Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma

time_stated_uk

 1. Na hapo ndio tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja kwa hii leo. Asante kwa kusoma taarifa zetu.

 2. Mke wa waziri mkuu nchini Israel akiuka kanuni za corona

  Sara Netanyahu
  Image caption: Sara Netanyahu amejitetea akisema, alidhani anaruhusiwa kutengenezwa nywele kwasababu ya kushiriki kwenye utengenezaji wa filamu ya kuhamasisha umma.

  Ripoti zinadai kwamba mke wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Sara, amevunja kanuni zilizowekwa za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 ili atengenezwe nywele.

  Kulingana na gazeti la Yedioth Ahronoth, msusi alikwenda kwenye makazi rasmi ya waziri mkuu wiki iliyopita.

  Hata hivyo, kanuni zilizowekwa mwezi uliopita baada ya kuongezeka kwa idadi ya maambukizi ikiwemo kutoruhusiwa kutembea zaidi ya kilomita 1 kutoka eneo lako la nyumbani isipokuwa tu kwa mahitaji maalum.

  Hayo hayajumuishi mahitaji ya urembo kwa mtu ambaye hana majukumu rasmi kama mke wa Netanyahu.

  Kutembelea makazi ya mwingine pia hakuruhusiwi.

  Vyanzo vinasema Bi. Netanyahau alijitetea akisema alifikiria kwamba anaruhusiwa kutengenezwa nywele kwasababu alikuwa anashiriki utengenezaji wa filamu ya kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kuvaa barakoa.

  Aidha, waliongeza kwamba yeye na msusi wake walivaa barakoa na glavu wakati anatengenezwa nywele na pia alimuomba msusi wake kuepuka kuzungumza.

  Bi. Netanyahau, ndio wa hivi karibuni miongoni mwa watu wa ngazi ya juu kuvunja kanuni za kukabiliana na virusi vya corona.

 3. Janga laathiri ukuaji uchumi wa mwongo mmoja Afrika

  Ukuaji wa uchumi huenda ukaimarika mwaka ujao
  Image caption: Ukuaji wa uchumi huenda ukaimarika mwaka ujao

  Benki ya Dunia imesema janga la virusi vya corona limeathiri ukuaji wa uchumi Afrika na huenda kukasababisha kushuka kwa uchumi kwa asilimia 3.3 mwaka huu wa 2020.

  Hata hivyo, benki hiyo inatabiri kuimarika kwa uchumi huo mwaka ujao.

  Hadi kufikia sasa, Afrika imefanikiwa kukwepa athari kubwa za janga la corona huku idadi ya maambukizi ikiwa chini ikilinganishwa na mabara mengine.

  Lakini hatua ya kutotoka nje ili kukabiliana na janga hilo kumesababisha ukuaji wa kasi ya chini ya uchumi, hususan Afrika Kusini nchi ya pili yenye ukuaji mkubwa wa uchumi.

  Benki wa Dunia imeonya kwamba raia zaidi ya milioni 40 huenda wakatumbukia kwenye lindi la umaskini.

 4. 'Sokwe azaliwa licha ya vipimo vya ujauzito wa mama yake kukutwa hana mimba’

  Sokwe aliyezaliwa katika hifadhi ya Chris Yarwood
  Image caption: Hifadhi ya wanyama ya Chris Yarwood imesema bado haijafahamu jinsia ya sokwe aliyezaliwa

  Sokwe amezaliwa kiajabu katika hifadhi ya wanyama baada ya mama yake kupimwa ujauzito miezi michache iliyopita kabla hajajifungua na kukutwa hana mimba.

  Mhudumu wa hifadhi hiyo ya wanyama Chris Yarwood amesema sokwe huyo amezaliwa baada ya mama yake kufanyiwa vipimo kadhaa na kukutwa hana ujauzito.

  Ameongeza kuwa mtoto huyo wa sokwe alizaliwa mwezi Juni, na alimficha kwa wahudumu tangu alipozaliwa.

  Matokeo yake, wahudumu hawafahamu jinsia ya sokwe huyo mpaka sasa.

  Katika kisiwa cha Asia, sokwe wako hatarini sana kupotea na sasa wamesalia 55,000.

  Mama Leia amekuwa akimficha mtoto wake tangu alipozaliwa mwezi Juni
  Image caption: Mama Leia amekuwa akimficha mtoto wake tangu alipozaliwa mwezi Juni

  Bwana Yarwood amesema kuzaliwa kwa sokwe huyo mpya kumewapa matumaini mapya licha ya kwamba dunia haina uhakika wa uwepo wao, lakini maisha yanaendelea kama kawaida na kuzaliwa kwa sokwe huyo kumetoa mwangaza mpya".

