Faidika na BBC 2010

Mwaka 2010, kama ilivyokuwa miaka mitatu iliyotangulia, BBC Idhaa ya Kiswahili itaendesha shindano la kutafuta kijana mjasiriamali kutoka Afrika Mashariki na Kati.

Vijana wajiandae mapema kuandika mchanganuo ya biashara kufuatana na kanuni ambazo zimeainishwa kwenye tovuti hii. Biashara zenye ubunifu na mawazo ya kipekee ndio zitakuwa na nafasi kubwa ya kupata mafanikio.

Kila mwaka, kuanzia mwaka 2007, BBC Idhaa ya Kiswahili imekuwa ikiendesha shindano kwa vijana waishio Afrika mashariki na kati. Shindano hili lilianza mwaka 2007 kuadhimisha miaka 50 ya matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC. Fainali ya kwanza ilifanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania na mshindi wa kwanza wa shindano hilo alikuwa David Ssegawa.

Mgeni rasmi katika sherehe za fainali hizo alikuwa rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete. Rais Kikwete alivutiwa sana na wazo hilo kiasi kwamba alipendekeza shindano hili lifanyike kila mwaka. Kuanzia hapo washindi wengine wawili wamepatikana. Mshindi wa mwaka 2008 alikuwa Ashura Kisesa kutoka Burundi na mshindi wa mwaka 2009 alikuwa Jane Mweni kutoka Kenya. Mwaka 2010 utakuwa wa kuvutia zaidi.

Tarehe ya kuanza kutuma michanganuo itatangazwa kupitia tovuti hii pamoja na katika BBC Idhaa ya Kiswahili.