Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Muhtasari

 1. Rais Kenyatta alitangazwa mshindi wa urais Ijumaa usiku baada ya kupata kura 8, 203, 290 sawa na asilimia 54.2 zilizopigwa
 2. Mgombea wa upinzani Raila Odinga alipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.7
 3. Baada ya matangazo, visa vya maandamano viliripotiwa katika baadhi ya maeneo ambayo ni ngome ya upinzani, mfano Kisumu, Homa Bay na Migori magharibi mwa nchi hiyo
 4. Kulitokea pia visa vya maandamano na polisi kufyatua gesi ya kutoza machozi katika baadhi ya mitaa jijini Nairobi

Habari za moja kwa moja

time_stated_uk

Yasemavyo magazeti leo nchini Kenya

Hivi ndivyo vichwa vya habari katika magazeti ya leo nchini Kenya:

Taifa
BBC
Standard
BBC
Nation
BBC

Matiang'i hakuna watu wameuawa na polisi

Kaimu waziri wa usalama Kenya Dkt Fred Matiang'i amesema hakuna waandamanaji ambao wameuawa na maafisa wa polisi.

Amesema baadhi ya waliokabiliwa na polisi ni wahalifu na waporaji.

"Polisi hawajatumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji popote nchini Kenya. Anayesema hivyo ni muongo," amesema Dkt Matiang'i.

"iwapo ni waandamanaji wanaofanya hivyo kwa amani, wanalindwa. Lakini kama ni wahalifu, wanaopora, hawajalindwa na sheria."

Habari za hivi pundeWanahabari waliokamatwa na polisi waachiliwa huru

Wanahabari wawili wa runinga ya kibinafsi ya KTN waliokuwa wamekamatwa na polisi mtaa wa Kibera, Nairobi wameachiliwa huru, kituo hicho cha habari kimetangaza.

Duncan Khaemba na David Otieno walikuwa wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani.

Matiang'i: Kenya iko salama

Waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i amesema maeneo mengi ya Kenya ni salama baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa jana isipokuwa maeneo machache.

Amesema kumetokea visa vya uvunjifu wa amani mfano Mathare na Kibera, Nairobi na maeneo ya Kisumu.

Maeneo mengine ya Kenya ni salama na Wakenya wanaendelea na shughuli zao za kawaida.

"Ingawa tuna haki ya kuandamana, hii sharti itumiwe kwa amani na bila silaha. Bila kutishia maisha ya watu na mali," amesema.

"Serikali itafanya kila iwezao kulinda uhai na mali ya watu. Wanaoenda kinyume na haya watakabiliwa kikamilifu na nguvu za kisheria."

Dkt Matiang'i amesema moja ya yanayochangia vurugu ni uchochezi unaoenezwa kupitia mitandao ya kijamii.

Amesema kuna sheria na wanaoeneza chuki na taarifa za uongo watatafutwa na kukamatwa.

Waziri huyo amesema wanaotaka kuandamana watalindwa na maafisa wa usalama wakifuata utaratibu uliowekwa kisheria. Hata hivyo, amesema polisi watakabiliana vilivyo na waporaji.

Kamishna athibitisha mtu mmoja amefariki Nyanza

Kamishna anayesimamia uliokuwa mkoa wa Nyanza, magharibi mwa Kenya amethibitisha kwamba mtu mmoja aliuawa wakati wa vurugu zilizozuka baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais Ijumaa.

Mtu huyo aliuawa katika mtaa wa Maseno.

Kamishna huyo Wilson Njenya amewaambia wanahabari mjini Kisumu kwamba watu watatu pia wamekamatwa.

Amesema walikamatwa wakipora na kuharibu mali.

Bw Njenga amepuuzilia mbali taarifa kwamba polisi wanatumia risasi halisi kukabiliana na waandamanaji na pia akasema hakuna agizo la kuwapiga risasi waandamanaji.

Amesema polisi wanatumia vitoa machozi na njia nyingine kukabiliana na waandamanaji.

"Risasi halisi hutumiwa kama njia ya mwisho ya kujikinga. Hatutaki kuwapoteza maafisa wa usalama pia tukilinda maisha na mali," amesema.

Bw Njenga amesema maeneo mengine kama vile Bondo na Homa Bay yameathiriwa pia. Mjini Homa Bay amesema waandamanaji wamekuwa wakifunga barabara na wamekuwa wakirejea kila polisi wanapoondoka baada ya kuondoa vizuizi.

Eneo la Bondo, Siaya amesema waandamanaji walijaribu kuchoma moto vituo viwili vya mafuta lakini wakazuiwa na polisi.

Mtaa wa Kisumu Magharibi, waandamanaji waliteketeza basi.

Mwanahabari wa KTN akamatwa Kibera

Mwanahabari wa kituo cha runinga cha kibinafsi cha KTN amekamatwa na maafisa wa polisi akiripoti matukio yanayojiri katika mktaa wa Kibera, Nairobi.

Maaskofu wa kanisa Katoliki wawaomba polisi kutotumia nguvu kupita kiasi

Maaskofu wa kanisa Katoliki wametoa wito kwa Rais Kenyatta na serikali yake kufanya juhudi haraka kuunganisha tena Kenya baada ya uchaguzi.

Wamesema wanatumai hakuna jamii itakayotengwa kutokana na msimamo wake wa kisiasa.

Wamewaomba wanasiasa kuhubiri amani na maridhiano.

Wamewaomba maafisa wa usalama kutotumia nguvu kiasi na kuheshimu maisha ya binadamu wakidhibiti makundi ya watu wanaoandamana.

"Tumepokea visa vya kusikitisha vya watu kuuawa katika maeneo mbalimbali nchini. Hakuna mtu anayefaa kufariki kwa sababu ya uchaguzi," wamesema kupitia taarifa.

Maaskofu hao wamewashauri wagombea ambao hawajaridhishwa na matokeo kutumia njia za kisheria kutafuta haki.

Watu wawili wauawa katika makabiliano Kisumu

Watu wawili wamefariki na wengine watano wanauguza majeraha ya risasi hospitalini mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya baada ya makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wakipinga matokeo ya urais yaliyotangazwa Ijumaa usiku.

Maeneo mengi ya mji huo hayana watu na biashara zimefungwa. Maafisa wa usalama wanaendelea kushika doria.

Makundi ya vijana wameweka vizuizi katika barabara ya kutoka Kisumu kwenda Nairobi.

Polisi wanajaribu kuwatawanya vijana hao na kuondoa vizuizi.

s

Kisumu
BBC
Waandamanaji wamekuwa wakifunga barabara katika baadhi ya maeneo
Kisumu
BBC
Baadhi ya maeneo hakuna wapi na maduka yamefungwa
Kisumu
BBC
Polisi walikabiliana na wafuasi wa upinzani usiku

Magufuli ampongeza Kenyatta kwa ushindi Kenya

Rais wa Tanzania John Magufuli amempongeza Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne.

Bw Kenyatta alitangazwa mshindi Jumanne.

Amemtakia Kenyatta: "Mafanikio mema".

Marais Paul Kagame (Rwanda) na Yoweri Museveni (Uganda) pia wamempongeza Rais Kenyatta.

View more on twitter

Hali ya utulivu yarejea Garissa

Hali ya kawaida imeanza kurejea mjini Garissa siku moja baada ya matokeo ya uchaguzi wa urais kutangazwa.

Sehemu ya soko kuu mjini humo iliteketezwa Jumatano wakati wa ghasia kati ya wafuasi wa wagombea wawili wa ugavana. Lakini jana na leo hali imekuwa tulivu.

Mwandishi wetu Bashkas Jugsodaay amepiga picha hizi za wananchi wakiendelea na shughuli zao za kawaida leo asubuhi.

Rukwama
BBC
Kununua mboga
BBC
Magari
BBC

Wafuasi wa upinzani waandamana kupinga matokeo ya urais Kenya

Polisi Kondele
Getty Images
Polisi wakipiga doria katika mtaa wa Kondele, Kisumu baada ya matokeo kutangaza Ijumaa usiku

Maafisa wa polisi nchini Kenya walikabiliana na waandamanaji waliojitokeza barabarani muda mfupi baada ya Rais Kenyatta kutangazwa mshindi wa urais.

Hali Jumamosi asubuhi hata hivyo imekuwa tulivu katika miji mingi.

Maeneo yaliyoathiriwa na makabiliano kati ya polisi na waandamanaji Ijumaa jioni ni Kisumu magharibi mwa Kenya pamoja na baadhi ya mitaa jijini Nairobi.

Katika mtaa wa mabanda wa Kibera, kelele zilisheheni hewani baada ya matangazp kutolewa.

Katika maeneo ya Siaya, Kisumu na Migori wafuasi wa upinzani waliandamana kupinga matokeo.

Mjini Kisumu, ngome ya mgombea wa upinzani Raila Odinga, polisi walitumia helikopta kushika doria kutoka angani Ijumaa jioni.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, katika mitaa ya Buruburu na maeneo ya Kiambu, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya makundi mawili. Kundi moja lilikuwa linasherehekea ushindi na jingine likipinga matokeo hayo.

Matokeo ya urais ya wagombea wote wanane

Kulikuwa na wagombea wanane katika kinyang'anyiro cha urais nchini Kenya. Matokeo kamili yalikuwa kama ifuatavyo:

 • Ekuru Aukot 27,311 (0.18)
 • Abduba Dida 38,093 (0.25)
 • Cyrus Jirongo 11,705 (0.08)
 • Japheth Kaluyu 16,482 (0.11)
 • Uhuru Kenyatta 8,203,290 (54.27)
 • Michael Wainaina 13,257 (0.09)
 • Joseph Nyagah 42,259 (0.28)
 • Raila Odinga 6,762,224 (44.74)

Ushindi mkubwa kwa Rais Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.2 na pia akapata angalau asilimia 25 ya kura katika kaunti 35.

Mshindi wa urais huhitajika kupata asilimia 50 ya kura na kura moja zaidi, pamoja na angalau asilimia 25 katika kaunti 24.

Baada ya kutangazwa mshindi, alitoa wito kwa mpinzani wake Raila Odinga, ambaye muungano wake uliyakataa matokeo, aungane naye kufanya kazi kwa maslahi ya taifa.

""Sana kwa Raila Odinga, namuomba yeye, wafuasi wake, wote waliochaguliwa kupitia upinzani, tutafanya kazi pamoja, tutashirikiana, tutakua pamoja na kuendeleza nchi pamoja," alisema.

Kenyatta
Uhuru Kenyatta/Twitter
Kenyatta na mkewe Margaret na William Ruto na mkewe Rachel
Uhuru Kenyatta/Twitter
Kenyatta na mkewe Margaret na William Ruto na mkewe Rachel
Kenyatta na Ruto
Uhuru Kenyatta/Twitter
Kenyatta alichapisha mtandaoni picha hii inayomuonesha yeye na Naibu Rais Ruto wakifuatilia tangazo kutoka kwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC Wafula Chebukati

Hujambo!

Karibu kwa taarifa za moja kwa moja kuhusu uchaguzi mkuu Kenya. Ni siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Jumanne nchini Kenya, matokeo ambayo yalipingwa na muungano wa upinzani National Super Alliance.