Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Watoto kwenda bar

Image caption Waziri Dermot Ahern

Polisi nchini Ireland, wanafanya mipango ya kutuma vijana wadogo kwenda baa na kuagiza vinywaji vikali, katika mpango wa kukamata wamiliki wa baa, ambazo zinauza vinywaji vikali kwa vijana wadogo. Waziri wa sheria Dermot Ahern amesea siku ya Jumanne kuwa mpango huo utaanza mwezi ujao, kuwasaka watu wanaouza pombe kwa vijana chini ya umri wa miaka kumi na minane.

Hatua hii imekuja Kutokana na Ireland kukabiliwa na changamoto ya kuwa na utamaduni wa ulevi wa kupindukia, barani Ulaya, unaoanza kwa vijana wakiwa bado wadogo. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, polisi watakuwa na ruhusa, kwa ridhaa ya wazazi, kutuma vijana wa kati ya miaka kumi na tano hadi kumi na saba kwenda katika baa na kuagiza vinywaji vikali kama mtego.

Image caption Watoto chini ya miaka 17 hawaruhusiwi kuuziwa pombe

Iwapo baa hizo zitawahudumia watoto hao na vinywaji vikali, zitakabiliwa na adhabu ya kufungiwa, kushitakiwa na kupigwa faini. Hata hivyo waziri wa sheria amesema mpango huo utafutwa mara moja iwapo usalama wa watoto hao utakuwa mashakani kwa njia yoyote ile.

Mwizi aomba radhi

Image caption Rupia

Mwizi mmoja nchini India alikamatwa, baada ya kurejea katika nyumba aliyofanya wizi wake na kumwomba radhi mtu aliyemuibia.

Mwizi huyo, Naresh Dasri, huku akibubujikwa na machozi alimuambia Suresh Bhagwat kuwa anaona aibu sana kwa kumuibia. Mwizi huyo aliamua kujitokeza na kusema wazi kuwa ndiye aliyeiba rupia elfu themanini na sita na mia tano, ambazo ni sawa na dola elfu moja na mia tisa, ambazo ni za bwana Bhagwat.

Mwizi huyo baada ya kuomba radhi, pia alimuomba Bwana Bhagwat kumpa adhabu yeyote ile anayodhani inamfaa. Bwana Bhagwat, huku akiwa kashitushwa na mwizi wake kujisalimisha mweyewe, badala ya kumpa adhabu, aliamua kupiga simu polisi. "unajua mwanzo nilidhani huyu mtu amelewa" amesema bwana Bhagwat, "lakini baada ya kunieleza vizuri, nikaona bora niwaite polisi tu" ameongeza bwana huyo aliyeibiwa fedha zake. Gazeti la India Daily limesema mwizi huyo amefikishwa katika mahakama ya Pune, katika jimbo la magharibi la Maharashtra, na hukumu yake ilikuwa ikitarajiwa kutolewa wiki hii.

Harusi ya mbwa

Image caption Harusi ya mbwa

Kuna msemo usemao, kila mbwa ana siku yake. Na msemo huu umedhihirika, sio kwa mbwa mmoja bali wawili hapa Uingereza.

Mbwa hao ambao majina yao ni Pete na Zoe, wenye umri wa miaka mitano, wanatarajiwa kufunga ndoa hivi karibuni. Gazeti la The Sun limeripoti kuwa wawili hao wanaoishi katika nyumba ya kulelea wanyama wa mitaani, watafanya harusi yao katika ukumbi wa kituo cha wanyama cha Wood Green huko Godmanchester, Cambridgeshire.

Harusi hiyo ya aina yake itahudhuriwa na wafanyakazi wa kituo hicho, wananchi wa kawaida na marafiki wa karibu wa mbwa hao, ambao pia ni mbwa. Ndoa hiyo itafungishwa na Kasisi Gael Lees wa kitengo cha kulelea paka cha hapo Wood Green, ambaye atasoma ahadi maalum zilizoandikwa kwa ajili ya mbwa hao.