  Mtoto huyo wa sokwe ni wa pili kuzaliwa kutokana na sehemu ya mpango wa njia ya kupandikiza wanyama katika hifadhi.

  Awali hifadhi hiyo ya wanyama ilisema programu za aina hiyo zimekumbana na changamoto ya ufadhili baada ya kutokea kwa ugonjwa wa Covid 19.

 5. Nzi atawala mdahalo wa makamu rais Marekani

  Mike Pence
  Image caption: Nzi aliyetawala mdahalo wa makamu wa rais Marekani

  Ikiwa moja ya vipimo vya mafanikio ni umaarufu kwenye mitandao ya kijamii basi mdahalo wa makamu rais Marekani umechukua kikombe.

  Licha ya wagombea hao kujitahidi kwa kila namna kwenye hoja zao, hakuna walichosema kilichoendana na watu waliokuwa wanawafuatilia mitandaoni kama ilivyokuwa kwa nzi aliyejitokeza ambaye hakukutarajiwa.

  Kwa takriban dakika mbili, nzi alitua kwenye kichwa cha makamu rais Mike Pence na moja kwa moja akawa maarufu.

  Neno ‘nzi’ limesambaa kwenye mtandao wa Twitter zaidi ya mara 700,000 tangu alipojiteokeza wakati mdahalo unaendelea.

  Kampeni ya Joe Biden nayo imetumia vizuri fursa hiyo kwa kusambaza maneno "flywillvote.com".

  Nzi huyo ameunganisha pande zote mbili huku mmoja akimpachika jina la "shujaa wa Marekani" na mwingine akisema "huenda ndio jambo litakalokumbukwa zaidi".

  Aidha, mmoja amelinganisha wakati wa mdahalo wa urais katika uchaguzi uliotanguliwa – miaka minne iliyopita ambapo nzi alijitokeza juu ya kichwa cha mgombea urais Hillary Clinton.

  View more on twitter

  Hilo halimaanishi kwamba nzi huyo ni yule yule aliyejitokeza wakati huo na sasa amerejea tena.

  Lakini sio wote waliomchukulia nzi huyo kwa utani kwasababu mchambuzi mwenye msimamo mkali Ben Shapiro alisema kuwa nzi huyo ni njia moja ya kutatiza kile kilichokuwa kinaendelea wakati wa mdahalo.

 6. Viongozi wa Kenya na Misri wajadiliana juu ya mzozo wa mto Nile

  Rais Abdel Fattah al-Sisi (kulia) na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (kushoto)
  Image caption: Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi (kulia) na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (kushoto)

  Mkutano kati ya rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta umengazia majadiliano yaliokwama ya bwawa la Ethiopia, kulingana na maafisa wa Misri.

  Viongozi hao wawili walikutana katika mji mkuu wa Cairo, Jumapili wakati rais Kenyatta anarejea nyumbani kutoka Ufaransa.

  Taarifa kutoka kwa msemaji wa Misri inasema: “Mkutano huo uligusia maendeleo ya hivi karibu yenye maslahi ya mataifa hayo mawili, hasa yenye kuzingatia bwawa la Ethiopia, kama ilivyokubalika kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili wakati wa kipindi kijacho juu ya suala hili nyeti na muhimu".

  Kenya haikusema lolote kuhusu bwawa hilo zaidi ya kusema kuwa viongozi hao walijadiliana masuala yenye kugusa maslahi ya nchi hizo mbili, miongoni mwao amani ya eneo na usalama, biashara na namna Afrika inavyokabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

  Bwawa la Ethiopia linalojengwa kutoka mto Nile linatarajiwa kutoa nguvu za umeme kwa raia milioni 65 wa Ethiopia.

  Kwa kaisi kikubwa mno, Misri inategemea mto Nile kwa maji ya matumizi yake na hivi karibuni ilionya kwamba ujenzi wa bwawa hilo ni tishio kwa taifa lake.

  Kenya ni mmoja wa waangalizi katika jopo la wapatanishi la Umoja wa Afrika katika utatuzi wa mgogoro unatokana na bwawa hilo.

 7. Mali imemuachilia Waziri Mkuu wa zamani aliyekuwa amekamatwa

  Mali imemuachilia Waziri Mkuu wa zamani aliyekuwa amekamatwa.

  Mamlaka huko Mali imetangaza kuachiliwa huru kwa wanasiasa kadhaa na wanajeshi waliokamatwa wakati wa mapinduzi ya Agosti.

  Walioachiliwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Boubou Cissé.

  Taarifa rasmi imeonesha kwamba waliokamatwa bado watasubiri uamuzi wa mahakama ikiwa kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.

