Nchi ya Tanzania ni mojawapo ya 'uumbaji' uliofanywa na mwanadamu. Miaka 100 iliyopita, eneo ambalo leo nchi hiyo ipo lilikuwepo lakini jina hilo halikuwepo. Wakati Watanzania wakijiandaa kutimiza miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9 mwaka huu -ni wakati mzuri sasa kutazama ni mambo ambayo yameifanya Tanzania kuwa hivi ilivyo leo.
Habari za moja kwa moja
Na Lizzy Masinga
time_stated_uk
Tunakomea hapo kwa leo. Tukutane tena Jumatatu ijayo katika matangazo mengine ya moja kwa moja.
Julian Assange anaweza kurejeshwa Marekani, mahakama yaamua
Mwanzilishi wa Wikileaks Julian Assange anaweza kurejeshwa Marekani kutoka Uingereza, Mahakama Kuu imeamua.
Marekani ilishinda rufaa yake dhidi ya uamuzi wa Januari wa mahakama ya Uingereza kwamba hangeweza kurejeshwa kwa sababu ya hofu kuhusu afya yake ya akili.
Majaji walitulizwa na ahadi za Marekani za kupunguza hatari ya kujiua. Mchumba wake amesema wanakusudia kukata rufaa.
Bw Assange anasakwa nchini Marekani kutokana na uchapishaji wa maelfu ya hati za siri mwaka wa 2010 na 2011.
Majaji wakuu walipata jaji wa ngazi ya chini alikuwa ametoa uamuzi wake wa Januari kwa kuzingatia hatari ya Bw Assange kuzuiliwa katika mazingira ya vikwazo vya hali ya juu iwapo atarudishwa nyumbani.
Hata hivyo, mamlaka ya Marekani baadaye ilitoa hakikisho kwamba hatakabiliwa na hatua hizo kali.
Marekani yamwekea vikwazo vya usafiri Isabel dos Santos
Marekani imemwekea vikwazo vya usafiri Isabel dos Santos, ambaye amekuwa akitajwa kuwa mwanamke tajiri barani Afrika, "kutokana na kuhusika kwake katika ufisadi mkubwa na ufuja fedha za umma kwa manufaa yake binafsi", taarifa kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken inasema.
Jina lake liko kwenye orodha ya watu wengine duniani wanaotuhumiwa kwa ufisadi ambao wanakabiliwa na vikwazo vya Marekani.
Lilitolewa kama sehemu ya harakati ya serikali ya Marekani ya kupambana na rushwa.
Bi Dos Santos ni bintiye rais wa zamani wa Angola, José Eduardo dos Santos, ambaye aliondoka madarakani mwaka wa 2017. Alipokuwa rais, alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya mafuta ya serikali.
Taarifa ya Bw Blinken haielezi kwa kina kuhusu kile Bi Dos Santos anatuhumiwa kufanya.
Mwaka jana, BBC iliripoti kwamba nyaraka zilizovuja zilifichua jinsi alivyojipatia utajiri kupitia madai ya ufisadi.
Alipata mikataba ya faida inayohusisha ardhi, mafuta, almasi na mawasiliano ya simu wakati babake alipokuwa rais wa Angola.
Hati hizo zilionyesha jinsi yeye na mumewe waliruhusiwa kununua mali ya serikali yenye thamani kupitia msururu wa mikataba ya kutiliwa shaka.
Wakati huo, Bi Dos Santos alisema madai dhidi yake yalikuwa ya uwongo na kwamba yalichochewa kisiasa na serikali ya Angola.
Isabel dos Santos: Mwanamke tajiri zaidi Afrika 'aliipora Angola'
Raila Odinga:‘Nitagombea urais Kenya 2022’
Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga ametangaza kwamba atagombea urais katika uchaguzi mkuu ujao nchini humo mwaka wa 2022.
Alitoa tangazo hilo katika kongamano la Azimio la Umoja siku ya Ijumaa.
"Ninatangaza kwamba ninakubali kujiwasilisha kama mgombeaji urais," Raila alisema.
Alizindua vuguvugu la Azimio la Umoja, ambalo alisema litakuwa muungano.
Kiongozi huyo wa chama cha ODM alisema hivi karibuni atatoa manifesto yake.
Raila alisema maafikiano yake na Rais Uhuru Kenyatta sio yenye nia ya kujitajirisha.
Alisema kuwa hatawahi kuuliza chochote kutoka kwa mwafaka huo isipokuwa kwa nafasi ya kutumikia.
