Everton yaibana Manchester United 3-3

Everton walifanya mashambulizi ya kufa na kupona katika dakika za mwisho na kufunga magoli mawili kuizuia Manchester United kupata ushindi na pointi tatu kwenye mechi iliyofanyika Goodison Park.

United walionekana kupata ushindi bila mshambuliaji Wayne Rooney, ambaye katika mechi hiyo ya 700 kwa Sir Alex Ferguson, alipumzishwa kutokana na matatizo ya kifamilia ambayo bado anaendelea kujaribu kuyatatua.

Lakini walijisahau kufunga milango na matokeo yake wakachapwa mawili ya haraka haraka kabla ya filimbi ya mwisho.

Wakiwa 3-1, Everton walijipanga vyema na kufunga kutokana mpira wa kichwa wa Tim Cahill, kabla ya Mikel Arteta kuchana nyavu hali iliyoamsha shamra shamra kwa mashabiki wa Everton kwa kupata sare ambayo ni sawa na ushindi.

Wafungaji

Everton 3-3 Man Utd Mwisho
(Mapumziko: 1-1)
Pienaar 39Cahill 90+1Arteta 90+2 Fletcher 43Vidic 47Berbatov 66