Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

time_stated_uk

 1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

 2. Algeria yaonya 'matumizi ya dawa ya minyoo kutibu Covid'

  WHO imetoa tahadhari dhidi ya matumizi ya dawa ya minyoo
  Image caption: WHO imetoa tahadhari dhidi ya matumizi ya dawa ya minyoo

  Wizara ya afya ya Algeria imeonya dhidi ya kutumia dawa ya kupambana na minyoo kwa jina Ivermectin kutibu Covid-19 kwani inaleta "hatari kwa afya ya binadamu", gazeti la kila la kibinafsi El Khabar limeripoti.

  Gazeti hilo limesema limeona barua iliyotumwa na wizara kwa maafisa wa afya wa eneo hilo, ikionya kuwa dawa hiyo inazunguka kwenye soko haramu, na wanapaswa "kujua hatari zinazotokana na utumiaji wa dawa hii" kwa wanadamu.

  Ivermectin hutumiwa kutibu vimelea vya minyoo , lakini wengine wameielezea kama tiba bora ya coronavirus ingawa haijathibitishwa kisayansi.

  Imekuwa maarufu pia kwenye soko haramu nchini Afrika Kusini, ambapo vita vya kortini vinaendelea ikiwa inapaswa kutumiwa kutibu Covid-19.

  Kidonge kwa sasa hakina leseni ya matumizi ya kibinadamu na Mamlaka ya Udhibiti wa Bidhaa za Afya ya Afrika Kusini. Imesajiliwa tu kutibu vimelea katika wanyama.

  Maelezo zaidi:

  Virusi vya corona: Madaktari wa Afrika Kusini wanatumia dawa ambayo haijathibitishwa kutibu Covid-19

 3. Mahakama ya ICC yamfuta mashtaka rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo

  Mahakama ya ICC imefuta mashtaka dhidi ya aliyekuwa rais Ivory Coast Laurent Gbagbo

  Mahakama ya ICC imefuta mashtaka dhidi ya aliyekuwa rais Ivory Coast Laurent Gbagbo.

  Jopo la majaji wa rufaa katika mahakama ya mashtaka ya Jinai ICC siku ya jumatano limeidhinisha uamuzi wa kumpata bila hatia aliyekuwa rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo mwaka wa 2019.

  Majaji wamesema kuondolewa mashtaka dhidi ya Gbagbo kulifanywa kwa njia ifaayo na kutupilia mbali pingamizi za upande wa mashtaka.

 4. Ubalozi wa Marekani wafungwa baada ya ufyatulianaji wa risasi

  Gari la vita la wanajeshi

  Ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Niger, Niamey, umefungwa, huku kukiwa na ripoti za jaribio lililoshindwa la askari kufanya mapinduzi.

  "Ubalozi wa Marekani Niamey utafungwa Jumatano, Machi 31, 2021, kwa sababu ya milio ya risasi iliyosikika karibu na kitongoji chetu.

  Huduma za kibalozi zinasimamishwa hadi itakapotangazwa. Wafanyikazi wote wanahimizwa kukaa nyumbani, hadi hapo itakapotangazwa tena," ilisoma taarifa kwenye tovuti ya ubalozi.

  Milio mikali ya risasi ilisikika mapema leo asubuhi karibu na ikulu ya rais na katika vitongoji vingine vya Niamey.

  Ripoti zinasema hali hiyo sasa inadhibitiwa, chini ya masaa 48 kabla ya kuapishwa kwa Rais Mteule Mohamed Bazoum.

  Ikiwa atachukua madaraka itakuwa ni uhamisho wa kwanza wa kidemokrasia wa kupokezana madaraka nchini Niger.

 5. Tanzania yafunga maisha mwanablogu kwa ulanguzi wa dawa za kulevya

  Shamim Mwasha

  Mahakama kuu nchini Tanzania imemhukumu kifungo cha maisha mwanablogu na mume wake kwa kujihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya.

  Shamim Mwasha ni maarufu nchini Tanzania kupitia blogu yake ya mitindo ya nguo na chaneli ya YouTube.

  Alikamatwa na mume wake Abdul Nsembo nyumbani kwao Dar es Salaam mwezi Mei mwaka 2019.

  Walidaiwa kupatikana na dawa ya kulevya aina ya heroin.

  Wawili hao walifikishwa mahakamani na kunyimwa dhamana.

 6. Makamu wa rais mpya wa Tanzania aapishwa

  Dkt.Philip Mpango ameapa rasmi kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania

  Dkt. Philip Mpango amepishwa kuwa Makamu wa Rais mpya wa Tanzania.

