Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

MREMBO WA PLASTIC 2010

Image caption Warembo wa plastic

Michuano ya kumsaka mrembo bora wa mwaka huu yanafanyika mjini Budapest nchuni Hungary. Hata hivyo mashindano haya si kama yale ya kawaida ya kutafuta mlimbwende. Vigezo katika mashindano hayo, ni kuwa wakinadada lazima wawe na viungo feki, au vya plastiki.

Shindano lenyewe linaitwa Miss Plastic mwaka 2010.

Maziwa ya kupachika, pua zilizonyooshwa na nyuso zilizoinuliwa, ndio vigezo kwa warembo kushiriki.

Mchuano mkali

Majaji katika shindano hilo wanasema mchuano ni mkali baina ya washiriki ishirini na wawili wanaowania taji hilo la taifa. Wasichana wanahitajika kuonesha vyeti vya hospitali kuthibitisha kuwa wamefanyia marekebisho maeneo na viungo mbalimbali vya miili yao. Yaani plastic surgery.

Image caption Wa kuchonga

Majaji watatoa pointi kwanza kwa uzuri wao wa asili, na baadaye kuongeza pointi katika uzuri ambao umeongezwa au kurekebishwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuongeza nakshi mwilini. Mshindi katika shindano hili, atakwenda kupambana na washindi kutoka nchi nyingine, ili kupata mrembo wa dunia wa plastiki.

Mshiriki Timea Kertesz, mwenye umri wa miaka 27, ambaye amepachika maziwa na kufania marekebisho makalio yake amesema alianza kujitengeneza tangu akiwa na miaka 17.

Image caption Mambo fulani....

"Nilimshawishi mama yangu kunipeleka hospitali ili kurekebisha masikio yangu yaliyokuwa yamejitokeza sana" amesema mlimbwende huyo " Na tangu hapo, nimekuwa najiamini zaidi na sijaacha kufanyia marekebisho mahala ambapo naona kidogo palikosewa kuumbwa".

Urembo wa dukani.... Uzuri si lazima kuzaliwa nao...?

PADRE 'MCHEMSHO'

Padre wa kanisa la England -- Church of England, la hapa Uingereza, ambaye alibashiri kuwa ndoa ya mwana mfalme William na Kate Middleton haitadumu zaidi ya miaka saba, amesimamishwa kuhudumu kanisani.

Image caption Kasisi mstaafu

Padre huyo wa Willesden, Kasisi mstaafu Pete Broadbent alitoa matamshi hayo baada ya Prince William kutangaza anataka kufunga ndoa na Bi Kate, wiki iliyopita.

Matamshi hayo aliyatoa kupitia mtandao, pia yalisema familia ya kifalme imejaa ndoa zilizovunjika na uhusiano wa nje ya ndoa, na kuonesha kusikitishwa kwake kuwa harusi hiyo itagharimu fedha nyingi za wananchi.

Shirika la habari la Reuters limesema, licha ya padre huyo kuomba radhi kutokana na matamshi yake hayo, pandre huyo alisimamishwa kazi siku ya Jumanne. Kiongozi wa padre huyo, Padre wa London kasisi mstaafu Richartd Chartes ni rafiki wa karibu wa mwana mfalme William, na kuna tetesi kuwa huenda ndiye atakayefungisha ndoa hiyo ya kifalme.

Image caption 'Madudu' aliyoandikwa Facebook

Padre Broadbent aliandika maneno hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook, mara tu baada ya harusi hiyo kutangazwa. Waswahili husema, ulimi uliponza kichwa ... Lakini siku hizi wanamtandao wanasema Jihadhari na maneno unayoyaandika kwenye Facebook... Kwani yanaweza pia kuponza.... kichwa?

Harusi ya Prince William na mchumba wake Kate Middleton itafanyika Aprili 29 hapa London, na huenda ikawa siku ya mapumziko, ili sote tusherekee...

Image caption Itakuwa harusi ya kukata na shoka.. nyote mnaalikwa

DAWA YA MINYOO

Mfugaji mmoja nchini Ufaransa amejikuta matatani kufuatia kutumia utaalam wake mpya wa kupambana na minyoo waliokuwa wakisumbua bata wake.

Image caption Msokoto wa bangi.. lakini hautibu minyoo

Mtandao wa Thaindia News umedai kuwa mfugaji huyo Michel Rouyer aliwapa bata wake bangi, ili kuwalevya minyoo walipo tumboni mwa bata hao.

Akijitetea mfugaji huyo amesema baada ya kuwapa tiba hiyo, hivi sasa bata wake wapo katika hali nzuri kabisa na hawana tatizo la minyoo tena.

Image caption Bata kama huyu kapewa bangi

Baada ya kufikishwa mahakamani alikutwa na hatia na kupewa kifungo cha nje na faini ya Euro mia tano. Imeelezwa kuwa polisi walipovamia nyumba yake kufanya upekuzi walikuta miche kumi na miwili ya bangi na karibu kilo tano za majani ya bangi, zikiwa zimefichwa nyumbani kwake.

Alipoulizwa, alisema, ndiyo, huwa anavuta bangi hiyo kidogo, lakini zaidi ni ya kuwaponya bata wake kutokana na minyoo.

Image caption Miche kadhaa

"hakuna dawa nzuri kama hii, nawaambia" aliwaambia polisi.

Hata hivyo jaji mahakamani hakuamini neno lake hata moja. Polisi nao walisema hawajawahi kusikia bangi kuweza kutibu minyoo.

SADAKA HAIIBIWI

Mwizi mmoja aliyejaribu kutaka kuiba fedha za sadaka kanisani nchini Ujerumani, ameangukiwa na moja ya sanamu kanisani humo na kujeruhiwa.

Image caption Sanamu kama hili

Mwizi huyo alikuwa akilinyatia boksi la kuwekea sadaka na ghafla sanamu lenye ukubwa wa binadam likaanguka, na kumchana kichwani.

Mtandao wa kijerumani uitwao The Local umesema sanamu hilo ni la Mtakatifu Antonius, na lilimuangukia mwizi huyo, wakati akijaribu kuvunja boksi la sadaka ambalo lilikuwa limeunganishwa na sanamu. "Nadhani mtakatifu Antonius hakutaka sadaka iibiwe," amesema pande wa kanisa hilo Ludwig Sperrer, huku akitabasamu.

Image caption Sadaka

Mwizi huyo baadaye alikwenda katika nyumba iliyo jirani na kanisa hilo kuomba msaada wa kuzuia damu isiendelee kumwagika kutoka kichwani mwake. Hata hivyo bahati haikuwa yake mwizi huyo, kwani wakati akifungwa kidonda chake, mtu mwingine alimuibia mwizi huyo pochi yake.

Na kwa Taarifa yako........

Panya anaweza kishi muda mrefu zaidi bila kunywa maji, kuliko hata ngamia.

Tukutane Wiki Ijayo... Panapo Majaliwa.....

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali.