Fainali ya 2008

Ashura Kisesa, raia wa Burundi, wakati huo akiwa na umri wa miaka 24, ndiye aliibuka mshindi wa Faidika na BBC 2008. Alikabidhiwa zawadi ya juu ya shindano hilo na Waziri mkuu wa Uganda, Bw Apolo Nsibambi.

Bi Ashura alikabidhiwa tuzo maalum pamoja na hundi yenye thamani ya dola elfu tano za Marekani, ili aweze kuanzisha mradi wake wa kujenga vyoo vya kulipia, katika miji ya Afrika Mashariki na Kati.

Ashura Kisesa, alikuwa msichana pekee aliyeingia kwenye fainali hizo, zilizorushwa moja kwa moja, kupitia BBC Idhaa ya Kiswahili na Televisheni ya UBC, aliwashinda vijana wengine wanne, kwa kuwashawishi majaji na jinsi atakavyotumia fedha za zawadi kuanzisha mradi wenye mafanikio na kunufaisha jamii inayomzunguka.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Uganda, Profesa Apolo Nsibambi alisema “ Wakati shindano hili likianzishwa mwaka jana, hawakuwepo wasichana katika fainali, hivyo natoa pongezi kwa Ashura. Natoa wito kwa BBC kuchukua hatua thabiti kuhimiza wanawake zaidi kuingia katika biashara. Hii ni jitihada nzuri ya BBC ya kusaidia vijana kuwa wabunifu na kuwafanya wawe waundaji wa nafasi za kazi, badala ya kuwa watafutaji kazi.”

Wakati akiingia fainali Bi Ashura alikuwa mwanafunzi wa uchumi wa kilimo (agronomia) katika chuo kikuu cha Burundi.

Ashura alishiriki katika shindano la Faidika na BBC 2007 lakini hakupata mafanikio. Hatimaye ndoto hiyo ilitimia kwa Ashura kutokana na kuibuka mshindi wa jumla wa Faidika na BBC 2008, kwenye fainali iliyoungura Kampala, Uganda.