  Jumatatu, serikali ya mpito ilitangaza baraza jipya la mawaziri ambapo wanajeshi waliopanga mapinduzi walikabidhiwa nafasi muhimu serikalini ikiwemo ulinzi, usalama, utawala wa mipaka na maridhiano ya kitaifa.

  Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, imeiondolea Mali vikwazo, na kutambua kile ilichokitaja kama kupigwa kwa hatua muhimu kuelekea kwenye utaratibu wa kikatiba.

  Boubou Cissé
  Image caption: Boubou Cissé ni miongoni mwa walioachiliwa huru
 8. Nani ataingia kwenye fainali ya kuwania uongozi wa (WTO)

  Wanaowania nafasi ya kuongoza WTO
  Image caption: Wanaowania nafasi ya kuongoza WTO

  Wagombea watano wanaowania kuchukua uongozi wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), wanatarajia kufahamu nani anaingia kwenye fainali ya kinyang’anyiro hicho, Alhamisi.

  Kumekuwa na tetesi kwamba huenda wagombea wa Nigeria na Korea Kusini wakaingia kwenye awamu ya fainali.

  Aidha Shirika la WTO halijawahi kuongozwa ama na mwanamke au mwafrika.

  Wagombea wote wamekuwa na majukumu wanayoyatekeleza katika ngazi ya kidunia.

  Aliyekuwa waziri wa fedha wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala aliwahi kuhudumu kama Mkurugenzi mkuu wa Benki ya Dunia ilihali akiwa waziri wa fedha wa Kenya, Amina Mohamed alikuwa mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri wa WTO katika mkutano uliofanyika Nairobi mwaka 2015.

  Aidha, wawili hao wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa waziri wa biashara wa Korea Kusini Yoo Myung-hee, pamoja na Mohammad Maziad Al-Tuwaijri mshauri wa familia ya kifalme wa Saudi Arabia na Liam Fox, aliyekuwa waziri wa Uingereza.

  Matumaini ni kwamba ikiwa mwafrika ndiye atakayechaguliwa kuongoza Shirika la WTO, hilo huenda likaimarisha uchumi, ambao umekwama kwa asilimia 2 hadi 3 kwa muda katika kiwango cha wastani duniani.

  Mgombea atakayeibuka na ushindi anatarajiwa kutangazwa mwezi ujao.

 9. Joshua Cheptegei avunja rekodi ya mita 10,000

  Cheptegei sasa anashikilia rekodi nne za dunia
  Image caption: Cheptegei sasa anashikilia rekodi nne za dunia

  Mwanariadha wa Uganda Joshua Cheptegei alivunja rekodi ya dunia upande wa wanaume katika mbio za mita 10,000 huku mwanariadha wa Ethiopia Letesenbet Giedy akivunja rekodi ya wanawake katika mbio za mita 5000 mjini valencia nchini Uhispania.

  Cheptegei mwenye umri wa miaka 24 aliweka muda wa dakika 26 na sekunde 11 na kuvunja rekodi ya miaka 15 iliowekwa na mwanariadha wa Ethiopia Kenenisa Bekele kwa zaidi ya sekunde sita.

  Gidey alivunja rekodi ya dunia ya miaka 12
  Image caption: Gidey alivunja rekodi ya dunia ya miaka 12

  Gidey mwenye umri wa miaka 22 aliweka muda wa dakika 14 na sekunde 6.62 na kuvunja rekodi iliowekwa na Tirunesh Dibaba 2008.

  Walifikia muda huo katika mbioa za NN Valencia za rekodi za dunia.

  Nafurahia alisema Gidey ambaye alishinda medali ya shaba katika mbio za mita 10,000 kwenye mashindano ya riadha ya dunia mjini Doha Qatar 2019.

  ‘’Hii imekuwa ndoto ya muda mrefu. Ni kitu kikubwa kwangu. Rekodi ya Bekele ya awali ya muda wa dakika 26 na sekunde 17 .53 ilisimama kwa muda mrefu bila kuvunjwa’’.

  Rekodi ya awali ya Bekele ya dakika 26 na sekunde 17.53 ilikuwa ndio ya muda mrefu zaidi kudumu katika historia kwa mbio za mita 10,000 kwa wanaume.

  Mafanikio ya Cheptegei yanaadhimisha rekodi ya nne duniani katika kipindi cha miezi 10, baada ya kuvunja rekodi ya mbio za marathoni ya kilomita 10 Desemba na kilomita 5 mwezi Februari.

  Katika mbio za Monaco Diamond League zilizofanyika Agosti, alivunja rekodi nyingine ya dunia ya Bekele, ya miaka 16 ya mita 5,000 kwa sekunde mbili.