Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Muhtasari

 1. Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika maeneo ya kaskazini mwa mji mkuu Harare mapema leo.
 2. Jeshi la Zimbabwe lilisoma taarifa kwenye kituo cha runinga cha serikali ZBC, likisema kuwa linachukua hatua ya kuwalenga wahalifu.
 3. Meja Jenerali Sibusiso Moyo amesema Rais Robert Mugabe na familia yake "wako salama salimini."
 4. Taarifa zinasema kiongozi wa kundi la vijana wa Zanu-PF linalomuunga mkono Bw Mugabe amekamatwa

Habari za moja kwa moja

time_stated_uk

 1. Mkuu wa AU asema yanayojiri Zimbabwe ni 'kama mapinduzi'

  Alpha Conde, ambaye ni rais wa Guinea amesema kilichotokea Zimbabwe bila shaka ni "wanajeshi kujaribu kuchukua mamlaka kwa nguvu".

  Mkuu huyo wa Umoja wa Afrika (AU) ametoa wito kwa jeshi kukomesha wanalofanya - jambo ambalo amesema "linaonekana kama mapinduzi ya serikali", kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

  Hilo linakinzana na msimamo wa jeshi la Zimbabwe ambalo limesisitiza kwamba halijatekeleza mapinduzi ya kijeshi, bali linajaribu kuwaondoa "wahalifu" wanaomzingira Rais Mugabe.

  Conde amekuwa mwenyekiti wa AU tangu Januari
  Image caption: Conde amekuwa mwenyekiti wa AU tangu Januari
 2. China inafuatilia kwa karibu matukio Zimbabwe

  Xi Jinping alizuru Harare na kukutana na Robert Mugabe mwaka 2015
  Image caption: Xi Jinping alizuru Harare na kukutana na Robert Mugabe mwaka 2015

  China ambayo ni mshirika mkuu zaidi wa kibiashara wa Zimbabwe, na imekuwa ikiisaidia na kufanya biashara na nchi hiyo licha ya vikwazo vya kiuchumi vya nchi za magharibi.

  Wiki jana tu, Jenerali Constantino Chiwenga - aliyetangaza kwamba jeshi lingeingilia kati kusitisha kufukuzwa kwa watu waliopigania uhuru kutoka chama cha Zanu-PF - alizuru beijing kwa kile ambacho China leo imesema ulikuwa "mkutano wa kawaida wa kubadilishana mawazo kijeshi".

  Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Geng Shuang amesema:

  Quote Message: Kama nchi ambayo ni rafiki wa Zimbabwe, tunafuatilia kwa karibu sana matukio na hali nchini Zimbabwe.
  Quote Message: Kudumisha amani na ustawi thabiti ni vitu vinavyoendana na maslahi ya Zimbabwe na mataifa ya kanda na ni nia ya pamoja ya jamii ya kimataifa.
  Quote Message: Tunatumai kwamba wahusika Zimbabwe watashughulikia ipasavyo masuala hayo ya ndani.
 3. EU yataka amani idumishwe Zimbabwe

  Umoja wa Ulaya (EU) umeomba kuwe na "suluhu ya amani" kwa mzozo wa sasa nchini Zimbabwe baada ya jeshi kusema limechukua udhibiti wa nchi hiyo.

  Msemaji wa EU amesema:

  Quote Message: Matukio ya hivi karibuni kisiasa nchini Zimbabwe, na matokeo yake, ikiwa ni pamoja na hatua ya majeshi ya nchi hiyo, ni mambo yanayozua wasiwasi.
  Quote Message: Tunatoa wito kwa wahusika wote kujiepusha na makabiliano na badala yake kuhusika katika mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa njia ya amani."
 4. Polisi 'wadhibitiwa' na jeshi Harare

  Fadzayi Mahere

  Mwanasheria mmoja katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare amepakia kwenye Twitter picha inayoonyesha kundi la maafisa wa polisi wakiwa wameketi kwenye foleni, huku wakiwa chini ya uangalizi wa maafisa wa jeshi.

  Fadzayi Mahere, ambaye anapania kuwa mbunge wa Mount Pleasant, Harare, anasema alipiga picha hiyo kupitia dirisha la afisi yake.

  Haijabainika nini kilikuwa ninatokea kwenye picha hiyo.

 5. Grace Mugabe anaweza kuwa ametorokea Namibia?

  Grace Mugabe

  Mbunge wa upinzani nchini Zimbabwe Eddie Cross ameambia BBC kwamba anaamini mke wa Rais Mugabe, Grace, ametorokea Namibia.

  Mwanasiasa huyo wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) amesema anafahamu kwamba Grace aliruhusiwa kuondoka nchini humo usiku wa kuamkia leo na jeshi.

  Ameongeza kwamba alikuwa hana kwingi kwa kwenda kutafuta hifadhi baada yake kudaiwa kumdhalilisha mwanamitindo Afrika Kusini jambo lililomaanisha kwamba hawezi kuwa salama huko.

  Hata hivyo, taarifa hizi hazijathibitishwa na jeshi.

  Nick Mangwana, mwakilishi wa chama tawala cha Zanu-PF nchini Uingereza ameambia BBC kwamba mwenyewe pia amepokea taarifa kwamba Grace hayupo tena nchini Zimbabwe.

  Lakini Bw Mangwana amesema katika siasa za Zanu-PF, Bi Mugabe ni mtu wa chini sana na hana usemi wowote.

  Amesema ana mamlaka tu kwa sababu ya kuwa ni mke wa Rais Mugabe.

  "Alichukua wadhifa wa juu kuliko ule anaostahiki kuwa nao,” amesema.

  Soma zaidi: Grace Mugabe anaweza kuwa ametorokea Namibia?

 6. Zuma: Nimewasiliana na Mugabe na yuko salama

  Mugabe
  Image caption: Mugabe na Zuma awali

  Rais Robert Mugabe "yuko salama", rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema.

  Bw Zuma amesema amezungumza na kiongozi huyo wa miaka 93 kwa njia ya simu.

  Amesema Mugabe amemjulisha kwamba yupo nyumbani kwake ambapo amezuiwa kuondoka, kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa afisi ya rais wa Afrika Kusini.

  Zuma amesema kwamba amewasiliana pia na Majeshi ya Ulinzi ya Zimbabwe (ZDF), taarifa hiyo imesema.

  Afrika Kusini inapanga kuwasiliana na pande zote mbili.

  Bw Zuma amekariri wito wake wa awali kwamba kuwe na "utulivu"

 7. Grace Mugabe ni nani?

  Anaaminiwa kuzuiliwa akiwa na mume wake, nyumbani kwao kwenye mji mkuu Harare.

  Lakini Grace Mugabe ni nani na mbona kuinuka kwake kunakumbwa na utata?

  • Alianza uhusiano na Robert Mugabe, ambaye ni mkubwa kwake kwa miaka 41,akifanya kazi kama mpiga chapa katika ikulu.
  • Bw. Mugabe baadaye akasema kuwa mke wake wa kwanza Sally, ambaye alikuwa mgonjwa wakati huo alifahamu na kuidhinisha uhusiano huo.
  • Aliolewa na Mugabe, mume wake wa pili mwaka 1996 kwenye sherehe kubwa. Wana watoto watatu.
  • Alipewa jina (Gucci Grace) na wakosoaji wake kwa matumizi yake ya pesa nyingi kwa anasa.
  • Yeye na mume wake wakewekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya na Marekani vikwemo vya usafiri.
  • Kwa njia ya utata alipata shahada ya PhD mwezi Sepetemba mwaka 2014 baada ya miezi miwili tu.
  • Aliteuliwa mkuu wa kitengo cha wanawake cha Zanu-PF mwaka 2014. Aliliumiwa na mwanamitindo wa Afrika Kusini kwa kumpiga Agosti mwaka 2017.
  Grace Mugabe
  Image caption: Grace Mugabe
 8. Gazeti la serikali nchini Zimbabwe limeandika taarifa za kwanza

  Gazeti la serikali nchini Zimbabwe, The Herald, hatimaye limechapisha taarifa kuhusu yale ambayo yamekuwa yakiendelea katika kipindi cha saa chache zilizopita.