“Lazima niongeze hapa kwamba kwa maridhiano haya, siombi chochote na kamwe sitaomba chochote isipokuwa nafasi ya kutumikia,” alisema.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kuwa kuleta amani si biashara ya kujitajirisha, bali ni wito kutoka kwa Mungu.
Tanzania yateketeza silaha 5,230 haramu
Eagan Salla
BBC Swahili, Dar es Salaam
Tanzania imeteketeza silaha haramu 5230 ikiwa ni moja ya kipengele kwenye maazimi ya Nairobi juu ya udhibiti wa silaha ndogo na nyepesi.
Kwa mujibu wa kamishna wa polisi msaidizi Renalda Milanzi ambaye ni mkuu wa kitengo cha udhibiti wa silaha na utoaji wa vibali vya silaha Tanzania, silaha haramu zilizoteketezwa zimepatikana kutokana na operesheni jeshi la polisi za kukabiliana na uhalifu.
Kamishena Milanzi amesema yoyote atakayepatikana na silaha haramu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Asilimia 71.2 ya silaha zilizo teketezwa ni magobore ambayo yamekuwa yakitumika kwenye uwindaji haramu wa wanyama pori.
Mara ya mwisho zoezi kama hili lilifanyika mkoani kigoma mwaka 2018.
Zoezi hili hudhuriwa na katibu mtendaji wa RECSA ambao ni wadhibiti na wasimamizi wa silaha ndogo na nyepesi Afrika mashariki luteni jenerali Badreldin Elamin ambaye amesema anaipongeza Tanzania kwa kufanya zoezi hili kwa uwazi kwani hakuna asiyejua madhara ya silaha haramu kuzagaa mtaani.
Kenya na Tanzania zaondoa vikwazo 46 vya kibiashara kati ya 64
Veronica Mapunda
BBC Dar es Salaam
Nchi za Tanzania na Kenya zimefanikiwa kuondoa jumla ya vikwazo 46 vya biashara kati ya 64 vilivyokuwa vinaikabili nchini hizo tangu walipokutana nchini Kenya May 4, 2021.
Hatua hiyo imeongeza uagizaji wa bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine ambapo Kenya imeagiza bidhaa Tanzania zaidi ya mara tatu ukilinganisha na mwaka uliopita 2020.
Hayo yamejidhihirisha leo katika mazungumzo maalumu yaliyofanyika ikulu ya Tanzania kati ya rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
"Tulipokutana tulikuwa na vikwazo vingi vya biashara lakini tukasema kwa kutumia majina yetu la kwake Uhuru tukasema sasa ni uhuru wa kufanya biashara Kenya au Tanzania na la kwangu suluhu tukasema sasa tutafute suluhu ya changamoto zinazotukabili" alisema.
Rais Samia Suluhu wa Tanzania Lakini licha ya kupunguza vikwazo hivyo Rais Samia anasema kuwa bado kuna changamoto hivyo anatoa wito kwa mawaziri wa biashara kuendelea kujadili changamoto zilizobaki ili kukuza biashara baina ya nchi hzio.
Biashara baina ya nchi hizo imekuwa kutoka bilioni 885 mpaka trilioni 1.1 ukulinganisha na mwaka 2020.
Katika mazungumzo hayo baadhi ya makubaliano waliyoafikiana ni pamoja na kushirikiana katika sekta ya utalii na kuwataka Mawaziri wazungumze juu ya changamoto zilizopo ili nchi zote mbili zifaidike kuleta watalii wengi.
Katika kuimarisha uhusiano katika masuala ya utalii wa nchi hizo rais Samia anasema Kenya wana ndege wachache aina ya Korongo ambao wapo Tanzania hivyo waliomba ndege hao wakae kwenye mbuga zao.
"Leo hii nina furaha kumkabidhi muheshimiwa rais cheti maalumu cha ndege hawa 20 kuwapeleka Kenya wakae katika mbuga za wenzetu, hii ndio zawadi yetu ya Krismasi Kenya lakini na mimi nikamwambia kwenye mbuga zangu nina madume wawili tu wa faru hawana wake, sisi tupo tayari kutoa mahari" alisema rais Samia.
Wasafiri wote kwenda Ghana wanahitaji kupewa chanjo
Serikali ya Ghana imesema kuanzia usiku wa manane siku ya Jumapili wageni wote wanaotembelea nchi hiyo wanahitaji kupewa chanjo kamili dhidi ya Covid 19 kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini humo.
