Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Ambia Hirsi na Lizzy Masinga

time_stated_uk

 1. Na kufikia hapo tumefika mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo .Kwaheri

 2. Watu 29 wapoteza maisha kutokana na corona Tanzania

  Waziri wa Afya wa Tanzania Dkt Dorothy Gwajima

  Watu 29 wamepoteza maisha kutokana na kuugua ugonjwa wa Covid-19 nchini Tanzania.

  Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Dkt Dorothy Gwajima alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hii leo kuzungumzia hali ya uwajibikaji katika kuchukua hatua dhidi ya virusi vya corona.

  ''Tusichukulie kwa wepesi tu kuwa mbona wimbi la kwanza na la pili lilipita na mimi nipo na fulani yupo, wako wenzetu wengi wamepita na hayo mawimbi , ukabaki wewe kwa kusudi la Mungu na hata leo wapo waliopita na jana wapo waliopita''.

  ''Ikumbukwe pia si kuwa watu hawafariki, la hasha, na kwa takwimu za tarehe 21mwezi Julai hesabu inasema kuwa watu 29 wamefariki kwa ugonjwa wa corona''.

  ‘’Jamii ya virusi vya corona inabadilika na kutofautiana makali ya kushambulia hivyo amesema tusiipe miili yetu kazi ya ziada kwamba unauchosha mwili kwa kuuacha tu’’.Alisema waziri Gwajima

  Amesema kuwa tarehe 21 mwezi Julai Tanzania ilikuwa na wagonjwa 682, wiki mbili kabla walikuwa wagonjwa 408, hivyo amesema hii ni ishara kuwa wagonjwa wanaongezeka.

  ''Idadi hii ndio takwimu zilizotufikia na tunajua vituo vyetu vingine viko mbali, takwimu mpaka wakuletee sio leo. Lakini kuna watu wanaugulia majumbani wala hawafiki kwenye vituo.

  Lakini pia kwa jana pekee Dkt Gwajima amesema wako wagonjwa waliolazwa 176 nchi nzima, acha wale wanaougulia nyumbani.

  Kuhusu kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya virusi vya corona, waziri Gwajima amesema viongozi katika maeneo yao wanawajibika kuhakikisha kuwa hatua zinazostahili zinachukuliwa katika kupambana na janga la corona.

  “Serikali haitaendelea kuvumilia kuona baadhi ya viongozi ambao hawatimizi majukumu yao katika kupambana na Uviko 19” .Alisema Dkt Gwajima.

 3. Jadon Sancho: Winga wa England ajiunga na Man United kwa £73m kutoka Borussia Dortmund

  sancho

  Winga wa Uingereza Jadon Sancho anasema kujiunga na Manchester United ni "ndoto inayotimia" baada ya kumaliza uhamisho wake wa pauni milioni 73 kutoka Borussia Dortmund.

  Sancho ndiye mchezaji wa pili mwenye gharama ya juu zaidi wa England wakati wakati wote nyuma ya mwenzake mpya wa United Harry Maguire.

  Anajiunga na United kwa mkataba wa miaka mitano.

  "Nitashukuru Dortmund kila mara kwa kunipa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, ingawa siku zote nilijua kwamba nitarudi England," Sancho, 21, alisema

  "Nafasi ya kujiunga na Manchester United ni ndoto iliyotimia na siwezi kungojea kunawiri kwenye Ligi ya Premia.

  "Hiki ni kikosi kichanga na cha kusisimua na najua, kwa pamoja, tunaweza kuendeleza kuwa kitu maalum cha kuleta mafanikio ambayo mashabiki wanastahili."

  United ilikubali ada ya Sancho mnamo 1 Julai na mkataba wake wa miaka mitano na kilabu una chaguo la kuongezwa kwa miezi 12.

  Kukamilika kwa makubaliano hayo kunamalizia harakati ya muda mrefu ya United ya kutafuta mchezaji wa zamani wa Manchester City Sancho waliyetarajia kumsaini msimu uliopita wa kiangazi lakini hawakuweza kukubalina kuhusugharama yake.

  Sancho alifunga mabao 50 na kusaidiakufunga mabao 57 katika mechi 137 za Dortmund.

  Kocha wa United Ole Gunnar Solskjaer anasema Old Trafford itampa Sancho "jukwaa analohitaji kutoa talanta yake ambayo haijatumika".

  "Jadon ni aina ya mchezaji ninayetaka kumleta kwenye kilabu - ni mchezaji wa mbele katika mitindo ya Manchester United," Solskjaer aliiambia tovuti ya kilabu.

