Fainali ya 2009

Mshindi wa 2009
Image caption Jane Mueni, mshindi wa Faidika 2009

Faidika na BBC 2009 ina malikia mpya, Bi Jane Mweni, raia wa Kenya ambaye aliwabwaga washindani wenzake watano kwenye fainali zilizofanyika Mombasa tarehe 13 Agosti 2009.

Bi Mweni ambaye anasubiri matokeo ya mitihani yake ya elimu ya diploma, aliwasilisha mchanganuo wa kuanzisha biashara ya kuzoa katika jiji la kitalii la Mombasa ambako anaishi.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Bi Mweni alibainisha kuwa ameishiwa maneno kutokana na furaha ya ushindi: "Nimeishiwa maneno....hapa nilipo natetemeka!"

Vijana sita walifuzu kuingia katika fainali za 2009. Washindani mwaka huu walikuwa Nyota Anjelique Kikukama kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Chiza Bonye wa Burundi, Hakizimana Aladin aliyeiwakilisha Rwanda, Gakuo Roy wa Uganda, Mbaraka Juma kutoka Tanzania na wenyeji Kenya waliibuka kidedea baada ya ushindi wa Jane Mweni.

Mshindi alijizolea dola elfu tano za kimarekani (US$ 5,000) pamoja na kikombe. Vile vile atapata fursa ya kusafiri kwenda visiwa vya Trinidad na Tobago (Caribbean) ambako atahudhuria kongamano la vijana katika mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Madola mwezi Novemba 2009.

Walengwa wa shindano hili ni vijana wenye umri kati ya miaka 16 hadi 24 na kwamba washiriki wanapaswa kuandika mchanganuo wa aina ya biashara ambao utafafanua jinsi watakavyoiendesha kwa bajeti ya fedha ambazo zitatolewa kama zawadi ya kwanza.

Hakika shindano hili tangu kuanzishwa kwake miaka kadhaa limekuwa likivutia wasikilizaji wetu wengi, na hata katika fainali wageni wa heshima wamekuwa wakiipongeza BBC kwa shughuli pevu kama hiyo. Baadhi wamekuwa wakiomba shindano kama hili lirudiwe, na sisi bila hiana, tumefanya hivyo.

Kwa mashabiki wa Facebook sasa wanaweza kufuatilia mambo ya Faidika na BBC 2009. Jiunge nasi usikie wenzako wanasema nini.

Kimsingi, shindano la Faidika na BBC 2009 kama ilivyokuwa mwaka uliopita limekuwa na awamu mbili:

Awamu ya kwanza:

Kila nchi inakuwa na shindano lake, ambapo anapatikana mshindi mmoja katika nchi husika.

Awamu ya pili:

Hii ndiyo fainali yenyewe. Washindi kutoka kila nchi husika, watapambana katika fainali hii ambayo mwaka huu wa 2009 itafanyika tarehe 13 Agosti 2009 huko Mombasa katika pwani ya Kenya.

Nchi sita za Afrika Mashariki na Kati zinahusika katika shindano hili, nazo ni: Uganda, Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Fainali itatangazwa moja kwa moja katika matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, kupitia kipindi chake maarufu - Dira ya Dunia, na pia kwenye mtandao bbcswahili.com.

Fainali ya mwaka huu ilifanyika Mombasa, Kenya.

Historia

Faidika na BBC ilianzishwa mwaka 2007 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC. Tuliandaa shindano la kwanza kutafuta kijana mwenye kipaji cha biashara, katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. Mafanikio yalikuwa makubwa sana.

Tuliweza kupata mapendekezo mengi, na baada ya uchambuzi yakinifu tukapata washindani watatu, ambapo baada ya mchuano wa mwisho, tuliweza kupata mshindi mmoja ambaye aliondoka na kitita cha dola elfu mbili za kimarekani, na kompyuta.

Baada ya hapo kila mwaka vijana wamekuwa wakishindania fursa hiyo muhimu.