Raia wa Ghana ambao wana nia ya kurejea nchini katika wiki mbili zijazo hawaruhusiwi, lakini watapewa chanjo watakapowasili, taarifa kutoka kwa huduma ya afya ya nchi hiyo inasema.
"Waghana wote wanaosafiri nje ya nchi wanapaswa kupewa chanjo kamili," taarifa hiyo inaongeza.
Agizo hilo ni sehemu ya hatua za kusaidia kudhibiti kuenea kwa aina mpya ya kirusi cha Covid19, Omicron
Taarifa ya huduma ya afya inasema kwamba visa vingi vya kirusi hicho nchini vilitoka kwa watu waliofika katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Accra - na wengi wa watu hao walikuwa hawajachanjwa.
Ghana imerekodi zaidi ya visa 130,000 vya Covid 19 kwa jumla na vifo 1,200.
Ada za shule huchukua sehemu kubwa ya mapato ya familia za Kiafrika - UN
Familia katika nchi za Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinatumia sehemu kubwa ya mapato kusomesha watoto wao, huku wengi wao wakifungiwa nje ya elimu bora kwa sababu ya gharama ya juu, ripoti mpya kutoka kwa bodi ya elimu ya Umoja wa Mataifa, Unesco, inasema.
Nchini Ghana, kwa mfano, wastani wa 13% ya matumizi ya familia huenda shuleni.
Kwa ujumla katika Ukanda wa kusini mwa Sahara karibu asilimia 40 ya fedha zinazotumika katika elimu zinatoka kwa familia, badala ya vyanzo vingine kama vile serikali.
Katika ripoti yake ya hivi punde ya Global Education Monitoring (GEM) iliyotolewa Ijumaa, Unesco inasema kuna hatari inayoongezeka ya ukosefu wa usawa na kutengwa katika kutoa elimu.
Manos Antoninis, mkurugenzi wa ripoti hiyo, anasema athari za Covid-19 zimebana bajeti za familia zaidi, na kufanya ada za shule na gharama zingine zishindwe kumudu kwa wengi.
Ripoti hiyo inaonya kuwa 8% ya familia katika nchi za kipato cha chini na cha kati zinalazimika kukopa pesa ili kuwalipia watoto wao kwenda shule.
Kiwango hicho ni cha juu zaidi katika nchi kama Uganda na Kenya ambapo thuluthi moja ya familia zote wanapaswa kuchukua mikopo ili kulipa karo ya shule.
Unesco inazitaka serikali kujitolea zaidi kutoa miaka 12 ya elimu bora bila malipo kwa watu wote, kwa ajili ya maskini ambao hawawezi kumudu elimu katika shule binafsi
Raila Odinga kutangaza iwapo atawania urais 2022
Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga hii leo anatarajiwa kuzindua azma yake ya urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Raila ambaye atakuwa anawania wadhfa huo kwa mara ya tano, anatarajiwa kutoa uamuzi wake iwapo atajibwaga katika kinyanganyiro hicho katika sherehe kubwa inayofanyika katika uwanja wa Kasarani.
Baadhi ya viongozi wa kimataifa wakiwemo wale walioteuliwa humu nchini wanatarajiwa kushiriki katika hafla hiyo itakayoshuhudiwa na maelfu ya Wakenya waliosafiri hapo jana kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Azma ya Raila kutangaza kuhusu kuwania uchaguzi inajiri baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi na wafanyabiashara wa eneo la mlima Kenya – eneo ambalo rais Uhuru Kenyatta anatoka.
Hatahivyo baadhi ya viongozi walioshirikiana naye katika muungano wa Nasa katika uchaguzi mkuu uliopita huenda wasihudhurie hafla hiyo licha ya kualikwa.
Huku baadhi yao wakitofautiana naye kisiasa , wengine wamejipata katika shughuli za kitaifa katika mataifa ya kigeni.
Hii leo kuanzia mwendo wa saa moja uwanja wa kitiafa wa kasarani jijini Nairobi umekuwa eneo la shughuli nyingi baada ya wafuasi wa chama cha ODM nchini Kenya kuwasili katika uwanja huo tayari kwa mkutano huo wa Azimio la Umoja.
Makumi ya wafungwa watoroka gerezani DR Congo
Makumi ya wafungwa kutoka gereza la Boma magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wametoroka.
Wafungwa hao walitumia fursa ya muziki wa sauti ya juu uliokuwa ukipigwa katika eneo la mazishi ili kuwavuruga walinzi.
Wafungwa tisa walikamatwa karibu na gereza hilo na mmoja kujeruhiwa wakati walinzi wakifyatua risasi hewani, Radio Okapi iliripoti.
