Unawajua wasimulizi wako?

Wasimulizi wa BBC Sema Kenya

Joseph Warungu

Warungu ana uzoefu wa miaka mingi kama mwandishi wa habari nchini Kenya na pia kimataifa katika shirika la BBC.

Akiwa BBC alisimamia vipindi vya “Focus on Africa” na “Network Africa”. Alikuwa pia mhariri mkuu wa jarida la “Focus on Africa.”

Warungu alitumikia kazi vituo vya BBC Redio na TV kwa takriban miaka ishirini.

Awali alikuwa mwanahabari katika vituo vya televisheni vya KBC na KTN.

Ameendesha mijadala ya umma kuhusu masuala ya utawala bora na maendeleo. Katika kazi yake ya uandishi amekutana na kuwahoji viongozi wengi duniani kwa mfano Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown; Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter; Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan na marais wengi wa Afrika.

Maryam Dodo Abdallah

Maryam ni mtangazaji na mwandishi habari aliye na uzoefu nchini Kenya na kimataifa kwa miaka takriban kumi sasa.

Kabla ya kujiunga na BBC, Maryam amefanya kazi na Deutsch Welle Ujerumani, Royal Media Services na KBC nchini Kenya.

Katika kazi yake, Maryam Dodo Abdalla anafurahia zaidi kutangamana na wananchi mashinani na kupata kutambua matatizo halisi na kusaidia kwa kuyaangazia wazi, kubadili upeo wa mambo, na kuleta mabadiliko bora katika jamii.

Bonnie Musambi

Bonnie ni mtangazaji mwenye uzoefu mwingi. Haswa anajulikana kwa kipindi chake cha Zinga la Asubuhi katika Radio Taifa ya KBC, pia ni mtangazaji wa habari katika kituo hicho.

Kabla ya kujiunga na KBC, Bonnie alikuwa mtayarishi wa vipindi katika Baraka FM Mombasa. Aliteuliwa kufanya mafunzo maalum kuhusu uhalifu wa kimataifa nchini Uholanzi.

Anapenda kuratibu kipindi cha Sema Kenya kwa sababu anapata nafasi ya kuwapa Wakenya jukwaa la kujadili masuala na wataalam na viongozi vilivyo.