Haki za Wafanyikazi

Kupata kazi huwa ni jambo la kufurahisha sana kwa mtu yeyote. Wakati huo mtu huwa na raha isiyo kifani kwa vile ulikuwa ukitafuta kazi kwa muda mrefu.

Lakini si ajabu kumsikia mtu analalama miezi michache baada ya kuanza kuifanya kazi ambayo awali alifurahia sana kupata, swali ni nini huenda mrama?

Tatizo mara nyingi huwa hali au mazingira ya kufanya kazi kando na mshahara anaolipwa.

Haya yote yanakuelekeza kwa jambo ambalo ni muhimu sana kwako kama anayefanya ama anatafuta kazi, jambo hili ni haki zako kama mfanyikazi.

Je unafahamu kuwa kuna sheria zilizoweka kwa minajili ya kukulinda wewe kama mfanyikazi?

kulingana na kifungu cha 23 la Tamko la kimataifa kuhusu haki za binadamu ambalo lilitolewa mwaka wa 1948 na Umoja wa Mataifa (UN) ambao umetiwa sahihi na kuridhiwa na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa ; Kila mtu ana haki ya kufanya kazi, kuchagua kazi aipendayo, kuchagua kazi yenye masharti mazuri na ana haki ya kulindwa asikose kazi.

Mstari wa pili wa kifungu hicho unasema Kila mtu ana haki ya kupata mshahara sawa na wengine wenye kazi ya namna moja bila ubaguzi. Na mstari wa tatu wa kifungu hicho hicho unaashiria kuwa kila mfanya kazi anayo haki ya kupata mshahara wa kufaa na unaopendeza utakaomwezesha yeye mwenyewe pamoja na jamii yake kuishi katika hali bora, na mstari wa nne unasema ; Kila mtu anayo haki ya kuunda au kujiunga na chama chochote cha wafanya kazi kwa ajili ya kulinda haki zake za kazi.

Kifungu cha 24 kina kamilisha msururu wa haki za msingi za kikazi kwa kusema ; Kila mtu ana haki ya kupumzika na kufanya kazi kwa kiasi cha saa zinazostahili. Pia ana haki ya kupata likizo, kwa vipindi, na kupokea mshahara kama vile angekuwa kazini.

Ni jambo la kusikitisha sana kuwa hata baada ya mataifa kutia sahihi Tamko la kimataifa kuhusu haki za binadamu pamoja na mikataba na itikadi zingine za kulinda haki za wafanya kazi, matukio ya ukiukaji wa haki hizo vinaendelea zaidi bara Asia na Afrika, hasa katika sekta zisizo rasmi.

Utakuta wafanyi kazi wengi wanalipwa pesa duni, hawapati muda ufaao wa kupumzika, ama kunyimwa likizo ya uzazi maarufu kama maternity leave, isitoshe matukio ya ukosefu wa mavazi ya kujikinga kutokana na athari za kazi hasa wale wanofanya kazi kama vile ukulima, uchimbaji madini, ujenzi na kadhalika.

Waajibu wako kama muajirwa ni kuhakisha kampuni, shirika ama mtu binafsi aliyekuajiri anafuata sheria zilizoko kabla ya kukubali kuifanya kazi hiyo.

Inafaa pia kujisajili katika chama cha wafanyikazi ili chama hicho kiweze sio tu kutetea haki zako za kazi, bali pia kilete uwiano kati yako na muajiri wako endapo mtazozana kazini.

Vile vile ni vyema kung’amua sheria zinazohusiana na kazi zinasemaje pale ulipo.

Ken Owino