Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa Wiki Hii

Polisi wafupi

Sheria ina mkono mrefu... Hata hivyo Ufaransa huenda ikageuza msemo huo, kwani watu wafupi sasa wanaruhusiwa kujiunga na jeshi la polisi nchini humo.

Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Ufaransa, sheria mpya imepitishwa kuhusina na urefu ambao polisi wanatakiwa kuwa nao.

Sheria hii imepitishwa katika kipindi ambacho rais Nikolas Sarkozy yuko madarakani. Rais Sarkozy, ana urefu, ama ufupi wa chini ya futi tano na nchi tano.

Kabla ya sheria hiyo kubadilishwa, kujiunga na polisi, mtu alitakiwa kuwa na urefu wa zaidi ya futi tano na nchi tano. Vyama vya wafanyakazi vya Ufaransa vimefurahishwa na hatua hiyo vikisema kuweka kipimo kunazuia kwa njia moja ama nyingine kupatikana kwa polisi wenye uwezo wa kiakili na maadili.

Rais Sarkozy huwa makini sana na urefu wake, na mara nyingi hujaribu kuhakikisha anazungukwa na watu wafupi kuliko yeye ili aonekane mrefu zaidi.

Kwa mujibu wa gazeti la Metro la hapa London, mapema mwaka huu rais huyo aliagiza kutafutiwa walinzi binafsi, yaani bodyguards - ambao wana urefu karibu na wake--, au ufupi,--- na mara nyingi huonekana akichuchumia, au akisimama juu ya vistuli vya mbao ili aongeze centimita kadhaa.

Rais huyo ambaye ni maarufu kwa kuvaa viatu vyenye soli ndefu hutaka pia mkewe, Carla Bruni ambaye urefu wake ni futi tano na nchi tisa awe anavaa viatu visivyo na kikanyagio kirefu,--yani flat shoes-- wakati wakiwa wote hadharani.

Hata hivyo kuingia kwa polisi wasio warefu sana, haina maana sheria itakuwa na mkono mfupi....

Bwana harusi

Bwana harusi mmoja nchini Uturuki amewapiga risasi na kuwaua baadhi ya wageni waalikwa katika harusi yake, akiwemo baba yake mzazi.

Katika harusi za Uturuki, ni utamaduni kwa bwana harusi kufyatua risasi hewani kama ishara ya kusherekea.

Bwana harusi huyo Tevfik Altin, aliyekuwa akivurumisha risasi kutoka kwenye bunduki aina ya AK47 alishindwa kudhibiti silaha hiyo na kummiminia risasi baba yake, pamoja na shangazi zake wawili.

Mtandao wa Thaindian news umesema watu wengine sita walijeruhiwa katika sekeseke hilo.

Kati ya waliojeruhiwa ni pamoja na watoto wenye umri wa miaka kumi hadi kumi na sita. Mkasa huo umetokea katika kijiji kidogo cha Akcagoze, kwenye eneo la kusini mashariki kwa Uturuki. Bwana harusi huyo amekamatwa na polisi.

Mtabiri ala kichapo

Mahakama moja nchini Urusi imemhukumu bwana mmoja kwenda jela kwa miaka zaidi ya ishirini, baada ya kukutwa na hatia ya kumpa kichapo mtabiri mmoja.

Bwana huyo Gennady Osipovich alikutana na mwanamama mmoja ambaye anadai ni msoma nyota na huweza kutabiri maisha ya baadaye, na kumuomba amtzamie mustakabali wake.

Mtandao wa BNO News umesema mwanamama huyo alipotazama, alimuambia bwana Osipovich kuwa anaona nyumba kubwa ya serikali ikiwa katika maisha ya baadaye ya bwana huyo. Nchini Urusi, nyumba kubwa ya serikali, maana yake ni jela.

Gazeti la Moscow Times limekaririwa likisema, baada ya kusikia utabiri huo, wa kwenda jela, alikasirishwa mno, na kuanza kumpa kipigo mtabiri huyo.

Hata hivyo mtabiri huyo alifanikiwa kuchoropoka na kukimbia, lakini bwana Osipovich aliwachoma kisu watu wawili wakati akimfukuza mwanamama huyo. Osipovich amehukumiwa kwenda jela kwa miaka ishirini na mbili.

Ghadhabu za mfungwa

Mfungwa mmoja nchini Marekani aliyeshikwa na hasira kutokana na kushindwa kuonana na padri, aliamua kutafuna na kumeza miwani ya mfungwa mwenzake.

Shirika la habari la CBS news limemkariri liwali wa wilaya ya Burleigh, huko Bismark, Meja Les Witkowski akisema mfungwa mwenye miaka arobaini na mbili amefanya kituko hicho. Amesema alipandwa na jazba na hasira pale aliposhindwa kuonana na kuzungumza na mtu anayehubiri dini kwa wafungwa wa hapo.

Mfungwa huyo alimeza kioo kimoja baada ya kingine, kati ya viwili vinavyounda miwani, na hatimaye kumalizia na kutafuna pia fremu ya chuma ya miwani hiyo na kuimeza.

Meja Witkowski amesema mfungwa huyo alikimbizwa hospitalini katika chumba cha dharura, lakini hata hivyo alirejeshwa jela, baada ya madaktari kufanya tathmini na kuona hakupata madhara yoyote. Miwani hiyo ilikuwa na thamani ya dola mia mbili na hamsini. Mamlaka za huo zinafikiria kumfungulia mashitaka ya uhalifu utukutu (criminal mischief). Mfungwa huyo.

Watoto kwa mpigo

Kinadada wanne wa familia moja nchini Marekani, kila mmoja amejifungua mtoto mmoja katika kipindi cha siku nne.

Kina dada watatu kati ya hao walisaidiwa kujifungua na mkunga huyo huyo katika hospitali moja mjini Chicago siku ya Ijumaa na Jumamosi, huku mdada wa nne akijifungua mwanaye siku ya Jumatatu mjini California.

Wanafamilia wa familia hiyo wamesema wala hawakupanga jambo hilo. Mkunga aliyesaidia kujifungua kwa kinadada watatu, Dokta Jean Alexandre amesema "Si jambo la kawaida, lakini ni jambo jema". "Tumeshitushwa na pia kushangazwa",amesema mmoja wa waume wa kinamama hao. Watoto wote wanne wamezaliwa wakiwa na afya njema kabisa. Bila shaka watakuwa wakiwaza, je sherehe za kuadhimisha kuzaliwa kwao, zitafanywa kila mmoja peke yake na kufuatana kwa siku nne mfululizo, au watafanya moja tu kwa watoto wote wanne??

Na kwa taarifa yako..... Binaadamu hawezi kujitekenya mwenyewe.

Tukutane wiki ijayo... panapo majaaliwa.