Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

NYOKA KITANDANI

Haki miliki ya picha AP
Image caption Uso kwa uso na nyoka

Msichana mmoja nchini Poland aliyekuwa amelala, aliota kuwa anakumbatiana na mpenzi wake, na alipozinduka, alikuta amekumbatia nyoka.

Msichana huyo Iga Radkiewicz wa mjini Krakow, Poland, amesema aliruka kutoka kitandani huku akitetemeka. "Nilikuwa naota njozi murua kuhusu mimi na mwanaume wangu, lakini niliposhituka, nikakuta naangaliana macho kwa macho na bonge la nyoka" amesema Iga.

"Kidogo nife kwa hofu" amesema msichana huyo mwenye umri wa miaka 19, akikaririwa na gazeti la Croatian Times. Wataalam wa nyoka walimkamata nyoka huyo, ambaye hata hivyo imeelezwa kuwa sio nyoka hatari na wala hana madhara yoyote.

Msemaji wa polisi amesema nyoka huyo alitoroka kutoka katika duka moja la kuuzia wanyama wa kufuga, na alikuwa akitafuta joto tu.

WEVI WASAHAULIFU

Image caption Usisahau mafuta

Wezi wawili, wanawake hapa Uingereza waliingia katika duka moja na kuiba pombe, lakini wakasahau kuweka mafuta ndani ya gari walilotumia kubebea mali waliyoiba.

Kinamama hao Devlin mwenye miaka 59 na mwenzake Egan mwenye miaka 52 walionekana wakiiba pombe yenye thamani ya karibu dola elfu moja.

Hata hivyo baada ya kufanya wizi huo waliingia katika gari lao na kuondoka lakini hawakufika mbali, kwani gari hilo liliisha mafuta na kuzimika.

Wawili hao walilazimika kulisukuma gari lao hadi kwenye kituo cha mafuta na kununua mafuta na kisha kuondoka, bila kufahamu kuwa kila wanachokifanya kinarekodiwa na kamera maalum za usalama, CCTV. Gazeti la Metro limesema wawili hao wamekiri kufanya wizi katika mahakama ya Manchester.

Pombe walizoiba zilikuwa nyingi kiasi kwamba walipata tabu kufunga buti ya gari.

UZURI

Image caption Daktari feki alikuwa akimdunga sindano za simenti

Mwanamama mmoja nchini Marekani aliyetaka kuutengeneza mwili wake uwe wa kuvutia zaidi amejikuta matatani, baada ya kudungwa sindani za saruji na gundi ili kuongeza ukubwa wa makalio yake.

Mwanamke huyo ambaye hakutajwa jina kutokana na sababu za kisheria, alikuwa akitaka kufanya kazi katika klabu ya usiku, na hivyo alitafuta daktari anayeweza kumbadilisha, lakini kwa bei nafuu.

Polisi wamesema mwanamke huyo alikutana na mwanamke mwingine aliyejifanya ni daktari, na kuanza kujaza mwili wake kwa saruji, gundi ya kuzibia matairi na mafuta. Msichana huyo alilipa dola mia saba ili kupatiwa hips ba makalio ya kuvutia.

Hata hivyo sindano za mchanganyiko wa saruji, na mafuta na gundi zilimsababishia maumivu makali na akalazimika kwenda hospitali. Kila alipokwenda hospitali kutokana na maumivu alikuwa akiona aibu kusema hasa chanzo cha maumivu yake.

Hata hivyo mama wa msichana huyo alimbana mwanaye hadi akasema kilichomsibu. Polisi walimkamata daktari huyo feki na kumshtaki kwa kosa la kufanya udaktari bila leseni na pia kusababisha maumivu.

Mamlaka za huko zinasema huenda kuna wasichana wengine wengi wamekubwa na jambo hilo lakini wanaona aibu kujitokeza.

DOLA KIBAO

Haki miliki ya picha RIA Novosti
Image caption Mabunda ya noti

Sanduku moja linalodhaniwa kuwa na dola milioni moja liliachwa katika mgahawa mmoja mjini Sydney Australia na kusababisha tafrani.

Wamiliki wa mgahawa huo, walidhani sanduku hilo ni bomu na hivyo kuliweka nje na kuita polisi. Watu walioshuhudia wamesema waliona polisi wakifungua sanduku hilo kwa tahadhari na kukuta mabunda ya noti za dola za Kimarekani.

Taarifa zinasema inawezekana sanduku hilo liliachwa na awali mtu moja anayedhaniwa kuwa na umri wa miaka thelathini aliyeingia katika mgahawa huo na kuagiza kahawa.

Polisi wamegoma kuthibitisha ni kiasi gani cha fedha kilichokuwemo ndani ya sanduku hilo.

MBEGU ZA WIZI

Haki miliki ya picha other
Image caption Mapacha kama hawa

Bwana mmoja nchini Marekani amedai kuwa mpenzi wake za zamani amemuibia mbegu zake za kiume, na sasa anakishtaki kituo kimoja cha afya kilichomsadia msichana huyo kupaa uja uzito.

Bwana huyo Joe Pressil amesema aligundua kuhusu mpango huo baada ya kupokea risiti kutoka katika kituo cha afya ikionesha kuwa yeye ni mteja wao, kimeripoti kituo cha TV cha KPRC cha Houston.

Bwana Pressil alishangaa kuona msichana wake alipata uja uzito miezi mitatu baada ya wawili hao kauchana. Bwana huyo amesema msichana huyo miaka yote wakiwa pamoja alikuwa akidai kuwa hawezi kupata uja uzito kutokana na sababu za kiafya.

Msichana huyo hatimaye alijifungua watoto mapacha na kumtaka bwana huyo kulipia gharama za watoto, baada ya vipimo vya damu kuonesha yeye ndio baba.

Bwana huyo amesema sasa anakumbuka kwa nini mpenzi wake huyo alikuwa akisisitiza kwenda kutupa mipira ya kiume kila baada ya wao kukutana.

Na kwa taarifa yako.....

Chakula pekee mende wasichokula ni matango

Tukutane Wiki Ijayo.... Panapo Majaaliwa...

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali duniani