  Taarifa yake kuu kwa sasa ni kuhusu hatua zilizochukuliwa na jeshi.

  Herald Newspaper
  Image caption: Herald Newspaper
 9. Zuma: Ninafuatilia kwa karibu kinachoendelea Zimbabwe

  Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anasema atafuatilia kwa karibu yale yanayoendelea katika taifa jirani la Zimbabwe.

  Taarifa rasmi iliyotolewa na ofisi ya Bw. Zuma ililitaka jeshi kusuluhisha mzozo uliopo kwa njia ya amani.

  Mwezi Agosti Afrika Kusini ilijipata kwenye mzozo wa familia ya Mugabe, wakati Grace Mugabe alidaiwa kumpiga mwamamitindo kwenye hoteli mjini Johannesbug

  BI Mugabe hakushtakiwa baada ya serikali ya Bw. Zuma kumpa kinga.

  Jacob Zuma
  Image caption: Jacob Zuma
 10. Vituo vya serikali vimekuwa vikicheza nyimbo za vita vya uhuru Zimbabwe

  Vyombo vya habari vya serikali vimekuwa vikicheza nyimbo za uhuru za kuanzia wakati wa uhuru miaka ya themanini na kurudia matangazo ya Meja Jenerali Sibusiso Moyo.

  Jenerali Moyo alitangaza kupitia kituo cha runinga cha serikali nchini Zimbabwe (ZBC) TV kuwa jeshi lilikuwa limetwaa madaraka na kuwa Rais Robert Mugabe alikuwa salama.

  Pia kituo cha radio cha serikali nacho kilitanga taarifa hiyo ya Jenerali Moyo.

  Vituo hivyo havijatanga matangazo mengine.

  Nyingi ya nyimbo hizo ni kuhusu vita vilivyoendeshwa na wapiganaji wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa wazungu.

 11. Kiongozi wa vijana wa Zanu PF akamatwa Zimbabwe

  Kudzai Chipanga, kiongozi wa vijana katika chama cha Zanu-PF, amekamatwa mjini Harare, siku moja baada ya kusema kuwa wafuasi wake walikuwa tayari kufa wakimpigania Rais Robert Mugabe.

  Kitengi hicho cha vijana kinamuunga mkono mke wa Mugabe Grace kama mrithi Mugabe.

  Bw. Chipanga alimpinga hadhararani Jenerali Constantino Chiwenga , baada ya mkuu huyo wa Majeshi kusema Jumatatu kuwa alikuwa amejiandaa kuchukua hatua kumaliza hisia za kutengwa katika chama cha Zanu PF.

  Kisha kiongozi huyo wa vijana akajibu jana na kusema kuwa Jenerali Chiwenga hakuwa na uungwaji mkono wa jeshi lote

  Kudzai Chipanga
  Image caption: Kudzai Chipanga
 12. Gazeti la serikali nchini Zimbabwe halijaandika chochote

  Gazeti na serikali nchini Zimbabwe la - The Herald - halijaandika chochote kuonyesha yakle ambayo yamekuwa yakiendelea usiku kucha.

  Bado mtandao huo una taarifa zinazoonekana kumuunga mkono Rais Robert Mugabe.

  Taarifa yake kuu inamnukuu kiongozi wa wa vijama katika chama cha Zanu-PF Kudzai Chipanga akimunga mkon Rais Mugabe, alisema tunampigania Rais kwa masha yetu."

  Gazeti la serikali nchini Zimbabwe halijaandika chochote
  Image caption: Gazeti la serikali nchini Zimbabwe halijaandika chochote
 13. Magari ya kijeshi katika mitaa ya Harare

  Magari ya kijeshi yanaonekana yakipiga doria katika barabara za mji mkuu wa Zimbabwe Harare.

  Picha zilizochukuliwa mapema leo zinaonyesha magari ya kijeshi na wanajeshi, wakionekana kuelekeza au kuzuia magari.

  Magari ya kijeshi katika mitaa ya Harare
  Image caption: Magari ya kijeshi katika mitaa ya Harare
  Magari ya kijeshi katika mitaa ya Harare
  Image caption: Magari ya kijeshi katika mitaa ya Harare
 14. Emmerson Mnangagwa ni nani?

  Akaunti ya chama cha Zanu PF inasemama kuwa Emmerson Mnangagwa amefanywa kuwa rais wa mpito.

  Mnangawa mwenye umri wa miaka 75 alifutwa kama makamuu wa rais kutokana na kile serikali ilisema kuwa kutokuwa mtiifu.

  Kufutwa kwake kulionekana kama nia ya kumwezesha mke wa Rais Mugabe, Grace, kufuata nyayo za mumewe na kuwa kiongozi wa Zimbabwe.

  Awali alikuwa ametoa wito kwa mumewe kumfuta makamu wa rais.

  Bw. Mnangagwa ambaye ni mku wa zamani wa ujasusi amekuwa mtu ambaye alitarajiwa kumrithi Rais Mugabe 93.

  Kufutwa kwake kulimaanisha kuwa Grace Mugabe anatarajiwa kuteuliwa kuwa makamu wa rais wakati wa mkutano maalum wa chama tawala cha Zanu-PF mwezi ujao.

  Emmerson Mnangagwa
  Image caption: Emmerson Mnangagwa
 15. Mugabe anajiandaa kuondoka madarakani

  Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anajiandaa kuondoka madarakani saa chache baada ya jeshi la Zimbabwe kutwaa madaraka, kwa mujibu wa mtandao maarufu wa habari nchini Afrika Kusini.

  "Mugabe anajiandaa kuondoka madarakani," mtandao wa wa News24 uliandika bila ya kutoa taarifa zaidi.

  Misukusuko ya kisiasa imekuwa ikiongezeka tangu Mugabe hivi majuzi amfute Emmerson Mnangagwa, mshirika wake wa miaka mingi kama makamu wa Rais.

 16. Mzozo wa Zimbabwe: Kile tunachokifahamu hadi sasa

  Jeshi la Zimbabwe lilisoma taarifa kwenye kituo cha runinga cha serikali ZBC, likisema kuwa linachukua hatua ya kuwalenga wahalifu.

  Hata hivyo limesema kuwa hayo sio mapinduzi ya kijeshi na Rais Mugabe yuko salama.

  Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika maeneo ya kaskazini mwa mji mkuu Harare mapema leo.

  Taarifa hiyo ya jeshi ilikuja saa kadhaa baada ya jeshi kudhibiti kituo cha ZBC.

  Mwanamume mmoja ambaye alikuwa amevaa sare za jeshi alisema kuwa jeshi linataka kukabiliana na watu ambao wanatenda uhalifu unaoleta madhara ya kijamii na kiuchumi nchini Zimbabwe.

  "Wakati tutakapomalzia wajibu wetu, tunatarajia kuwa hali itadudi kuwa sawa."

  Taarifa hiyo ilisema kuwa Mugabe 93, na familia yake wako salama.

  Haijulikani ni nani anaongoza hatua hiyo ya kijeshi.

  Magari ya wanajeshi waliojihami kwa silaha yanaonekana maeneo ya mjini Harare.

  Hali hiyo ya wasi wasi wa lolote kuweza kutokea, imeanza hapo jana jioni, ambapo wanajeshi wakiwa na silaha walionekana wakijipanga katika maeneo kadhaa pamoja na kuzingira ofisi za shirika la utangazaji la Zimbabwe ZBC.