Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Esther Namuhisa

time_stated_uk

 1. Tukutane tena kesho katika matangazo mbashara, usiku mwema!

 2. 'Rais Samia ameagiza zifunguliwe televisheni za mtandaoni tu'

  Waziri wa habari nchini Tanzania Innocent Bashungwa na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Gerson Msigwa wametoa ufafanuzi kuwa agizo la rais Samia Suluhu Hassan kuvifungulia vyombo vya habari nchini humo linahusu televisheni za mtandaoni tu na si vyombo vyote.

  Toka jana jioni kumekuwa na mjadala mkali nchini Tanzania baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Dkt. Hassan Abbas kueleza kuwa agizo la rais Samia linalenga televisheni za mtandaoni tu na haligusi magazeti yaliyofungiwa pia.

  Kauli hiyo ya Dkt Abbas ilipingwa vikali na wadau wa habari wakimtuhumu kuwa amepindisha maelekezo ya rais juu ya kuvifungulia vyombo vyote mpaka magazeti.

  Msigwa ametoa ufafanuzi wake kupitia ukurasa wa Twitter huku Waziri Bashungwa akiitisha mkutano na wanahabari.

  Bashungwa ameeleza kufikia sasa kuna televisheni 400 za mtandaoni zilizosajiliwa, na kwamba zote zilizofungiwa zinatakiwa kurejea kazini. Kuhusu vyombo vingine nje ya televisheni za mtandaoni, vitashughulikiwa kesi kwa kesi.

  View more on twitter
 3. 'Hakuna kifo kilichotokea kutokana na chanjo ya AstraZeneca Kenya'

  Bodi ya ya Ufamasia na sumu nchini Kenya imekanusha ripoti kwamba mtu mmoja ameaga dunia baada ya kupewa chanjo ya Oxford AstraZeneca. Kupitia taarifa Bodi hiyo imesema kulikuwa na ripoti za kupotosha kuhusu athari za chanjo hiyo kwa watu waliodungwa dozi ya chanjo hiyo.

  Bodi hiyo imesema kati ya visa 279 vya watu waliochanjwa na kupata athari mbaya,272 ni walikuwa na athari ndogo ambazo zilishughulikiwa baada ya muda mfupi. Bodi hiyo imesema inachunguza athari zilizowakumba watu hao na hata wengine 7 ambao walipata athari mbaya tayari wameshughulikiwa .

  View more on twitter
 4. Aliyekuwa Gavana Nairobi akutwa na corona baada ya kupata chanjo

  Roncliffe Odit

  BBC Nairobi

  Facebook: Evans Kidero

  Aliyekuwa Gavana wa Jimbo la Nairobi nchini Kenya, Evans Kidero, amekutwa na virusi vya Corona, wiki moja tangu achomwe sindano ya chanjo ya ugonjwa wa COVID-19.

  Kidero amesema alipatikana na ugonjwa huo Jumanne, Aprili 6, wakati ambao yeye na familia yake walipokwenda kufanya vipimo baada ya kuonesha dalili za corona.

  Kwa mujibu wa Gavana huyo wa zamani, amesema alikutwa na virusi hivyo vya corona wiki moja baada ya kupatiwa chanjo ya ugonjwa huo mnamo Machi 29, 2021.

  Aliongeza kusema wengine katika familia yake walipimwa lakini hawakukutwa na Corona.

  Sasa Kidero atakuwa akijitenga kwa muda wa wiki mbili zijazo.

  Taarifa hii inakuja wakati serikali ya Kenya ikianza kufanya uchunguzi wa madai kwamba mgonjwa mmoja alifariki baada ya kuchomwa sindano ya chanjo dhidi ya Covid-19.

  Mapema leo katika mkutano na wanahabari, Dkt. Peter Mbwiiri Ikamati, Naibu Mkurugenzi wa Bodi ya Dawa na Sumu nchini kenya, amesema kwamba walikuwa wakichunguza kifo kilichotokea kwa raia mmoja wa Kenya kupokea chanjo na kufariki, na kuongeza kuwa jumla ya watu 279 wameathiriwa vibaya baada ya kupokea chanjo hiyo.

  Lakini muda mfupi baadae, Dkt. Collins Taabu - mkuu wa Programu ya Chanjo ya Kitaifa – alikanusha hilo, akisema hakuna uhusiano na kwamba bado haijafahamika ikiwa kifo hicho kilisababishwa na chanjo hiyo.