  "Atakuwa sehemu muhimu ya kikosi changu kwa miaka ijayo na tunatarajia kumuona akinawiri. Mabao yake yake na rekodi za kusaidia zinajisamamia na pia ataleta kasi kubwa, uzuri na ubunifu kwa timu.

  wachezaji

  Kurudi kwa Sancho kwenye ligi ya England kunakuja baada ya kuisaidia timu ya taifa kufika fainali ya Mashindano ya Euro , ambapo walishindwa kwa penati na Italia.

  Mchezaji huyo wa zamani wa vijana wa City, pamoja na Bukayo Saka na sasa mwenzake wa United Marcus Rashford, walilengw akatika ubaguzi wa rangi kwenye mitandao ya kijamii baada ya kushindwa kufunga bao kwenye mikwaju ya penalti

  Kuhamia kwa Sancho kwenda Old Trafford kutamfanya ajiunge na mwenzake wa England Rashford, lakini pia Edinson Cavani, Anthony Martial na Mason Greenwood kwa kile kinachoweza kuwa safu hatari ya ushambulizi ya timu ya Solskjaer.

  Sancho alifunga mabao 16 katika mashindano yote wakati wa msimu wa 2020-21, tano chini ya Rashford, lakini nne zaidi ya Greenwood, na tisa zaidi ya Martial. Cavani, ambaye alijiunga na United kwa uhamisho wa bure mwaka jana baada ya kuondoka Paris St-Germain, alitikisa nyavu mara 17.

  Katika misimu minne huko Dortmund, Sancho alisadia katika kufunga mabao 57 na akaunda nafasi 65 kubwa, zaidi ya Rashford, Martial, Greenwood na Cavani katika kipindi hicho hicho.

  Sancho pia yuko vizuri ikilinganishwa na majina makubwa huko Uropa.

  Tangu kuanza kwa msimu wa 2018-19, ni wachezaji saba tu ambao wana mabaoa na kusaidia kufunga mengine mengi kumliko nyota huyo wa kimataifa wa England. Kati ya wachezaji hao, ni Lionel Messi (43) wa Barcelona tu ndiye ameunda mabao mengi kuliko Sancho (41) wakati huo.

  Tetesi za Soka Ulaya Ijumaa 23.07.2021: Kane, Mbappe, Pogba, Varane, Kessie, Hazard, Xhaka

  Olimpiki Tokyo 2021: Ndoto ya miaka 40 ya Tanzania kupata ushindi itatimia?

 4. Mzozo Tigray : Misaada yahitajika wakati mapambano yakiendelea

  Kumekuwa na ongezeko la hofu ya ukosefu wa chakula Tigray

  Mapambano makali ya miezi minane ya kuwania udhibiti wa mji wa kaskazini wa Tigray nchini Ethiopia yameenea mpaka kwenye mji jirani wa Afar katika kipindi cha juma lililopita.

  Takribani raia 20 wameuawa na watu 54,000 wamekimbia makazi yao, ripoti zinasema, huku hofu ikiongezeka kuhusu kuongezeka kwa kasi kwa mzozo wa kibinadamu.

  Watu kadhaa mjini Afar wameiambia BBC kuwa wassi wa TPLF wamewaua raia.

  Madai haya hayajathibitishwa

  BBC pia imesikia ripoti za kuwepo kwa mashambulizi ya anga yaliyolenga maeneo ya waasi wa TPLF mjini Afar siku chache zilizopita.

  TPLF wanapambana na jeshi la Ethiopia na washirika wake mjini Afar, mji ulio kwenye mpaka na Tigray . Msemaji wa Afar amesema wapiganaji wa Tigray waliteka wilaya tatu mjini humo wiki hii.

  Wanaharakati wa mjini Afar wamesema kunahitajika chakula,maji na malazi ya dharura.

 5. Hospitali ya KCMC yazidiwa na idadi ya wagonjwa wanaohitaji Oksijeni

  oksijeni

  Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC imezidiwa na idadi ya wagonjwa wanaohitaji hewa ya Oksijeni ukilinganisha na mitungi 400 inayozalishwa kwa siku huku mgonjwa mmoja akitumia mitungi 8 hadi 10 kwa siku.

  Hayo yamesemwa leo Ijumaa Julai 23 na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali hiyo, Profesa Gilleard Masenga wakati akizungumza na Mwananchi Digital.

  Profesa Masenga amesema kwa siku inatumika mitungi ya Oksijeni zaidi 400 ukilinganisha na uzalishaji wake kwa siku ambayo ina uwezo wa kuzalisha mitungi 400.

  "Kwa siku mgonjwa mmoja anatumia mitungi 8 hadi 10 hili tatizo ni kubwa na wananchi msilichukulie kimzaha mzaha ni ugonjwa hatari sana, tuendelee kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na Wizara ya Afya," amesema Profesa Masenga na kuongeza,

  "Tuna kiwanda hapa KCMC cha kuzalisha mitungi 400 kwa saa 24 na mtambo huu Mungu alitusaidia tukauweka mwaka jana na tuliona hili litatusaidia kwa miaka 20 bila kuwa na shida ya Oksijeni,"

  "Matumizi yetu kwa siku yalikuwa ni mitungi 50 hadi 60 lakini ilipofika mwezi wa tatu mwaka jana kwenye wimbi la kwanza la corona tuliona umuhimu wake,"Mwananchi Digital ilimnukuu Profesa Masenga.

  Katika hatua nyingine hapo jana, serikali ya Tanzania imepiga marufuku shughuli zote za misongamano yote isiyo ya lazima, ikionesha kutorodhishwa na hali ilivyo katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo katika kuchukua hatua za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

  Wizara ya Afya imesema Hali hii imeendelea kuchangia kuongezeka kwa maambukizi na kufanya idadi ya wagonjwa waliolazwa kuongezeka ambapo kufikia tarehe 21 Julai katika vituo vyote vya afya nchini humo kulikuwa na wagonjwa 682 waliokuwa wakiugua Covid-19.

  Halikadhalika serikali ya Tanzania imetoa wito kwa raia kujiandaa kupata huduma ya chanjo.

  Taarifa ya Wizara ya afya imesema wataalamu wa afya wamekutana kupata mafunzo tayari kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma ya chanjo dhidi ya Covid-19.

  Virusi vya Corona: Serikali ya Tanzania yaonya kuhusu wimbi la tatu la Corona

 6. Mwanariadha wa Uganda afurushwa Japan

  Olimpiki

  Mnyanyuaji uzani wa Uganda aliyetoweka katika kambi ya Olimpiki magharibi mwa Japan Ijumaa iliyopita amerejea nyumbani saa chache kabla ya kuanza rasmi kwa michezo ya Olimpiki.

  Julius Ssekitoleko alirejeshwa nyumbani leo asubuhi na kuchukuliwa na polisi muda mfupi baada ya kutua katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Entebbe.

  Mama yake mzazi, mke wake mjamzito na maafisa wengine wa serikali waliokuwa wamesafiri kumlaki hawakufanikiwa kumuona.

  Katika taarifa, Wazara ya Mambo ya Nje ilisema, "Serikali ya Uganda imejitolea kuendelea kumhudumia mwanariadha huyo ili kumsaidia atulie na kuendeleza kazi yake lakini pia kumsaidia kuelewa jinsi vitendo kama hivi vibaya havimuathiri yeye tu kama mwanariadha lakini pia wanariadha wengine katika sekta ya Michezo na taifa kwa ujumla. "

  Wakati alipotoweka katika chumba chake cha hoteli huko Izumisako mjini Osaka, Julius alikuwa hajatimiza viwango vya Olimpiki vilivyowekwa kimataifa alipofika Japan.

  Alitakiwa kurejea nyumbani Uganda katikati ya wiki hii.

  Aliacha kijikaratasi chenye ujumbe pamoja na mizigo yake akisema anataka kubaki Japan na kufanya kazi.

  Polisi wa Japan walimpata Julius katika mji wa Yokkaichi, maili 105 kutoka kambi wa wachezaji wa Olimpiki.

 7. Wanajeshi wa Rwanda wawaua wanamgambo wa kjihadi Msumbiji

  Wanajeshi kutoka nchitofauti za Afrika wanapelekwa Msumbij
  Image caption: Wanajeshi kutoka nchitofauti za Afrika wanapelekwa Msumbiji

  Vikosi vya Rwanda vilivyotumwa kusaidia kukabiliana na waasi vimewauwa wanamgambo wa kijihadi wasiopungua 30, maafisa wa usalama nchini Msumbiji wanasema.

  Maafisa hao wanasema wanajeshi walikuwa wakiifanya oparesheni ya usalama katika msitu wa karibu na mji wa bandari wa Palma walipokutana na wanamgambo hao.

  Karibu wanajeshi 1,000 wa Rwanda walipelekwa nchini Msumbiji mapema mwezi huu.

  Jumuia ya maendeleo ya mataifa ya kusini mwa Afrika (SADC) imepeleka wanajeshi wake nchini humo na vikosi vya Ureno vinasaidia kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Msumbiji.

  Karibu watu 800,000 wamefurushwa makwao kutokana na ghasia hizo zilizodumu miaka minne.

  Maelfu ya watu wameuawa na wengine wengi kukatwa vichwa.

  Soma zaidi:

 8. Kanye West ashirikiana na hasimu wake Jay-Z katika albamu yake mpya Donda.

  Wasanii wa Marekani

  Kanye West amefichua kwamba Jay-Z ni miongoni mwa wasanii walioshiriki katika albamu yake mpya alioizindua.

  West aliandaa sherehe ya albamu hiyo ya Donda -aliyoipatia jina la mamake ambaye ni marehemu katika uwanja uliofurika wa Mercedes Benz , mjini Atlanta katika jimbo la Georgia , mji aliozaliwa.

  Akivalia jaketi la rangi nyekundu , lililofanana na suruali aliyovaa na viatu vya rangi ya machungwa zote zikiwa na nembo yake, Yeezy Mogul,44 , usoni alivalia kile kilichoonekana kuwa barakoa iliotengenezwa na mpira.

  Aliingia katika ukumbi bila kusema na albamu ikaanza kuchezwa bila utangulizi rasmi kutoka kwa mtengenezaji wake.

  Wimbo wa mwisho ulimshirikisha Jay-Z, rafiki yake wa siku nyingi , mpinzani na mshirika wake.

  Mshororo mmoja wa Jay-Z ulishirikisha neno ‘’red cap’’ – akimaanisha kofia ya Kanye West ilioandikwa MAGA {‘Make America Great Again’}.

  Young Guru, mzalishaji wa muziki na muhandisi ambaye amefanya kazi na Jay-Z , alifichua kwamba mshororo huo uliongezwa dakika za mwisho , pengine akielezea kwanini sherehe hiyo ilichelewa kwa saa mbili.

  Alituma ujumbe wa twitter: ‘’HOV aliimba mshororo huo hii leo!!! Saa 10 jioni’’.

 9. Nigeria yapokea ndege sita za kupambana na waasi

  Ndege

  Nigeria imepokea ndege sita za kijeshi iliyonunua kutoka Marekani, ambazo zinatarajiwa kupiga jeki juhudi za kukabiliana na makundi kadhaa yaliyojihami.

  Ndege hizo aina ya A-29 Super Tucano zilitua katika mji wa kaskazini wa Kano siku ya Alhamisi na kupokelewa na Waziri wa Ulinzi Bashir Magashi na wakuu wengine wa kijeshi.

  Nigeria ilikuw aimeagiza ndege kadhaa za kijeshi kutoka Marekani ambazo zilichukua miaka kadhaa kuundwa.

  Ndege zingine sita zilizobakia zinatarajiwa kuwasili nchi mwezi Oktoba, Msemaji wa jeshi la anga la Nigeria Edward Gabkwet aliiambia BBC.

 10. Kamati ya Bunge Marekani yalaani kukamatwa kwa Mbowe

  Mbowe
  Image caption: Mbowe pamoja na wenzake 11 kutoka chama cha Chadema walikamatwa na polisi usiku wa kuamkia Jumatano jijini Mwanza.

  Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje kuhusu masuala ya Afrika katika bunge la wawakilishi la Marekani, Karen Bass ameelezea kusikitishwa kwake na hatua ya kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe na watu wengine 11.

  Karen amesema Tanzania inapaswa "kukomesha ukandamizaji wa vyama vya upinzani na viongozi wake."

  "Mamlaka za Tanzania lazima zikomeshe ukandamizaji unaozidi kuongezeka dhidi ya vyama vya upinzani na viongozi wake. Kukamatwa kiholela na kuzuiliwa kwao kunaonyesha kupuuzwa utawala wa sheria, haki za binadamu, na haki za uhuru wa kujieleza na kushirikiana.

  Wale waliokamatwa hawajashtakiwa kwa kosa lolote la jinai.’’ alisema katika taarifa yake.

  Tamko hili linakuja wakati mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yakishinikiza kuachiliwa huru kwa Mbowe na wenzake.

  Bw. Mbowe pamoja na wenzake 11 kutoka chama cha Chadema walikamatwa na polisi usiku wa kuamkia Jumatano jijini Mwanza.

  Polisi nchini Tanzania mesema Mwenyekiti huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kuua viongozi wa Serikali.

  Soma zaidi:

  Kiongozi wa Upinzani Tanzania, Mbowe atuhumiwa kwa kula njama ya kuua viongozi wa Serikali