Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Abdalla Seif Dzungu na Lizzy Masinga

time_stated_uk

 1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho alfajiri kwaheri.

 2. Marekani yahofia 'kufungwa' kwa kambi za wakimbizi Kenya

  Marekani imeelezea wasi wasi wake kuhusu uwezekano wa kufungwa kwa kwa kambi za wakimbi za Dadaab na Kakuma nchini Kenya.

  Kupitia Waziri wake wa mambo ya nje Anthony Blinken, utawala wa Rais Joe Biden siku ya Alhamisi uliangazia suala lakufungwa kwa kambi hizo mbili.

  Utawala wa Biden inataka kujua hali ya kuregeshwa kwa wakimbizi katika mataifa yao.

  Hii inafuatia mkutano kati ya katibu wa katika Wizara ya Mamboya Nje wa Kenya Macharia Kamau na Derek Chollet ambaye ni mshauri wa sera wa ngazi ya juu wa Waziri wa Mmbo ya ya nej wa Marekani Anthony Blinken.

  Akijibu swali hilo Macharia, hatahivyo, alisema kufungwa kwa kambi hizo mbili za wakimbizi ni swala ambalo limekuwepo tangu mwaka 2016.

  Uchunguzi huo unakuja wakati Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Fred Matiangi na mwenzake wa Masuala ya Kigeni Raychelle Omamo walifanya mkutano na ujumbe wa washirika 25 wa maendeleo mjini Nairobi kujadili suala hilo.

  Washirika has wa kimaendeleo ni pamoja na Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, na wawakilishi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).

 3. Wanafamilia watano waliofariki wakati wa kumuaga hayati Magufuli wazikwa

  Miili ikiwa kanisani

  Shughuli ya maziko ya wanafamilia watano waliofariki wakati wa shughuli ya kumuaga hayati John Magufuli imefanyika leo jijini Dar es Salaam.

  Shughuli hiyo ilitanguliwa na ibada ya kuwaombea marehemu na kuaga miili katika kanisa la Kilutheri Usharika wa Kimara Korogwe na baadaye mazishi kwenye makaburi ya familia katika eneo la Kimara Dar es Salaam.

  Mtoto Michelle
  Mtoto Natalia
  Mtoto Christian
  Mama, Susan Nzilani
  Mtoto Nathaniel

  Katika hatua nyingine hapo jana Bw. Denis aliiambia BBC kuwa mwili wa msaidizi wao wa kazi aitwaye Anitha ambaye alikuwa akitafutwa umepatikana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

  Kupatikana kwa mwili huo, sasa familia hiyo ya Denis Mtua, imepoteza jumla ya watu sita yaani mke wake, watoto wawili, wapwa zake wawili, na msaidizi wa kazi.

  Maelezo zaidi:

 4. Watu wenye miaka 58 na zaidi kupewa kipaumbele katika chanjo ya corona Kenya

  Kenya kwa sasa inashuhudia wimbi la tatu la maambukizi ya Corona

  Serikali sasa imesema itawapa kipaumbele wale walio na umri wa miaka 58 na zaidi katika shughuli inayoendelea ya kutoa chanjo ya Covid-19.

  Mpango wa awali ulikuwa kuwazingatia mwanzo wahudumu wa afya ,walimu na wale walio katika vikosi vya usalama katika kuwapa chanjo kwa sababu ya mazingira ya kazi zao .

  Lakini Wizara ya Afya sasa inasema uamuzi wa kuwajumuisha wazee katika awamu ya kwanza ulifikiwa baada ya data kuonyesha kuwa watu katika umri huu wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa sugu na wanachangia asilimia 60 ya vifo vilivyorekodiwa nchini.

  Kenya kwa sasa inashuhudia wimbi la tatu la maambukizi ya Corona na idadi ya wanaopatikana na virusi hivyo inazidi kuongezeka kila uchao .

  Tayari hospitali nyingi hazina nafasi katika vitengo vya wagonjwa walio katika hali mahtuti ,ICU hatua ambayo imeilazimu serikali kurejesha tena mpango wa kuwatunza wagonjwa wa Corona majumbani .

  Mwenyekiti wa jopo kazi la utoaji wa chanjo Willis Akhwale amesema uamuzi huo wa serikali unaambatana pia na mapendekezo ya shirika la afya duniani WHO na jopo kazi la kitaifa linaloongoza utoaji wa chanjo .

 5. Waliomburuza barabarani mwanamke mfanyabiashara wasimamishwa kazi Kenya

  Maafisa wakimburuza mfanyabiashara barabarani

  Gavana wa kaunti ya Kisumu amewasimamisha kazi maafisa waliopigwa picha wakimburuza barabarani mwanamke mfanyabiashara wa matunda.

  Vyombo vya habari vimeripoti kuwa mwanamke huyo alikataa kutoa rushwa. Alikuwa akiuza machungwa na ndimu njia ya wapita kwa miguu eneo ambalo limepigwa marufuku kufanyika biashara.

  Mwanamke huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa mmoja kati ya maafisa hao alikaa kwenye gari aina ya pick-up akiwa amemshika mkono wake na kukataa kumuachilia wakati gari hiyo ilipokuwa ikiondoka.

  View more on twitter

  Dereva aliendesha chombo hicho cha moto mpaka katika kituo cha polisi cha karibu baada ya kundi la watu kuamua kukimbiza gari.

  Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu waliokuwa na ghadhabu waliokusanyika katika kituo hicho.

  Gavana Anyang’Nyong’o amesema amewasimamisha kazi maafisa wote waliohusika na tukio hilo mpaka uchunguzi utakapokamilika.

  View more on twitter
 6. Watu wanne wakamatwa kwa kukejeli msiba wa hayati Magufuli

  Kamanda wa Polisi Mbeya, Urlich Matei

  Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kukejeli kifo cha Hayati Dkt. John Magufuli kwa kupika supu.

  Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Urlich Matei amesema ni jambo la kushangaza kwa baadhi ya watu kufanya vitendo hivyo huku nchi ikiwa kwenye maombolezo ya siku 21.

  ‘’Nchi yetu ipo katika huzuni kubwa ya kuondokewa na mpendwa wetu, Dkt John Magufuli, kufuatia kifo hicho,tupo katika maombolezo kwa siku 21, lakini katika kipindi hiki, polisi mkoani Mbeya tarehe 20 tulipata taarifa ya kuwepo kwa watu wanne wakifanyia kejeli msiba huu’’. Kamanda Matei aliviambia vyombo vya habari jijini Mbeya.

  Watu watatu walikamatwa katika eneo la Mwanjelwa wakiwa wameandaa supu ya Mbuzi na utumbo pia wakiwa na ndoo ya pombe ya kienyeji aina ya ulanzi.

  ‘’Vitendo vile ni ishara ya kuleta tafrani na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo lile’’.

  Kole Mwasongwe, Asifiwe Mwasaga na Ernest Kaponela walikamatwa wakiwa na supu walioiandaa barabarani eneo la njiani sambamba na pombe.

  ‘’Tumewachukua na tunaendelea na mahojiano, ushahidi utakapokamilika tutawafikisha mahakamani'' alieleza kamanda Matei.

  Katika tukio jingine, majira ya usiku wa tarehe 20, eneo la Soweto mtaa wa mabuchani, mtu mmoja kwa jina Tumaini Talazwa alikamatwa kwa kosa la kutoa lugha ya kejeli kuhusu msiba huu.

  Kamanda wa polisi amewataka wakazi wa Mbeya kutii sheria bila shuruti wakati huu wa maombolezo.

  Kifo cha rais John Pombe Magufuli: Fahamu Jinsi ya kuepuka mkanyagano katika maeneo ya umati mkubwa

 7. Watu wenye silaha washambulia mji wa kaskazini mwa Msumbiji, Palma

  Shamba la mpunga karibu na Palma, ambapo amana kubwa za gesi zimepatikana pwani, picha ya mwaka 2017 kabla ya uasi kuanza

  Watu wenye silaha wameshambulia mji wa kaskazini mwa Msumbiji, Palma, wenye mradi wa gesi wa gharama za mabilioni ya dola unaoongozwa na Kampuni kubwa ya mafuta ya Kifaransa, Total, vyanzo vimeeleza.

  Uvamizi huo umefanyika wakati ilipotangazwa kuwa ujenzi utaanza hivi karibuni.

  Kazi ilisimama mwezi Desemba kwasababu za kiusalama zilizodaiwa kusababishwa na wanamgambo wa kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo, uasi ulioanza tangu mwaka 2017.

  Milio ya risasi ilisikika mjini humo na kisha mawasiliano yalikatwa, Shirika la habari la Reuters lilinukuu vyanzo vya taarifa vikizungumza na shirika la habari la Kireno , Lusa.

  Maelfu ya watu wamekimbia machafuko katika mji wa Cabo Delgado ulio kaskazini mwa Msumbiji.

  Msumbiji: Je, Cabo Delgado ni kituo cha wapiganaji wa Islamic State?

  Video ya kuogofya iliyochukuliwa Kaskazini mwa Msumbiji

 8. Watu watano waliofariki katika tukio la kumuaga Hayati Magufuli kuzikwa leo

  Watu watano waliopoteza maisha katika tukio la kumuaga Hayati John Magufuli uwanja wa uhuru wanazikwa leo jijini Dar es Salaam.

  Watoto Nathaniel, Michelle, Natalia, Christian na Mama aitwaye Susan watazikwa leo katika eneo la familia kwa mujibu wa baba wa familia Bw.Denis Mutua.

  Hapo jana Bw. Denis aliiambia BBC kuwa mwili wa msaidizi wao wa kazi aitwaye Anitha ambaye alikuwa akitafutwa umepatikana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

  Kupatikana kwa mwili huo, sasa familia hiyo ya Denis Mtua, imepoteza jumla ya watu sita yaani mke wake, watoto wawili, wapwa zake wawili, na msaidizi wa kazi.

  Unaweza kusikiliza mazungumzo ya Bw. Denis Mtua alipozungumza na BBC

  Video content

  Video caption: Familia iliyopoteza watu watano yapata msiba mwingine

  Wote hao walienda kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli siku ya Jumapili katika Uwanja wa Uhuru, lakini hawakurejea tena nyumbani.

  Kwa siku tatu familia hiyo ilikuwa ikimtafuta binti huyo, bila mafanikio kabla ya kuukuta mwili wake kwenye moja ya vyumba vya kuhifadhia maiti.

  Familia ya Mtua inafanya mawasiliano na familia ya Anitha ili kujua kama binti huyo atazikwa Dar es Salaam au nyumbani kwao Njombe, nyanda za juu kusini mwa Tanzania.

  Kifo cha rais John Pombe Magufuli: Fahamu Jinsi ya kuepuka mkanyagano katika maeneo ya umati mkubwa

 9. Ikuzi Kicheko kumuaga kwa mara ya mwisho rais Magufuli

  Ikuzi kicheko ameanza safari ya kuaga mwili kuanzia Dar es Salaam na hatimae amefika mjini Chato kumuaga hayati rais Magufuli. Fedha za safari yake zimechangwa na baadhi ya watanzania.

  Uombolezaji wake umevutia wengi hasa kutokana na mavazi yake ya kihadzabe

  Ikuzi Kicheko akimuomboleza Magufuli
  Image caption: Ikuzi Kicheko akimuomboleza Magufuli
 10. Wakazi wa Chato wamiminika uwanja wa Magufuli kuuaga mwili wa kiongozi wao

  Wakaazi wa Chato mkoani Geita nchini Tanzania wamevumilia baridi kali ya asubuhi ili kwenda kuuona kwa mara ya mwisho na kuuaga mwili wa Hayati John Pombe Magufuli, rais wa awamu ya tano nchini Tanzania aliyefariki kutokana na matatizo ya moyo.

  Khanga za Magufuli zimepata umaarufu mkubwa miongoni mwa waombolezaji
  Image caption: Khanga za Magufuli zimepata umaarufu mkubwa miongoni mwa waombolezaji
  Wakaazi wa Chato wakipanga foleni kuingia katika uwanja ambao jeneza la Magufuli litakuwepo ilii kuuagwa mwili wake kwa mara ya mwisho.
  Image caption: Wakaazi wa Chato wakipanga foleni kuingia katika uwanja ambao jeneza la Magufuli litakuwepo ilii kuuaga mwili wake kwa mara ya mwisho.
 11. Natumai hamjambo. Ni siku nyengine tena ambapo tutaendelea kukupasha mubashara kuhusu yanayojiri kufuatia kifo cha Hayati John Pombe Magufuli nchini Tanzania