Baada ya harusi hiyo, mbwa harusi hao watarejeshwa katika makazi yao na kupatiwa keki yenye ngazi tatu iliyotengenezwa kwa maini ya ngombe, na bakuli la maji. Bwana harusi wa mbwa, bila shaka ataitwa.. Mbwana harusi, bibi harusi je..??

Ombaomba tajiri

Image caption Dubai

Polisi huko Dubai wamegundua hivi karibuni kuwa kazi ya ombaomba katika mitaa ya mjini Dubai ina malipo makubwa mno. Omba omba mmoja kutoka nchi ya Asia, aliyekamatwa hivi karibuni kwa makosa ya kuomba pesa mitaani, alikutwa akiishi katika hoteli ya kifahari yenye hadhi ya nyota tano, yaani five star hotel.

Kwa mujibu wa Gazeti la Khaleej Times la Dubai, mkurugenzi wa usalama wa watalii wa Dubai Meja Mohammed Rashid Al Muhairi aliwaambia polisi kuhusu maisha ya kifahari ya omba omba huyo, ingawa haikutajwa anatoka katika nchi gani ya Asia.

Meja Mohammed Rashid Al Muhairi amesema mtu huyo siku za awali aliwahi kutimuliwa kutoka Dubai na kurejeshwa nchini mwake, lakini alirejea kimyakimya kutokana na mapato makubwa aliyokuwa akiyapata kwa kuomba omba mitaani.

Meja Al Muhairi ameongeza kuwa omba omba wapatao mia tatu na sitini wamekamatwa mjini Dubai wakati wa mwezi wa Ramadhani na baada ya sikukuu ya Eid mwaka huu. Amesema wengi wa waliokamatwa kwa makosa ya kuomba omba sio raia wa Dubai na wanaishi huko kwa visa za muda mfupi huku raia wa Asia wakiongoza orodha hiyo, wakifuatiwa na waarabu.

Jogoo mtemi

Jogoo aliyekuwa akiwatesa wakazi wa Newcastle hapa Uingereza hatimaye ametiwa mbaroni.

Image caption Jogoo mtemi

Kwa muda wa wiki tatu, jogoo huyo aliyepachikwa jina la Chookzilla alikuwa akianza kuwika zaa tisa za usiku na kuamsha watu, na mchana akiwatisha na kuwafukuza watoto wadogo katika mitaa ya kitongoji cha New Lambton. "Alikuwa akimkimbiza mtoto wangu wa kike, na hata kumtisha rafiki yangu aliyekuja kinisalimia" amesema Gloria Smith, mwanamama mkazi wa huko.

"Niliita mafariki zangu waje kumkamata, lakini hakuna aliyeweza kufanya hivyo, mpaka nilifikiri labda ni jini" ameongeza Bi Gloria akizungumza na gazeti la Telegraph. Binti wa miaka kumi na minne wa Bi Gloria, aitwaye Rachel alimpachika jina la 'Jogoo muovu' na alikuwa na furaha sana baada ya jogoo huko kukamatwa na maafisa wa baraza la mji.

Image caption Labda akichinjwa na kupikwa atakuwa hivi

Jogoo huyo mwenye rangi nyeusi na nyekundu pia alikuwa na tabia ya kumkimbiza mkazi mwingine Sally Lambaco, kila mara anaposhuka kwenye basi akitoka kazini. Hata hivyo siku ya kukamatwa kwake pia haikuwa kazi rahisi kwani aliwasumbua sana maafisa wa mji, ingawa baadaye alitiwa kwenye wavu.

Jogoo huyo amepelekwa katika ofisi za mji wa Newcastle na huenda akachinjwa iwapo mmiliki wake hatojitokeza haraka. Hata hivyo Bi Gloria amesema mahala panapomfaa zaidi jogoo huyo, ni kufanywa mchuzi tu.

Nani alisema Jogoo wa shamba hawiki mjini....

Na kwa taarifa yako........Duniani kuna kuku wengi zaidi kuliko binaadam.

Tukutane wiki ijayo... Panapo Majaaliwa......

Habari zimekusanywa kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao.