Wanawake wameafikia nini?

Elimu ya wasichana ni moja ya changamoto zinazowakabili wanawake duniani katika nchi zinazostawi. Barani Afrika elimu kwa wasichana inakumbwa na changamoto zaidi kwa sababu ya umasikini, kutopatikana kwa elimu yenyewe na changamoto zengine za kijamii.

Katika maeneo ya vijijini shule za sekondari ni chache na zilizopo ziko mbali.

Gharama ya kuishi katika shule za mabweni kwa wasichana Tanzania ni tatizo kwa familia nyingi na hivyo wasichana hulazimika kukodisha vyumba nje ya shule hizo na hivyo kuhatarisha maisha yao kwani wanaweza kubakawa na kutendewa dhuluma nyenginezo.

Mwandishi wa BBC Tulanana Bohela, alitembelea shule moja ya sekondari mkoani Rukwa na kujionea hali ya wasichana wakijitahidi kupata masomo.

''Ni wakati wa mapumziko katika shule ya sekondari ya Mzindakahya. Nawaona wanafunzi wanakusanyika kwa mkutano wa kila asubuhi na walimu wao , na katika shule hii kila kitu kinaoenaka kuwa shwari.'' Lakini baada ya tukio la hivi karibuni ambapo mwanafunzi mmoja alijitoa uai baada ya kushambuliwa na kubakwa katika chumba anamoishi na mwenzake nje ya shule hii,mambo hapa hayajakuwa kama kawaida.

''Wakati huu wa mapumziko , nazungumza na msichana mmoja ambaye alikuwa anaishi na msichana aliyejitoa uhai katika chumba kimoja. Yeye pia aliathirika.

Msichana huyu kwa jina Anna, anasema kuwa ilikuwa karibu usiku wa manane wakati waliposhambuliwa na watu ambao hawakuwajua. Mmoja wao alimshika kwa lazima mwenzake na kuanza kumbaka na mwengine pia alimbaka.

Anasema kuwa hakufahamu alichokuwa anakitafakari rafiki yake wiki mbili baada ya kitendo hicho, alimpata amejinyonga lakini hakuwahi kuzungumzia kilichokuwa kinamsumbua akilini.

Katika eneo hili kulingana na msichana mwengine, Ruth wanaofanya unyama huo hawaonekani kuchoka kwani karibu kila siku wanajaribu kuwabaka

Anaelezea kuwa wabakaji walivamia chumba chao kwa visu na kuwatisha huku wakiwalazimisha kuwapa pesa. Lakini,licha ya kuwapa pesa angalau dola moja bado waliwashambulia na kuwachapa.

Maafisa wa utawala katika shule hiyo wanasema kuwa wamepokea angalau ripoti za visa vitano vya ubakaji na mashambulizi ya aina nyingine dhidi ya wasichana lakini huenda visa hivyo vikawa vingi zaidi.

Naibu mkuu wa shuke hiyo Agatha Okumu anaelezea kuwa ni vigumu kubaini idadi ya matukio ya mashambulizi bila ya ushirikiano na jamii kwa ujumla.

Visa kama hivi havitokei tu katika shule hii.

Utafiti uliofanywa na shirikisho la wanawake katika vyombo vya habari katika mikoa 10 kote nchini , Tanzania, unaonyesha kuwa zaidi ya visa 300 vya dhuluma za kingono , viliripotiwa kisiwani Zanzibar pekee kati ya mwaka 2011 na 2013.

Wasichana katika shule hiyo wanalazimika kukodisha vyumba vya pesa kidogo kwa sababu wanatoka katika familia masikini ambazo haziwezi kumudu gharama ya pesa zinazotoza na shule za mabweni.

Baadhi ya wasichana hujipata wameolewa na wazee na kuacha masomo. Lakini kutokana via vingi visivyoripotiwa, pamoja na sheria duni za kukabiliana na tatizo hili, elimu kwa wasichana inaendelea kuwa ghali sana kila kuchao.