  Hafla ya kuapishwa kwake imeongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,katika Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

  Bw. Mpango anashika wadhifa huo baada ya Rais Samia, kuwasilisha pendekezo la jina lake katika kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi na baadaye jina hilo kuthibitishwa bungeni jana Jumanne.

  Kiti cha Makamu wa Rais wa Tanzania kilikuwa wazi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli mnamo Machi 17 mwaka huu kilichofanya aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aapishwe kuwa Rais.

  Maelezo zaidi:

 7. Waziri mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga apona Virusi vya Corona

  Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, amepona virusi vya Corona baada ya kupimwa Jumatano na kupatikana hana ugonjwa huo.

  Chama cha ODM anachokiongiza kimeatangaza kupitia Twitter kwamba Raila hayupo hatarini tena na ataanza kuangazia masuala yanayofaa kushughulikiwa.

  View more on twitter

  Odinga alipatikana na virusi vya Corona Machi tarehe 11 mwaka huu baada ya kulalamika kuwa na uchovu alipomaliza msururu wa kampeni za mwafaka wa maridhiano (BBI) katika eneo la Pwani.

  Raila alikutana na maafisa wa chama hicho Jumatano kujadili matukio ya hivi karibuni nchini ikiwa ni pamoja na utoaji wa chanjo nchini humo na hali ya uchumi wa Kenya.

  Alithibitisha kujitolea kwa ODM kufanikisha mwafaka wa BBI uliotiwa saini kati yake na Rais Uhuru Kenyatta na vile vile Muswada wa Marekebisho ya Katiba, 2020 uliotokana na BBI.

 8. Kesi dhidi ya mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari Rwanda yaendelea

  Yves Bucyana

  BBC Swahili Kigali

  Jean Claude Iyamuremye
  Image caption: Jean Claude Iyamuremye anatuhumiwa kwa kuhusika na mauaji ya kimbari Rwanda

  Mahakama mjini Nyanza kusini mwa Rwanda imeendelea kusikiliza kesi ya Bwana Jean Claude Iyamuremye maarufu ''Nzinga'’ aliyeshtakiwa mauaji ya kimbari.

  Amekana kuhusika kwa njia yoyote katika mauaji ya kimbari wala katika mashambulio yaliyofanywa na wanamgambo katika maeneo mbali mbali mjini Kigali na kuomba kuachiliwa huru mara moja.

  Jean Claude Iyamuremye maarufu Nzinga na mawakili wake leo wamepinga hoja za mwendesha mashtaka kuwa mshatakiwa alihusika katika mauaji dhidi ya Watutsi yaliyofanyika katika maeneo mbali mbali mjini Kigali ambako Watutsi walikuwa wamejificha wakati wa mauaji ya kimbari.

  Waliambia mahakama kuwa kama yeye alikuwa na umri wa miaka 18 tu wakati wa mauaji ya kimbari na pia alikuwa mwanafunzi na hakuwa na uwezo wa kukaa pamoja ama kujadili lolote na vigogo waliopanga na kutekeleza mauaji ya kimbari.

  Kadhalika amesisitiza kwamba hangeweza kuwa na nia yoyote ya kuuwa Watutsi kwa kile alichoeleza kwamba mama yake alikuwa Mtutsi.

  Upande wa mashtaka unadai kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba Bwana Iyamuremye Nzinga alikuwa akiendesha gari lililojaa wanamgambo na askari waliotekeleza mauaji katika kambi zilizowahifadhi watutsi.

  Kuhusu hoja za mashahidi,Iyamuremye Jean Claude ameiambia mahakama kuwa taarifa za mashahidi zilikuwa zinatofautiana na pengine mashahidi walionekana kujichanganya katika ushahidi wao na kwamba yale waliyosema katika upelelezi nchini Uholanzi yanatofautiana na waliyosema katika ngazi ya upelelezi ya Rwanda.

  Wakati wa vikao vya kesi vilivyotangulia mwendeshamashtaka alisema kwamba kulingana na ushahidi waliotoa mahakamani hakuna budi mstakiwa kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

  Leo upande wa utetezi umeiomba mahakama kutupilia mbali hukumu hiyo na badala yake kumwachilia huru mara moja.Hukumu itatolewa tarehe 30 mwezi 6.

  Iyamuremye Jean Claude mwenye umri wa miaka 45 alirudishwa Rwanda na nchi ya Uholanzi mwaka wa 2016 ili kukabili mashtaka ya mauaji ya kimbari.

  Alikamatwa na kuziliwa Uholanzi mwaka 2013 alipokuwa dereva wa watumishi wa balozi za Israel na Finland.

 9. Wakenya washinikiza kuondolewa kwa masharti ya kuzuia corona

  Maandamano

  Baadhi ya makundi ya kijamii nchini Kenya yametishia kufanyamaandamano ya kupinga masharti ya kudhibiti maambukizi ya corona.

  Wiki iliyopita Rais Uhuru Kenyatta alipiga marufuku usafiri wa kutoaka na kuingia majimbo matano yanayosadikiwa kuwa na viwango vya juu vya maambukizi ukiwemo mji Mkuu wa Nairobi, kukomesha ongezeko la maabukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

  Baadhi yao wanasema wana majukumu ya
  Image caption: Baadhi ya wale ambao walifanya kazi katika hoteli, wanasema wana familia za kulisha lakini waajiri wao wamelazimika kufunga hoteli zao
  Waandanaji

  Rais Kenyatta pia alipiga marufuku uuzaji wa pombe katika maeneo yaliyowekewa masharti ya usafiri na kuagiza wenye migahawa kuuza vyakula vya kwenda navyo nyumbani.

  Bunge la Mwananchi na Muungano wa wananchi wa Citizens Alliance unasema kuwa masharti hayo yanawaathiri wananchi wa kawaida , wakati shughuli za kisiasa zilichangia "kueneza" virusi.

 10. ICC kutoa uamuzi juu ya kuachiliwa kwa Gbagbo wa Ivory Coast

  Bw.Gbagbo

  Mahakama ya Kimataifa ya Kesi za Jinai ICC leo inatarajiwa kuamua ikiwa itadumisha hatua ya kumuondolea mashtaka Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo.

  Bw.Gbagbo na kiongzi wake wa zamani wa Charles Ble Goude walistakiwa kwa kujihusisha na ghasia baada ya uchaguzi katika nchi hiyo ya Afrika ya Magharibi zaidi ya mwongo mmoja uliopita.

  Ghasia zilizuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 wakai tBw Gbagbo – ambaye alikuwa madarakani kwa muongo mmoja – kukubali kushindwa .

  Waliondolewa kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu mwaka 2019.

  Upande wa mashtaka ulikata rufaa dhidiya uamuzi wa kumuondolea makossa Laurent Gbagbo, ukihojijinsi uamuzi wa kwanza ulivyofikiwa na kusisitiza kwamba maelfu ya nyaraka na mashahidi 96 waliotoa ushahidi wao wakati wa kesi, walidhibitisha kuwa kwamba uhalifu ulitekelezwa

  Gbagbo mwenye umri wa miaka 75 amekuwa akiishi mjini Brussels lakini ana matumaini ya kurudi nyumbani ikiwa rufaa ilitowasilishwa na waendesha mashtaka itakataliwa.

  Hukumu hiyo itafuatiliwa kwa karibu Ivory Coast, ambako rais huyo wa zamani anasalia kuwa na ushawishi mkuwa, katika nchi hiyo ambayo bado inajitahidi kupata utulivu wa kisiasa.

  Mwaka jana kulitokea makabiliano makali nchini humo baada ya hasimu wa kisiasa wa muda mrefu wa Bw. Gbagbo, Alassane Ouattara kutangaza kwamba ana mpango wa kugombea urais kwa muhula wa tatu .

 11. Makamu wa rais mteule wa Tanzania kuapishwa leo

  Dkt Mpango

  Aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuapishwa leo kuwa makamu wa rais mpya katika Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

  Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa, Dkt Mpango ataapishwa saa tisa.

  Bw. Mpango ataapishwa kushika wadhifa huo baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kuwasilisha pendekezo la jina lake katika kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi na baadaye jina hilo kuthibitishwa bungeni jana Jumanne.

  Maelezo zaidi:

 12. Mji mkuu wa Niger uko katika hali ya juu ya tahadhari, kulikoni?

  Niger is struggling to contain an Islamist insurgency.

  Milio mikali ya risasi imesikika karibu na eneo la makazi ya rais ambalo pia lina ofisi ya rais katika mji wa Niamey,Niger Jumatatno asubuhi.

  Milio hiyo ya risasi ilisikika karibu saa tisa usiku -03:00 (02:00 GMT), na ilidumu kwa karibu dakika 15, ikifuatiwa na milio ya risasi ya bunduki ndogo, wakazi walisema.

  Hali imesalia kuwa tete na mji huo kwa sasa umewekwa chini ya tahadhari ya hali ya juu.

  Ufyatulianaji risasi huo umejiri chini ya saa 48 kabla ya sherehe ya kuapishwa kwa rais mpya mteule, Mohamed Bazoum.

  Serikali ya Niger haijatoa tamko lolote kuhusiana na tukio hilo.

  Kumeshuhudiwa ongezeko la mashambulio kutoka kwa makundi ya wanamgambo waliojihami huku taharuki za kisisasa zikikumba nchi hiyo kufuatia ushindi wa Bw. Bazoum katika uchaguzi mkuu wa urais wa mwezi Februari.

  Mpinzani wake rais wa zamani Mahamane Ousmane, ambaye alishidwa katika duru ya pili ya uchaguzi, amepinga matokeo na kupuuza uamuzi wa mahakama wa kudumisha matokeo hayo.

 13. Libya 'mji wa mashetani'

  Abdel Manaam Mahmoud anamzika kaka yake ingawa hawezi kuwa na uhakika wa asimia 100 kwamba ni yeye

  Kama mtu mzima wa familia, Abdel Manaam Mahmoud hakuwa na budi zaidi ya kuzika mwili wa kaka yake Esmail katika nyumba yake ya milele. Lakini pia, huenda anayemzika hii leo, asiwe kaka yake kama anavyofikiria.Soma zaidi hapa.

 14. Afrika Kusini yapiga marufuku uuzaji wa pombe

  Rais Ramaphosa anasema unywaji pombe unachangia tabia ya uzembe
  Image caption: Rais Ramaphosa anasema unywaji pombe unachangia uzembe

  Serikali ya Afrika Kusini imepiga marufuki uuzaji wa pombe wa kwenda nayo nyumbani wikendi hii ya Pasaka, kuzuia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona .

  Rais Cyril Ramaphosa amesema pombe inachangia tabia ya kutojali na uzembe.

  Mabaa na migahawa hata hivyo huenda zikaruhusiwa kuuza vinywaji

  Mikusanyiko ya kidini pia imedhibitiwa kwa hadi asilimia 50 ikiwa inafanyika ndani ya jengo.

  Maambukizi ya corona yamepungua Afrika Kusini baada ya wimbi la pili la maambukizi kupanda mwezi Januari.

  Marufuku dhidi ya uuzaji pombe imewekwa mara kadhaa tangu janga la corona lililipoanza.

 15. Gavana anusurika kifo katika shambulio Sudan Kusini

  Governor Luis Lobong survived the ambush in Eastern Equitoria state

  Karibu watu 20 wamefariki katika jimbo la Equatoria Mashariki mwa Sudan Kusini ambako Gavana Louis Lobong Lojore aliponea shambulio hatari, Katibu wake wa habari amesema.

  Alinadro Lotok alisema Bw. Lobong aliponea shambulio kali Jumatatu jioni kutoka kwa vijana wa jamii ya Buya waliokuwa wamejihami.

  “Gavana Lobong alikuwa katika kambi ya -15 kutuliza hali ya taharuki katika eneo hilo baada ya shambulio la siku ya Jumapili dhidi ya kituo hicho, kusababisha vifo vya watu 17 ," alisema.

  Vijana waliokuwa na hasira huku wakiwa wamejihami walimfuata gavana na kushambulia kambi ya kijeshi Camp-15, na kuongeza idadi ya vifo katika visa hivyo viwili kufikia karibu 20, aliongeza.

  "Baada ya makabiliano ya risasi ya saa mbili na vijana hao, kitengo cha ulinzi wa gavana na askari katika kambi ya jeshi ya Camp-15 walifanikiwa kuwarudisha nyuma."

  Miongoni mwa waliofariki ni walinzi wa gavana na mke wa askari. Wengine watatu walijeruhiwa vibaya.

 16. Hospitali ya Kenya yasitisha utoaji wa chanjo ya corona

  Chanjo

  Hospitali moja ya kibinafsi jijini Nairobi imesitisha kutoa chanjo ya Covid-19 kutokana na uhaba wake, licha ya serikali kuwa na zaidi ya dozi milioni moja.

  Hospitali ya Aga Khan ilitangaza kwamba itaendelea na huduma za utoaji chanjo wakati itakapopata chanjo zaidi kutoka kwa serikali.

  Wizara ya Afya siku ya Jumanne ilisema ni watu 130,575 pekee ambao wamechanjwa kote nchini kufikia sasa, licha ya dozi 806,000 kusambazwa kati ya dozi milioni 1.12 zilizopo.

  Hayo yanajiri baada ya hospitali nyingine ya kibinafsi kuanza kutoza ada ya kupata chanjo ya corona ya Sputnik V ya Urusi, ambayo serikali imetoa tahadhari dhidi ya utumiaji na usambazaji wake.

  Serikali ya Kenya imeidhinisha matumizi ya chanjo ya Oxford-AstraZeneca.

  Ubalozi wa Urusi nchini Kenya siku ya Jumatatu ilijitenga na uingizaji wa chanjo ya Sputnik V nchini humo.

  Soma zaidi:

  Ukweli kuhusu hali ya mtu baada ya kupata chanjo ya Covid-19

 17. Hujambo na karibu katika matangazo mubashara kutoka BBC Swahili leo Jumatano 31.03.2021