  “Bora tu umepewa chanjo, chochote kitakachokupata baadae kitaangaliwa, kuchunguzwa, na kuripotiwa. Ndio maana tunafuatilia kesi hii, ”alisema Dkt. Ikamati.

 5. Nigeria yasitisha utoaji wa chanjo ya Oxford-AstraZeneca

  nigeria

  Nigeria imesitisha utoaji wa chanjo ya Oxford-AstraZeneca ili kuwapa dozi ya pili waliopewa ya kwanza.

  Mamlaka za nchini Nigeria zimesema zitaacha kutoa chanjo ya Oxford-AstraZeneca COVID-19 wakati watakapotumia nusu ya dozi zilizopo sasa.

  Naibu Waziri wa Afya amewaambia wanahabari kuwa nchi haikuwa na uhakika wa ni lini awamu ya pili ya dozi ya chanjo hiyo itafaika nchini humo; kusimamishwa huko kutawawezesha wale ambao walikuwa wamepokea dozi ya kwanza kumaliza chanjo yao kwa kupewa ya pili.

  Chanjo ya AstraZeneca inahitaji mtu kupewa dozi mbili. Naibu Waziri wa Afya Olorunnimbe Mamora amesema serikali ina wasiwasi juu ya kuweza kutoa dozi ya pili kwa wale ambao tayari wamepata dozi yao ya kwanza .

  Takwimu zilizotolewa na maafisa wa huduma ya afya zinaonesha kwamba karibu Wanigeria milioni moja wamepokea chanjo yao ya kwanza. Wafanyakazi wa afya na watu wanaoaminika kuwa katika mazingira magumu ndio wamepewa kipaumbele.

  Nchi hiyo ilipata dozi milioni nne za chanjo ya Oxford-AstraZeneca mnamo Februari, na mamlaka hazina uhakika ni lini awamu inayofuata itawasili.

  Wakati huo huo Nigeria imeanza majaribio ya kliniki kwa chanjo mbili za covid-19 ambazo wanasayansi wake wameanzisha.

  Nigeria ina rekodi ya watu 162,000 kupata virusi vya corona na zaidi ya 2,031 kufariki kutokana na virusi hivyo.

 6. Akamatwa kwa kutengeneza bango la picha ya Rais Kenyatta kulalamikia mikopo ya IMF

  View more on twitter

  Mwanaharakati Edwin Kiama anayedaiwa kutengeza bango lenye picha ya Rais Uhuru Kenyatta nchini Kenya ili kulalamikia hatua ya serikali kuuchukua mkopo mwingine wa shilingi dola bilioni 255 au dola bilioni 2.34 amekamatwa na polisi.

  Wanaharakati wenzake wametumia mtandao wa twitter kuitaka polisi imuachie huru baada ya kushtumiwa kwa kutekeleza uhalifu wa mtandaoni .

  Kiama katika bango lake alidai kwamba fedha mbazo serikali hukopa hufujwa na maafisa wakubwa .

  Tangu wiki iliyopita,Wakenya wamekuwa wakilalamika mitandaoni na hata kwenye kurasa za mitandao za shirika la Fedha duniani IMF ambalo liliidhinisha mkopo huo kwa serikali.

  Waziri wa Fedha Ukur Yatani hata hivyo ametetea mkopo huo mpya akisena unalenga kuisaidia Kenya kukabiliana na athari za janga la Corona na kusawazisha mzigo wa madeni ambayo Kenya inadaiwa.

  Hadi kufikia sasa Wakenya wapatao 200,000 wamesaini nyaraka mitandaoni kuitaka IMF kutoipa Kenya mkopo wowote.

 7. Watu 15 wamefariki kwenye ajali ya gari Mombasa

  Watu wapatao 15 wamefariki katika ajali ya gari iliyotokea barabara ya Mombasa-Malindi nchini Kenya, maofisa wa serikali wameiambia BBC.

  Watu wengine ishirini wamejeruiwa katika ajali hiyo iliyotokea mapema asubuhi ya leo katika ajali hiyo iliyohusisha mabasi mawili.

  Madereva wa magari yote mawili wamefariki dunia hapo hapo.

