Uandishi lazima uheshimu Lugha Asili

Image caption Prof. Abbas Kiyimba ni mhadhiri wa Chuo kikuu cha Makerere, Uganda. Kutoka kitivo cha fasihi na lugha. Amechaguliwa miongoni mwa maprofesa saba, katika mpango wa ushirika, chuo kikuu cha Cambridge kufanyia utafiti Fasihi ya Afrika. Profesa ameanza mradi wa kutafsiri vitabu maarufu vya waandishi wa ki- Afrika, kwa lugha za kiasili Afrika.

BBC ilipata fursa ya kuzungumza na Prof. Kiyimba mjini London

(Usikose kusikiliza mahojiano kamili na Prof. Kiyimba katika Dira ya Dunia , Alhamisi 6 Februari 2014)

Swali: Umeshinda tuzo ya kuja Uingereza kwa masomo zaidi.

Prof: Kuna Programme ya kufanyia utafiti wa Fasihi barani Afrika na tulishindania wengi...

Swali: Kwa hiyo wewe ni mmoja wa walio shinda, mlikuwa wangapi?

Prof: Tulishindana watu 24 na walikuwa wanataka 7. Na nilikuwa mmoja wa hao 7.

'Hongera sana...'

Swali: Umehusika katika kutafsiri baadhi ya vitabu maarufu Afrika, tueleze zaidi juu ya hilo.

Prof: Uganda tunazo lugha kama 33 za kienyeji. Kwa hivyo tuna tatizo la kusikilizana kama wananchi. Mwandishi mmoja anaandika kitabu kwa lugha yake na hatuna namna ya kuwezesha Waganda wenzake kujua anasema nini. Kuna mwandishi mmoja maarufu, 'Okot p'Bitek' aliandika kitabu ' Song of Lawino'. Mwanzoni alikiandika kwa lugha yake ya 'Kicholi'. Na baadaye alikifasiri kwa lugha ya kiingereza. Kwa ki-Acholi kilikuwa 'Wer Pa Lawino' . Kwa kiingereza kikawa 'Song of Lawino'. Na kilipata umaarufu sana. Na mimi niliona itakuwa vizuri sana nikitafsiri kwa lugha nyingine za nyumbani maanake kina mambo mengi mazuri sana. Nilianza kwa lugha ya kiganda polepole, na chuo changu kikanifadhili kuendelea mpaka nimemaliza.

Hofu ya Uandishi

Swali:Kama waandishi wa vitabu je hamuoni hatari ya kupoteza maana ya kitabu kimoja katika tafsiri?

Prof: Ndio hatari hiyo ipo, lakini, baada ya kutafsiri, kabla ya kuchapisha, wanampa msomi mmoja na wa pili na wa tatu kupitia ili kuhakikisha maana haikupotezwa katika tafsiri. Ni muhimu kuwe na tafsiri ili watu waweze kuelewana.

Ushauri nasaha

Swali: Unaweza kuwashauri vipi vijana wanaotaka kuingia katika uandishi sasa, hasa juu ya matumizi ya lugha?

Prof: Lugha yoyote, ili ikue, ni lazima kuwe na mambo yaliyoandikwa kwa lugha hiyo. Na ushauri wangu ni kuwa, andika! Hata kama ni ukurasa mmoja. Pili, usijali kama kitabu chako kitasomwa au la. Wewe andika, na utapata wasomi japo wachache. Tatizo ni pale kuanza. Na ukiogopa kuanza utapotea kabisa.

Swali: Unaweza kusema waandishi wa ki-Afrika wanatambulika nje ya Afrika?

Prof: Kwanza waandishi wa Kiafrika wanaotambuliwa nje ni wale walioandika kwa lugha ya kikoloni. Na wamefanya kazi nzuri kwa sababu wakoloni wengine hawakujua kuwa sisi pia tunao utamaduni wa kuheshimiwa. Lakini baada ya kusoma vitabu kama 'Things Fall Apart' na 'River Between' na kadhalika, sasa wameelewa kwamba Waafrika wana utamaduni wa kuheshimiwa. Lakini hivyo vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya kikoloni havieleweki kwa Waafrika wenyewe. Wale wasiojua kiingereza hawawezi kuvisoma vitabu hivi kwa kiingereza. Kwa hivyo ni lazima tutafsiri hivyo vitabu kwa lugha ya Kiafrika ili wale wanaozungumza hiyo lugha waweze kujua waandishi wao wanasema nini. Ndilo jambo lililonifanya nianze kutafsiri 'Song of Lawino'.