Waingereza na ubaguzi wa rangi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bendera ya Uingereza

Jamii ya Waingereza ni ya watu wanaotoka matabaka mbalimbali, lakini je, wako huru kiasi gani inapokuja suala la kuzungumzia ubaguzi wa rangi na ukabila.

Katika makala ya televisheni inayotakiwa kurushwa leo hii, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha kuangalia usawa nchini Uingereza, Trevor Phillips, ametoa madai kadhaa ambayo ni tata.

Miongoni mwa hayo, lililojitokeza sana, ni lile la kupandikiza heshima kwa watu wa jamii ndogo, na kuondoa hali ya kuchukiana, imefanya baadhi ya watu kuogopa kujadili mambo muhimu kwa hofu ya kuonekana wana ubaguzi wa rangi.

Kama mwenyekiti wa Kamisheni ya kuangalia usawa nchini Uingereza muongo mmoja uliopita, Trevor Phillips alitumia siku kadhaa kila wiki nje ya ofisi yake ya London, huku akikutana na watu wanaotoka katika jamii ndogo nchini kote.

Akiwa ni mtoto mhamiaji mwenye asili ya Afro-Caribbean, kazi yake ilikuwa kujenga hali ya ustahamilivu katika jamii ambayo inakuwa kwa kasi.

Hata hivyo, wiki hii, amekiri kwamba anajua kuna watu wanaopandikiza fikra hasi, lakini alishindwa kuchukua hatua.

Halafu, ilipofika mwaka 2005, kulitokea mashambulizi ya mabomu ya London, yaliyotekelezwa na waingereza wazawa waislamu, na kusababisha vifo vya watu hamsini na mbili huku wengi wakijeruhiwa.

Bwana Phillips hivi sasa anasema ana wasiwasi iwapo atahitajika kuwajibika kwa kushindwa kuona kitu gani kiko mbeleni.

Je, kwa nini alishindwa kutoa tahadhari?

Chama cha kisiasa cha UKIP kinataka kuthibiti uhamiaji.

Katika makala ya televisheni iitwayo 'things We Won't Say About Race That are True,' yani mambo tusiyoyazungumza kuhusu asili na ambayo ni kweli, anasema siasa za Uingereza na vyombo vya habari zinaogopa kuzungumzia maswala ya dini au rangi kwa kuhofia tuhuma za kupandikiza chuki.

Bwana Phillips anasema, hofu hiyo imeleta mambo mawili, la kwanza ni kusita kuzungumzia tatizo ndani ya jamii, hivyo kushindwa kulitatua.

Pili, ni ukuaji wa vuguvugu za kisiasa zinazochochewa na Waingereza wazawa ambao wanaiona jamii yao ikibadilika huku wakijihisi kudharauliwa na wanasiasa wakuu.