye amekuwa katika mstari wa mbele kudai fedha nyingi zaidi kutoka kwa serikali ya taifa.

Mgeni wa pili alikuwa ni Hassan Omar ambaye ni Seneta wa Mombasa katika muungano wa vyama vya upinzani vya CORD.

Yeye anaunga mkono kubadilishwa kwa katiba ili baraza la Seneti lipewe mamlaka zaidi ya kusimamia shughuli za serikali za kaunti.

Mwanajopo wa tatu alikuwa ni Kinuthia Wamwangi, mwenyekiti wa mamlaka ya mpito.

Kama kiongozi wa mamlaka hii inayosimamia utekelezaji wa mfumo wa ugatuzi, msimamo wake ni kwamba angetaka kura hiyo ya maoni iahirishwe kwa muda ili kumpa nafasi ya kuzisaidia serikali za kaunti kuimarisha utendaji wake wa kazi.

Mgeni wa mwisho alikuwa ni Agnes Odhiambo ambaye ni mdhabiti wa bajeti za kaunti.

Yeye ana jukumu la kuzichunguza kwa makini bajeti hizo kisha aziiidhinishe ili serikali ya taifa iweze kugawa hela zilizokubaliwa.

Bi Odhiambo alieleza kuhusu matumizi ya ajabu ajabu ambayo yaliwekwa kwenye makadirio ya pesa na baadhi ya kaunti, kama vile pesa za starehe na ununuzi wa magari na mavazi ya viongozi.

Kwa hali hii, kwa nini basi magavana wanadai hela zaidi ilhali senti chache walizonazo hazijalengwa vizuri kwa maswala muhimu ya maendeleo kama vile afya na elimu?

Gavana Ruto alijitetea vikali akisema kwamba kipato walicho nacho ni kidogo mno kukidhi mahitaji yote muhimu ya maendeleo ya serikali za kaunti.

Kwa hivyo hawana budi ila kushinikiza kubadilishwa kwa katiba ili kiwango wanachopata kutoka kwa serikali ya taifa kiwe ni asilimia 40 ya mapato yote ya serikali hiyo, badala ya kiwango cha sasa cha asilimia 32.

Seneta Omar naye aliunga mkono wito wa Bw Ruto na kusema kwamba baraza la Seneti tayari linaandaa mipango ya kubuni kamati kadha ambazo zitarahisisha usimamizi wa serikali za kaunti.

Kwa kumjibu Bw Wamwangi kwamba wawe na subira na wasiharakishe kuitisha kura ya maoni, Bw Omar alitumia msemo wa Kiswahili unaosema kwamba ‘kama sio sasa basi ni sasa hivi’.

Kwa maana kwamba mabadiliko ya katiba yafanyike pasipo kuchelewa ili mgongano wa sasa wa kimawazo baina ya serikali za kaunti pamoja na senate dhidi ya serikali ya taifa usigeuke kuwa janga.

Yalikuwa ni mazungumzo moto yaliyozua hisia mbalimbali.

Muhimu kilichojitokeza ni kwamba ni wananchi wachache sana ambao wanauelewa vizuri mfumo mpya wa serikali za ugatuzi.

Lakini licha ya hayo, na licha ya kwamba haijatimia hata miezi sita tangu kufanyika uchaguzi mkuu, huenda Wakenya tena wakajikuta kwenye kura ya kuamua vita vya sasa baina ya serikali ya taifa na serikali za kaunti.

Joseph Warungu,

Msimulizi wa Sema Kenya