Ukweli wa Mambo

Kipindi cha Kimasomaso kilianzishwa kwa lengo la kujadili maswala yanayowahusu vijana kama vile afya ya uzazi na mengineyo kwa ujumla.

Kimasomaso kimekuwa maarufu miongoni mwa wasikilizaji wetu kutokana na ukweli kwamba kimekuwa kikijadili mambo yanayowagusa katika maisha ya kila siku.

Katika kila makala ya Kimasomaso tumewaalika vijana maarufu katika nyanja zote, hasa hasa wasanii maarufu kote katika Afrika mashariki na kati. Tumewahoji wasanii kama vile AY, MwanaFA, Ray C, TID, Bushoke, KLynn, Nakaaya kutoka Tanzania, Nameless, Wahu, Kleptomaniax, Amani, Nyota Ndogo kutoka Kenya, Maurice Kirya, Bebe Cool, Ambassada kutoka Uganda, Serge Nkurunziza na Kidum kutoka Burundi na wengine wengi. Kando na kutoa burudani wasanii hawa wamemulikia maisha wanayoishi na kutoa maoni yao kuhusu afya ya uzazi.

Kimasomaso, ukweli wa mambo, ukweli halisi, ukweli usio na kificho ni kipindi kinachowahusu hasa vijana wa rika mbalimbali. Matarajio ni kuwa jamii nzima itaweza kujifunza mengi kutoka kwenye makala haya.

Makala ambayo yanayakabili maswala yanayowahusu vijana kwa uwazi sana labda kuliko ilivyo wahi kutokea huko nyuma.

Vijana wenyewe wanazungumza kuhusu ni kwa nini wanatumia madawa ya kulevya, kwa nini wanakuwa makahaba , kwa nini wanapata mimba wakiwa wadogo, kwa nini wanakabiliwa vibaya na ugonjwa wa ukimwi, kwa nini iwe hivi na vile.

Lakini baada ya yote, matarajio makubwa ni kwamba tupate funzo litakaloisaidia jamii kukabiliana na matatizo haya.