  Mashaidi wa ajali hiyo wamesema sehemu ambayo ajali hiyo imetokea katika eneo lililokuwa katika ujenzi.

 8. FIFA yaifungia Chad katika michuano ya kimataifa

  fifa

  Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, limeifungia Chad kushiriki michuano ama michezo yoyote ya kandanda ulimwenguni la baada ya serikali ya nchi hiyo kuingilia kati namna ambavyo shirikisho la soka nchini humo linavyofanya kazi.

  Hatua hii imekuja baada ya waziri wa vijana na michezo kuvunja shirikisho la soka nchini Chad mnamo mwezi Machi.

  Baada ya tangazo hilo lililotolewa na serikali ya Chad, Shirikisho la Soka Barani Afrika (Caf) liliitoa timu ya taifa katika raundi ya pili ya kufuzu kuingia kombe la mataifa ya Afrika.

  Chad haipo kwenye michuano yeyote ya kimataifa baada ya kuondolewa katika mashindano ya kombe la dunia ya mwaka 2022 na Sudan mwaka 2019.

  Taarifa rasmi kutoka shirikisho la soka la dunia limesema: "baraza la Fifa linaweza kuondoa marufuku hayo muda wowote kabla ya mkutano ujao wa Fifa na tutatoa taarifa rasmi."

  Mkutano ujao unatarajiwa kufanyika mtandaoni Mei 21.

 9. Kim Kardashian ajiunga klabu ya mabilionea

  mm

  Nyota wa Marekani wa kipindi cha TV Kim Kardashian West ameingia katika klabu ya matajiri wakubwa.

  Utajiri wake umefikia thamani ya dola bilioni moja(£720m) unaotokana na vipodozi, mavazi pamoja na mapato yake ya kipindi cha TV, mikataba mbalimbali na uwekezaji, Jarida la Forbes limeandika.

  Kwa sasa Kim Kardashian ni miongoni mwa idadi ya watu 2,755 ambao wameainishwa katika orodha ya mabilionea duniani iliyowekwa na jarida la Forbes.

  Muasisi wa Amazon Jeff Bezos anaongoza kwa kuwa na utajiri wa thamani ya dola bilioni 177.

  Wamarekani wengine ambao waliongezwa kwa mwaka uliopita ni muasisi wa programu ya mahusiano ya Bumble dating app,Whitney Wolfe Herd ($1.3bn), mtengeneza filamu Tyler Perry ($1bn) na Miriam Adelson ($38.2bn).

  Kim Kardashian West na mume wake ambaye Kanye West alikuwa tayari kwenye orodha kwa kuwa na dola bilioni 1.8 lakini dada yake wa kambo Kylie Jenner aliondolewa katika orodha hiyo mwezi Mei mwaka jana. Jarida hilo lilimshutumu kwa kudanganya thamani ya biashara ya vipodozi.

  Kim amefanikiwaje kufikia hapo?

  Jarida la Forbes limejumuisha thamani ya dola milioni 780 iliyoongezeka na kufikia dola bilioni moja inayotokana na biashara yake ya vipodozi na kampuni ya mavazi.

  Kampuni ya vipodozi ya KKW Beauty ilianzishwa mwaka 2017 na kampuni ya nguo ya Skims ilianzishwa miaka miwili iliyopita baada ya kuzindua vazi aliloliita Kimono, ingawa ilishuka kutokana na shutuma za kitamaduni.

  Bi.Kardashian West aliuza 20% ya kampuni ya vipodozi ya KKW Beauty mwaka jana kwa dola milioni 200, katika mkataba wa biashara ambao unafika thamani ya $1bn.

  Mradi wake wa sasa wa Skims una nguo za ndani na nguo ndefu na umesaidia katika mafanikio yake.

  Nyota huyo ametumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara zake , sasa akiwa na wafuasi milioni 213 kwenye Instagram; wafuasi milioni 69.7kwenye Twitter.

 10. Jeff Bezos aibuka tena kuwa tajiri zaidi duniani

  jeff

  Jeff Bezos ametajwa kuwa mtu tajiri zaidi kwa miaka minne mfululizo, akiwa na utajiri wenye thamani ya dola bilioni 177 , huku Elon Musk akiwa tajiri wa akiwa na utajiri wa thamani ya dola bilioni 151, wakati ambao hisa za Tesla na Amazon zimeongezeka.

  Mabilionea wote wawili wana thamani ya utajiri wa dola trilioni 13.1, wakati mwaka jana walikuwa na dola trilioni 8 . Marekani bado inaongozakwa kuwa na mabilionea 724, ikifuatiwa China ( Hong Kong na Macao zikiwemo) kwa 698.

  Orodha ya 35 ya mabilionea duniani kote imeongezeka na kufika 2,755-na bilionea -660 kuongezeka kwa zaidi ya mwaka mmoja.

  Rekodi mpya ambayo iko juu ina mabilionea 493 kila mwaka, ikijumuisha 210 kutoka China na Hong Kong. Na wengine 250 ndio wanashuka utajiri, ila bado 86% ni matajiri zaidi ya mwaka uliopita.

 11. Maadhimisho ya siku ya kimbari Rwanda

  Yves Bucyana

  BBC Swahili

  Rwanda

  Leo tarehe 7 April, Rwanda inakumbuka mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi kwa mara ya 27.

  Ilikuwa tarehe 7 April mwaka 1994 baada ya ndege ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Juvenal Habyarimana ilipotunguliwa akiwa pamoja na aliyekuwa rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira.

  Kwa mjibu wa umoja wa mataifa watu zaidi ya laki nane, Watutsi pamoja na wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa mnamo kipindi cha siku 100.

  kimbari

  Katika kuadhimisha siku hii, inatarajiwa kuwa viongozi wakuu wa serikali wataweka mashada ya maua na kuwasha mwenge kwenye makaburi ya makumbusho ya mauaji ya kimbari eneo la Gisozi mjini Kigali lakini hakuna hafla nyingine zinazotarajiwa kufanyika kutokana na janga la Covid 19.

  Wakati huo huo baadhi ya manusura wa mauaji hayo wanalalamikia kutokuwa na makazi huku wengine nyumba zao zikiwa zimezeeka zikihitaji kukarabatiwa.

  rwanda

  Shirika linalotetea manusura wa mauaji ya kimbari IBUKA kwa kifupi linasema suala la kutokuwa na makazi kwa manusura linatia wasiwasi wakati huu.

  Hata hivyo wakuu wa mfuko wa serikali wa kusaidia manusura wa mauaji ya kimbari wameiambia BBC kwamba swala la makazi hayo litakuwa limeishapatiwa ufumbuzi mnamo miaka miwili kuanzia sasa.Bi Uwacu Julienne ni mkuu wa mfuko huo:

  ‘’Manusura ambao bado hawana nyumba ni takriban 870 nchini kote.lengo letu ni kuwa tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa nyumba hizo hadi ifikapo mwaka 2024. Na kuhusu kukarabati nyumba za zamani sasa tumeanza sensa ya kujua idadi ya zinazohitaji kukarabatiwa haraka iwezekanavyo.’’

  Mkuu wa mfuko huo anasema kwamba nyumba zipatazo elfu 30 zimekwisha jengwa kwa ajili ya manusura wa mauaji ya kimbari.

 12. Umoja wa Mataifa: Watu milioni 27 wanakabiliana na njaa DRC

  drc

  Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yamesema theluthi ya wakazi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanakabiliwa na njaa kali na wametoa wito wa kuongezewa fedha za dharura ili kukabiliana na janga hili.

  Shirika la chakula duniani (WFP) na shirika la chakula na kilimo yamesema , hali haijawahi kuwa mbaya kiasi hiki kwa kuwa na raia wa Congo zaidi ya milioni 27 ambao wana uhitaji wa chakula kwa haraka- hii ni idadi kubwa ya watu kuliko eneo lolote lile duniani.

  Lakini mashirika hayo ya UN yameelezea ukubwa wa janga kuwa ni wa kushangaza na kusema DRC inapaswa kuwa na uwezo wa kulisha watu wake na hata kuuza nje chakula cha ziada.

  Migogoro ndio chanzo cha njaa hiyo haswa katika jimbo la mashariki ambako kuna makundi ya waasi ambao wanafanya mashambulizi kila mara.

  Hali ni mbaya katika jimbo la Kasai ambako kulikuwa na ghasia pia.

  Mashirika ya UN yamesema janga la virusi vya corona pamoja na uchumi kushuka pia kumechangia kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

 13. Habari...karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya ukurasa wa BBC Swahili leo 07/04/2021.