Wafungwa wengine 19 bado wako hawajapatikana, kulingana na redio hiyo. Gereza la Boma hapo awali lilikuwa na matukio ya utoro wa wafungwa.
Wenyeji wanasema gereza hilo linahitaji kufanyiwa marekebisho kama lilijengwa miaka ya 1900.
Jussie Smollett: Mwigizaji apatikana na hatia ya kusema uwongo kuwa alishambuliwa
Muigizaji wa Marekani Jussie Smollett alidanganya polisi alipodai kuwa mwathiriwa wa shambulio la ubaguzi wa rangi, chuki ya watu wa mapenzi ya jinsia moja, mahakama ya Chicago imebaini.
Katika kesi wiki hii, Smollett, 39, alisimama na kukanusha kwamba aliandaa shambulio la uwongo dhidi yake mwenyewe.
Alipatikana na hatia siku ya Alhamisi ya makosa matano ya kufanya fujo. Kila hesabu ina adhabu ya hadi miaka mitatu jela.
Kwa kuzingatia makosa ya Smollett na hatia za hapo awali, wataalam wamesema kuna uwezekano wa kutolewa hukumu nyepesi au kuachiwa kwa masharti.
Tarehe ya hukumu bado haijapangwa.
Mahakama ilifikia uamuzi wake siku moja baada ya mashauri kuanza.
Kesi hiyo ilitokana na kisa cha karibu miaka mitatu iliyopita, mnamo Januari 2019, wakati nyota huyo wa zamani wa kipindi cha televisheni cha Empire alipowaambia polisi kuwa alikuwa mwathirika wa shambulio.
Smollett, ambaye ni mweusi na anajihusisha na mapenzi ya jinsi moja, aliwaambia polisi kwamba alivamiwa na washambuliaji wawili ambao walipiga kelele, wakammwagia " kemikali" na kumfunga kamba shingoni alipokuwa akitembea usiku wa manane. Chicago.
Mamlaka ilianzisha uchunguzi kuhusu shambulio hilo, lakini mnamo Februari mwaka huo, polisi walimshtaki Smollett kwa kuwasilisha ripoti ya uwongo kwa polisi, akidai kuwa alifanya shambulio hilo.
Alikabiliwa na jumla ya mashtaka sita, kila moja likirejelea matukio tofauti ambapo alituhumiwa kuwadanganya polisi.
Alipatikana na hatia katika mashtaka matano kati ya sita, ikimaanisha kuwa la mwisho lilikuwa halijathibitishwa mahakamani.
Waumini 16 wauawa na watu wenye silaha nchini Nigeria
Watu wenye silaha katika jimbo la Niger nchini Nigeria wamewaua kwa risasi waumini 16 waliokuwa kwenye msikiti mmoja.
Baadhi ya watu wengine wamejeruhiwa katika shambulizi katika kijiji cha Ba’are eneo la Mashegu.
Washambuliaji waliwafyatulia risasi waumini wa Kiislamu wakati wa sala ya asubuhi ya Jumatano, afisa wa serikali ya jimbo la Niger, Ahmed Ibrahim Matane, aliiambia BBC.
Alisema wapiganaji hao waliokuwa wakiendesha pikipiki pia walimpiga risasi na kumuua mtu mwingine mmoja barabarani walipokuwa wakitoka nje.
Katika jimbo jirani la Katsina, kundi jingine la watu wenye silaha wamempiga risasi afisa mkuu wa serikali katika makazi yake.
Polisi wanasema wanachunguza mauaji ya Rabe Nasir, kamishna wa serikali wa sayansi na teknolojia.
Mkoa huo unakabiliwa na wimbi la utekaji nyara kwa ajili ya fidia na mauaji yanayofanywa na magenge ya wahalifu wenye silaha.
Mapema wiki hii, wasafiri wasiopungua 23 walivamiwa na watu wenye silaha na kuteketezwa hadi kufa ndani ya basi katika jimbo la Sokoto.
Nigeria ni miongoni mwa nchi zilizo hatari ulimwenguni kwa wanawake kuishi
Kifaa cha kusaidia kujiua chazua utata Uswizi
Mtengenezaji wa kifaa cha kujiua alisema ana uhakika kinaweza kutumika nchini Uswizi kuanzia mwaka ujao.
Sarco iliomba ushauri wa mtaalamu wa sheria, na akaihakikishia kuwa kifaa hicho hakikiuki sheria za Uswizi.
Lakini wanasheria wengine walihoji usahihi wa msimamo wake. Shirika la Dignitas, ambalo linahusika na suala la kusaidiwa kujiua, lilisema hakuna uwezekano kuwa kifaa hicho "kukubalika kwa kiasi kikubwa". Kujiua kwa kusaidiwa ni halali nchini Uswizi. Na watu 1,300 walikufa, kwa njia hiyo mnamo 2020.
Mkanganyiko wa kisheria
Njia inayotumika kwa sasa Uswizi ni kumpa mtu anayetaka kujiua majimaji, yakimeng'enywa maisha yake yataisha.
"Vidonge vya kujiua" vinaweza kuwekwa popote, vimejaa nitrojeni, na hupunguza haraka viwango vya oksijeni. Husababisha mtu kupoteza fahamu, na kisha kufa ndani ya dakika 10.
Kifaa kinaweza kuendeshwa kutoka ndani, na kina kitufe cha dharura cha kusaidia kutoka humo.
Sarco ilimwomba mtaalamu wa sheria Daniel Herlmann, profesa mshiriki katika Chuo Kikuu cha St. Gallen, kuthibitisha ikiwa matumizi ya kifaa cha kujitoa uhai yalikiuka sheria za Uswizi.
Aliambia BBC kuwa alidhani kifaa hicho "si kifaa cha matibabu" na kwa hivyo hakiko chini ya Sheria ya Bidhaa za Tiba.
Pia inaaminika kuwa haikiuki sheria zinazohusiana na matumizi ya nitrojeni, silaha au usalama wa bidhaa. Alihitimisha kuwa "Sheria za Uswizi hazishughulikii kifaa hiki."
"Uswizi imekuwa na sera ya kusaidiwa kujiua kwa miaka 35," Dignitas aliambia BBC. "Kwa kuzingatia matendo haya ya kitaalamu hatuwezi kufikiria kuwa kifaa cha kuokoa maisha kinaweza kukubaliwa au kuvutiwa na Uswizi."
Shindano la "Miss Camel" Saudi Arabia: ngamia 40 waondolewa kwa udanganyifu
Makumi ya ngamia hawakujumuishwa kwenye shindano la "Miss Camel Beauty" nchini Saudi Arabia kwa sababu walidungwa sindano ya Botox ili kupunguza mikunjo na kuwafanya waonekane warembo zaidi.
Shindano hili ni moja wapo ya hafla maarufu katika tamasha la ngamia la Mfalme Abdulaziz. Sifa kuu za ngamia wanaoshiriki katika shindano hilo ni pamoja na: midomo mirefu, iliyoinama, pua kubwa na nundu yenye kupendeza.
Shirika rasmi la wanahabari la Saudia (SPA) lilisema kuwa majaji katika shindano hilo walitumia teknolojia "ya hali ya juu" kugundua viboreshaji vipodozi vya ngamia kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Aliongeza kuwa ngamia wote walipelekwa kwenye ukumbi, ambapo sura na mienendo yao ilichunguzwa na wataalamu.
Vichwa vyao, shingo na kiwiliwili pia vilichunguzwa kwa kutumia X-ray na mashine ya 3D ultrasound, na sampuli zilichukuliwa kwa uchambuzi wa maumbile na vipimo vingine.
Shirika la Habari la Saudia lilisema kuwa ngamia 27 hawakujumuishwa katika shindano moja kutokana na kunyoosha sehemu za miili yao, na ngamia 16 waliokuwa wakishindana walifukuzwa kwa kupata sindano za Botox.
Waandaaji wa shindano la urembo wa ngamia walinukuliwa wakisema kwamba "wana nia ya kukomesha udanganyifu wote katika urembo wa ngamia" na kuahidi "kutoa adhabu kali kwa wadanganyifu."
Walieleza jinsi Botox ilivyodungwa kwenye midomo ya ngamia, pua, taya na sehemu nyingine za vichwa vyao ili kulegeza misuli.
Collagen pia imetumika kukuza midomo na pua, na pia homoni nyingine ili kukuza ukuaji wa misuli.
Walisema mipira pia ilitumika kwa wanyama hao kufanya sehemu za mwili kuonekana kubwa kuliko kawaida kwa kuzuia mtiririko wa damu.
Tamasha la Ngamia la Mfalme Abdulaziz ndilo kubwa zaidi la aina yake duniani.
Wamiliki wa ngamia wapatao 33,000, baadhi yao kutoka Marekani, Urusi na Ufaransa, watashiriki. Shughuli za tamasha zilianza Desemba 1 na zitadumu kwa siku 40, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja